Advertise Here

Saturday, March 8, 2014

Rais Uhuru Kenyatta avutiwa na Uimbaji wa Rufftone.

kenyaatta
Rais Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye siku chache zilizopita ameonesha nia yake ya wazi wazi ya kuutangaza zaidi Muziki wa Kenya, amekiri kuwa anapenda sana Mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini humo Rufftone.

Kupitia mahojiano yaliyofanywa na Easy Fm, Katibu wa Mawasiliano na msemaji wa Rais wa Kenya Manoah Esipisu amesema kuwa Rais Kenyatta anaupenda sana Muziki wa Kenya, na kuwa Rufftone ndiye Mwimbaji anayempenda zaidi.

Rufftone ni moja mojawapo kubwa sana Nchini Kenya kwenye tasnia ya Muziki wa Injili, ambaye anafanya vizuri sana kwa sasa kupitia Wimbo wake wa "Mungu Baba" ambao alipata fursa ya kuuimba wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Kenya. Huku Kaka yake Daddy Owen akiendelea kufanya vizuri pia katika tasnia ya Muziki wa Injili Nchini Kenya.

Friday, March 7, 2014

Askofu Zygmunt Zimowski azindua mradi wa kupima na tiba kwa wagonjwa wa Ukimwi Mkoani Shinyanga.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya, hivi karibuni, alizindua mradi wa kupima na tiba kwa wagonjwa wa Ukimwi, Jimbo Katoliki Shinyanga, Tanzania.

Ni mradi unaoendeshwa kati ya Mfuko wa Msamaria mwema, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Kampuni ya dawa kutoka Marekani ijulikanayo kama Gilead Sciences.

Zaidi ya watu 120, 000 wanatarajiwa kufaidika na mradi huu inayojikita katika: sheria na kanuni za tiba; maadili na utu wema. Watoto yatima watapewa kipaumbele cha pekee.

Mradi huu ni kielelezo cha mshikakano wa dhati katika mchakato wa kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili unaofanywa na Makanisa mahalia kama sehemu ya Uinjilishaji wa kina. Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya linapenda kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika Jimbo Katoliki la Shinyanga.

Hizi ni juhudi zilizofanywa kwa ushirikiano mkubwa kati ya Marehemu Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga pamoja na Monsinyo Jean Marie Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya, ambaye mara kadhaa alitembelea Tanzania ili kuangalia uwezekano wa utekelezaji wa mradi huu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wa Ukimwi nchini Tanzania.

- Radio Vaticana - 

Tuesday, February 25, 2014

Safu ya James Kalekwa: Mwisho tangu Mwanzo: Usuri wa njozi kwenye maisha binafsi Part 3


James Kalekwa
Kufuatilia sehemu ya pili ya somo Bofya Hapa

Njozi huweka boma au mipaka ya kieneo au aina ya watu unaopaswa kuwahudumia.
Ukiisoma vyema njozi ya mtume Paulo kwenye Matendo ya Mitume 26:15-18 ambayo yeye huiita “maono ya mbinguni” utagundua ya kwamba kuna aina fulani ya watu ambao Paulo anatumwa kwao, “… nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao…”  Wagalatia 2:7, “bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa.” Kutahiriwa na kutokutahiriwa ni lugha iliyotumika kueleza wayahudi (wanaotahiriwa) na watu wa mataifa (wasio tahiriwa)… Lugha ina mzizi toka kwenye agano la Mungu na Ibrahimu ambalo liliwekwa kwa tohara kwahiyo kutahiriwa kukawa ishara ya kuwa mtu yu katika agano na Mungu, Yehova. Kwahiyo mtume Paulo anapokea njozi maalum kwa ajili ya watu wa mataifa - hakuwa mtume kwa ajili ya watu wote!
Moyoni mwangu nilikuwa na maswali mengi sana ya kwamba ni kwanini Mungu anaachilia njozi ndani ya watu kwa ajili ya eneo fulani la kijiografia ama kwa ajili ya aina fulani ya watu? Wakati nikitafakari juu ya hayo ndipo ufahamu ukaniijia ya kwamba Mungu pekee ndiye Alfa na Omega; mwanzo na mwisho yaani hana mwanzo wala hana mwisho na pia Mungu yupo kila mahala kwa wakati mmoja (omnipresent). Lakini mwanadamu kwa asili anafungwa na hayo… Hawezi kuwepo kila mahala, kila wakati; hawezi kuwa kila kitu kwa kila mtu! Hivyo ni lazima mipaka hiyo iwe ndani ya njozi laasivyo njozi haitatimia… haitaufikilia mwisho wake!
Muhubiri 10:8 anasema mtu atakaye bomoa boma (boma la wakati na kijiografia ama asili fulani ya watu) nyoka atamwuma! Hebu tusome hii kwenye maandiko kisha tujifunze jambo katika mifano hiyo. Ndani ya kitabu cha Waamuzi sura ya 13 mpaka sura ya 16 kuna habari ya ndugu mmoja anaitwa Samsoni ambaye Biblia inamweleza kama mnadhiri wa Mungu. Ukisoma utaona jinsi Roho wa Mungu alivyokuwa akimshukia kwa nguvu… nguvu za kimwili kwasababu kusudi la kuzaliwa kwake lilikuwa ni kuwakomboa waisraeli kutoka kwenye uonevu wa Wafilsiti; kwahiyo ilikuwa ni sababu ya kivita hivyo alizihitaji nguvu hizo Waamuzi 13:5, “Kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.”. Hapo nimetamani uone kutoka kwenye maandiko jinsi malaika alivyoeleza lengo la kuzaliwa Samsoni. Kusudi lililonyuma ya kuzaliwa na kuishi kwa Samsoni… Hiyo ndiyo ilikuwa njozi ya maisha yake binafsi iliyounganikana na maisha ya taifa lake! 


Ukisoma habari zake kwenye sura nilizozitaja hapo juu utagundua kuwa karibia mara zote Samsoni alizitumia nguvu zake kutetea mahusiano (mapenzi) yake… Basi! Na mbaya zaidi ni kwamba Samsoni alienda kuoa nje ya taifa la Israeli kwahiyo alipokuwa anatumia nguvu zake kutetea mahusiano yake alikuwa ni nje ya kusudi la kuzaliwa kwake (out of scope). Alikuwa anatumia kitu sahihi kufanya kitu kisicho sahihi… Alitumia nguvu alizopewa na Mungu kuwapiga maadui wa taifa la Israeli; lakini kilichomsukuma kupigana na maadui haikuwa ni ukombozi wa taifa. Kwa maana nyingine ni kwamba mahusiano ilikuwa ni mlango wa kutokea (exit door) wa Samsoni na bila kujua alijikuta yuko nje ya boma. Alianza kupigana kukomboa mahusiano yake na kumbe Mungu alimkusudia apigane kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti. Hivyo alitumia nguvu nyingi sana lakini nje ya boma. Mwisho wake ulikuwa ni kutobolewa macho na kuteswa na Wafilisti kwa kupanga njama na mkewe Delila. Samsoni alikufa kifo cha kimasikini sana (alikufa akiwa mtumwa, akiwa ametobolewa macho, pasipo kutimiza ukombozi aliokusudia Mungu)! Alienda nje ya mipaka, alienda nje ya boma, alienda nje ya “scope” ya njozi yake. Kanuni inasema “…na mwenye kubomoa boma, nyoka atamwuma.”


Kuna mtumishi mmoja wa Mungu alitoa ushuhuda ambao uliyagusa maisha yangu sana. Ndugu huyo ameitwa na Mungu kufundisha neno la Mungu kwa watoto wa Mungu ili wakue katika kumjua Mungu na ameitwa maalum kwa ajili ya watu wa taifa husika barani Afrika. Udhihirsho wa Mungu ni mkubwa katika mafundisho yake! Watu wa nchi moja ya Amerika ya Kaskazini wakapenda sana huduma yake na wakatamani sana kufanya naye kazi ya Mungu. Wao walimuandalia kanisa kulea kama mchungaji wa kanisa la mahala husika na kuwa askofu wa hilo dhehebu. Walimwandalia malipo mazuri, nyumba nzuri na uhakika wa watoto wake kusoma, angepata huduma za afya, bima n.k (social security). Lakini jibu la yule mtumishi wa Mungu wa nchi ya Afrika ni kwamba angeenda kuhudumu nao wale watumishi, angekuwa nje wa “boma” la wito wa huduma yake. Angekuwa nje ya kusudi/njozi ya utumishi alioitiwa… Asingekuwa mwalimu wa neno la Mungu kama alivyo Afrika, kule angekuwa mchungaji na askofu na angekuwa mbali na watu alioitiwa kuwafundisha. Kama Paulo alivyoitwa kwa ajili ya watu wa mataifa, mtumishi yule aliitwa kwa ajili ya watu wa taifa lake la Kiafrika! Angebomoa boma la njozi yake… Nini kingetokea? “…na mwenye kubomoa boma, nyoka atamwuma.” Nilijifunza jambo la msingi sana kuhusu njozi katika ushuhuda huu. Watu wengi wangeweza kutoa visingizio kuwa “si unajua Mungu ni yule yule… si unajua kote, Amerika na Afrika, ni shambani mwa Bwana?... Si andiko limetuagiza twende ulimwenguni mwote?”. Kumbuka nilichokufundisha juu ya mipaka imbatanayo na njozi… Huwezi kuwa kila mahala kwa wakati mmoja, huwezi kuwa kila kitu kwa wakati mmoja na huwezi kuwepo milele hapa duniani. Visingizio vyote hivyo, tena ndugu wengine hutumia maandiko kuhalalisha utovu wa kinidhamu juu ya njozi (manipulation). Lakini hiyo haizuii ukweli kwamba nje ya boma ni kutafuta “kutobolewa macho.” Mungu akusaidie kuelewa jambo hili muhimu sana!

Somo hili litaendelea Jumatatu ijayo
Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa neno la Mungu. 
+255 714 762 669
+255 754 917 764
jameskalekwa@gmail.com

Mfahamu kiundani Mwimbaji Neema Decoras kutoka Tanzania.

Neema Decoras
Neema Decoras (Amezaliwa Tarehe 27 Julai 1984) ni mwimbaji na mtunzi wa nyimbo za Injili za Kikristo mwenye kipawa na hodari kutoka nchini Tanzania ambaye amejitoa kuwa chombo imara cha Uinjilisti na kutumikia kusudi la Mungu katika wakati wake. Alizaliwa katika jiji la Mbeya, Tanzania na ni watatu kuzaliwa katika familia ya watoto saba.

Neema Decoras ambaye kwa sasa ni mama wa watoto wawili wa kike na mke mpendwa wa mume mmoja alianza uimbaji wa nyimbo za injili akiwa mdogo sana katika shule ya Jumapili ya Kanisa La Pentekoste Tanzania (KLPT) kabla ya kuokoka na kubatizwa na mchungaji Mwakanyamale wa Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) ya Ilembo, Airport, Mbeya.

Neema Decoras aliendelea na huduma ya uimbaji katika kipindi chote alichokuwa akisoma, kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Akiwa anachukua elimu ya sekondari alikuwa mwanachama na mwalimu wa kwaya ya Christ's Ambassadors Students Fellowship Tanzania (CASFETA) katika shule yake na muimbaji wa nyimbo za kusifu na kuabudu katika kikundi cha kusifu na kuabudu na Kwaya ya Tumaini ya Kanisa La Pentekoste Tanzania (KLPT). Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanza kuwa na haja ya kukitumia kipawa cha uimbaji na utunzi wa nyimbo na kufanya huduma ya uimbaji kama muimbaji wa kujitegemea.

Haja ya kuwa muimbaji wa kujitegemea ilianza kutimia mwishoni mwa mwaka wa 2012 Neema Decoras alipofanikiwa kurekodi wimbo wake uitwao “Mungu ni Mwema” katika studio iitwayo Twins Records iliyopo Riverside, Ubungo jijini Dar es Salaam chini ya mtayarishaji wa muziki aitwaye Gabriel Maulana.

Mnamo January mwaka wa 2013 mume wake alimpeleka kwa mtayarishaji wa muziki aitwaye Ambangile Mbwanji anayejulikana sana kama Amba ambaye ni mmiliki wa studio iitwayo Amba Records iliyoko Ukonga, Jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Katika studio hiyo alifanikiwa kurekodi na kutoa albamu yake ya kwanza mwezi Julai mwaka wa 2013. Albamu hiyo iitwayo “Milele Nitalisifu Jina Lako” ina nyimbo nane ambazo zote ameziimba kwa lugha ya Kiswahili. Nyimbo zilizomo katika albamu hiyo ni; Milele Nitalisifu Jina Lako, Mikononi mwa Mungu, Unapojaribiwa, Nione Leo, Mungu ni Mwema, Rejea kwa Yesu, Ninaimba Sifa na Hakika Nimejua.

Akiongozwa na Neno kutoka katika Zaburi 145:1-2 “Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, Nitalihimidi Jina lako milele na milele. Kila siku nitakuhimidi, Nitalisifu Jina Lako Milele na Milele” Neema Decoras anasema kamwe hawezi kuacha kulisifu Jina la Bwana kwa kuwa Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana.

Kwa sasa Neema Decoras anaishi jijini Dar es Salaam ambapo amefanya maonyesho yake mengi sana japo yuko tayari kutumika katika Ibada, Matamasha na Mikutano ya Injili, Semina, Sherehe, na matukio mbalimbali ambayo yanahubiri Neno la Mungu popote pale ndani na nje ya Tanzania.

Sikiliza Wimbo wake huu wa Milele Nitalisifu Jina lako Bwana
 

Wasiliana Nae Sasa
Simu: +255 658 027 515

Dini yazuia wananchi kwenda hospitali na sekondari.

DINI mpya iitwayo Matengenezo inayozuia waumini wake kwenda sekondari na hospitali, imeingia wilayani Kakonko mkoani Kigoma. Inakataza waumini wasiende sekondari na hospitali, kwa madai kuwa Biblia inawakataza kufanya hivyo. Mkuu wa Wilaya hiyo, Peter Toima alibaini hayo juzi katika Kijiji cha Rumashi Kata ya Nyabibuye wilayani humo.

Alikuwa kwenye ziara katika shule za sekondari za wilaya hiyo mpya, ambapo kwanza aligundua wanafunzi wengi hawajaripoti shuleni kuanza Kidato cha Kwanza.

Toima alipohoji kulikoni hawajaripoti katika shule walizopangiwa huku wale walioandikishwa darasa la kwanza, pia nao hawaripoti, alielezwa kuwa sababu za kiimani zinazokataza wengine kusoma.

Mkuu huyo wa Wilaya alikatiza ziara yake na kuanza msako wa kuwasaka wanafunzi hao ambao hawajaripoti shuleni pamoja na waumini wa dini hiyo ya Matengenezo.

Alisema aliamua kufanya hivyo, kwa sababu dini hiyo inawakosesha watoto haki yao ya msingi na kukiuka sheria za nchi, kwani ni haki ya kila mtoto kupata elimu.

Katika msako huo, aliongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo na watendaji wa Halmashauri wakiwemo Maofisa Elimu Msingi na Sekondari.

Viongozi hao walifika katika familia ya Mchungaji wa Kanisa la Matengenezo, Medad Laurent (40). Baada ya kufika hapo, Toima aliwakuta mabinti watatu waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka huu lakini hawajaenda, kutokana na kile Mchungaji huyo alichodai kuwa sekondari wanafundisha uongo, kinyume na maandiko matakatifu yanavyosema.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya aliamuru Mchungaji huyo na mabinti zake wawili, kushikiliwa na Jeshi la Polisi huku utaratibu wa kuwapeleka mabinti hao shule ukiendelea. Pia, aliamuru Mchungaji huyo kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za elimu.

Siku iliyofuata Toima na Kamati ya Ulinzi na Usalama, walifanya kikao na kukubaliana kuwapeleka mabinti hao, Naomi Medard (16) na Anastazia Medard (14) katika shule za sekondari zenye mabweni kwa kuwatenganisha ili wasiendelee kusambaza sumu ya kukataa shule.

Naomi alipelekwa Shule ya Sekondari Nyamtukuza na Anastazia Shule ya Sekondari Kanyonza. Hata hivyo, katika familia hiyo binti mmoja Beatrice Merdad (19) alibaki nyumbani kwa madai kuwa hakuchaguliwa kuendelea na Kidato cha Kwanza.

Alidai kuwa hata angechaguliwa, asingeweza kuendelea kwani wanafundisha uongo na siku akifa hatakuwa na la kwenda kumwambia Muumba wake, kutokana na elimu hiyo ya dunia kuwapotosha.

Katika familia hiyo ya watoto saba, wawili walifariki dunia kutokana na kutokwenda hospitali. Mama wa watoto hao, Julitha Sebastian (39) alipohojiwa baada ya mtoto wake mchanga kuonekana kudhoofika na nywele kubadilika rangi, alisema kuwa dini yao haiwaruhusu kwenda hospitali.

Alisema hakuwahi kumpatia mtoto huyo chanjo ya aina yoyote wala hakuwahi kujifungulia hospitali. Kuhusu watoto wake waliokufa, alisema Biblia inasema “Ni heri wafao katika Bwana”.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya hiyo, Florida Gandye alisema waumini wa kanisa hilo, awali walikuwa Wakristo Wasabato, kisha wakajiengua na kuanzisha dini hiyo yenye imani za ajabu.

- Habari Leo -