WAKATI viongozi wa madhehebu ya dini ya Kikristo nchini,
wakionekana kushindana kwa utajiri, hali inayowafanya waishi `kifalme’
na kufungua miradi, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima amesema hana mpango wa kufungua biashara, zaidi ya
kujikita na mahubiri ya Injili.
Aidha, amesema Mungu anaendelea kumbariki katika kazi yake, ndiyo
maana mambo yake yanamnyookea, akitolea mfano kuwa baada ya kumiliki
nyumba, magari na fedha za kutosha, sasa amembariki na kumpa helikopta
atakayoitumia kufikia waumini wake wa ndani na nje ya nchi.
Usafiri huo wa angani, utaongeza idadi ya vyombo vya usafiri vya
Mchungaji huyo, ambaye anatajwa kuongoza kwa utajiri miongoni mwa
viongozi wa madhehebu ya Kikristo nchini, kwani anamiliki magari kadhaa,
likiwamo lakifahari aina ya Hummer lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni
200.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni kwa simu, Gwajima ambaye
alikuwa anaendesha mikutano ya kueneza Neno la Mungu katika mikoa
mbalimbali ikiwamo Kilimanjaro na Tanga, alisema helikopta
imeshanunuliwa na matarajio yake ni kwamba, baada ya kukamilika taratibu
zote za kisheria nchini, itawasili.
“Sipendi kusema mambo yangu sana, lakini kwa kuwa umeuliza naweza
kugusia kidogo, ni kweli nina mpango wa kuanza kuhubiri Injili kwa
helikopta, na kama ilivyo kwa gari, nayo hii nimepewa na watu wa Mungu
walioguswa na huduma yangu Japan."
“Itafika nchini wakati wowote mambo ya kisheria yakikamilika, huu si
wakati wa kuizungumzia sana maana bado haijafika,” alisema Gwajima
ambaye gari lake aina ya Hummer liliwahi kuzua gumzo, wengine
wakimhusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ingawa anapuuza
madai hayo.
Mchungaji Gwajima, alieleza wazi kuwa utajiri wake unatokana na
baraka anazopewa na anaowahudumia ndani na nje ya nchi na pia kazi yake
ya kufundisha anayoifanya ughaibuni.
Aidha, kutokana na utajiri anaosema unatokana na baraka za Mungu,
Mchungaji Gwajima anamiliki nyumba ya ghorofa nne eneo la Mbezi Beach
katika Manispaa ya Kinondoni, ingawa haijakamilika.
Pia, amewanunulia wachungaji wake 40 magari ya kutembelea kwa bei
tofauti, yakiwamo ya chini ya Sh milioni 10 na mengine ya zaidi ya Sh
milioni 20.
“Lakini nina wachungaji wa ngazi mbalimbali, hawa ni wale wa juu,
wengine wachungaji wadogo wapo zaidi ya 670, hawa ni watenda kazi muhimu
na wanatofautiana kwa ngazi zao, ndiyo maana kazi ya Mungu inasonga
mbele hata nisipokuwapo,” alisema.
Mbali na magari ya wachungaji, pia amenunua mabasi 20 ya kubeba
waumini kutoka na kwenda kanisani, yakianzia maeneo mbalimbali ya Jiji
la Dar es Salaam.
Alithibitisha kuwa, kila moja limegharimu kati ya Sh milioni 80 na
100. Mbali ya Mchungaji Gwajima, viongozi wengine wa makanisa wanaotajwa
kuwa na utajiri mkubwa wa mali na fedha ni Nabii na Mtume Josephat
Mwingira wa Kanisa la Efatha anayemiliki benki, mashamba makubwa na mali
nyingine, Mchungaji Getrude Lwakatare wa Mikocheni B Assemblies of God
anayemiliki mtandao wa shule za St. Mary’s nchini.
Wengine ni Askofu Zachary Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible
Fellowship, Anthony Lusekelo `Mzee wa Upako’ wa Kanisa la Maombezi `GRC’
na Mtume Onesmo Ndegi wa Kanisa la Living Water Center ‘Makuti Kawe’.
- Habari Leo -