JAMBO LA TANO
Uamuzi wa kuoa au kuolewa, unaweza ukabadilisha
utumishi wako na wito wako kabisa
Uamuzi wa kuoa au kuolewa, unaweza ukabadilisha
utumishi wako na wito wako kabisa
Ngoja nikutolee mfano wa kibiblia. Unamkumbuka mtu mmoja aliyeitwa
Samson, alimwoa dada mmoja aliyeitwa Delila, utumishi wake ulinyongewa
huko kwenye maisha yao ya ndoa. Ukisoma kile kitabu cha Waamuzi.16:21
kinasema hivi, “Wafilisti wakamkamata wakamng’oa macho, wakateremka naye
mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba naye alikuwa akisaga ngano
katika gereza”.
Unajua huyu alikuwa ni mtumishi wa Mungu mzuri kabisa. Lakini hakujua
ya kwamba yule mwanamke aliyempenda na akamwoa aishi naye alikuwa ni
‘ajenti’. Hakujua ya kuwa yule dada alikuwa ni ‘ajenti’ wa adui. Yule
dada alikuwa ni ‘ajenti’; kabisa akambembeleza mume wake amweleze siri
ya nguvu zake, lakini Samsoni mwenyewe alikuwa anaficha kusema siri ya
nguvu zake iko wapi. Lakini yule dada alikuwa na ujuzi wa kubembeleza.
Akambembeleza yule baba kiasi ambacho akashindwa kuficha siri yake, na
akaisema.
Unajua inapofika kwenye masuala ya ndoa inatakiwa muweze kusaidiana,
mtu asitumie udhaifu wako kukuangusha, mtu asitumie udhaifu wako
kukuzamisha, mtu asitumie makosa yako kukupeleka jehanamu, inatakiwa
ukimpata mwenzako ukiwa na udhaifu akusaidie, ukiwa kwenye dhambi
akuombee utoke, unaelekea jehanamu akusaidie kwenda mbinguni, ndivyo
inavyotakiwa iwe kwenye ndoa.
Lakini ninakuambia ukimpata mtu, na wewe una maisha yanayoelekea
jehanamu, anakuambia nenda salama, hii ni hatari. Yule dada alikuwa
anamfuatilia Samsoni kumnyang’anya kitu kilichokuwa ndani yake cha
utumishi alichokuwa amepewa na Mungu, na Samsoni hakujua. Alipofika
mahali pa kuisema siri yake alifikiri mke wake ni mwenzake ambaye
anaweza akampa siri yake vizuri bila shida.
Ndio maana kwenye ndoa ambazo watu hawaaminiani vizuri, siri zao
hawaambiani. Na ikishafika kwenye ndoa, mnasiri mlizozifichana iko
shida, maana yake kuna eneo ambalo usingetaka liingiliwe, unafunga na
ufunguo, kasha unatembea na ufunguo mfukoni. Ni eneo umeficha, kwenye
ndoa mnatakiwa mfahamiane kila siku, na udhaifu wako, na shida ilioko,
na matatizo yaliyoko, kila kitu kiwepo peupe, ili mwenzako atafute namna
ya kukusaidia.
Samsoni aliona kitu cha tofauti, lakini alikuwa mke wake, maadui
wakaja wakamshika, mke wake anatazama na kushangilia. Badala ya Samsoni
kumtumikia Mungu, akaenda akawa anasaga ngano gerezani. Biblia inasema
wakamtoboa macho. Kwa jinsi ya rohoni ningekuambia, wanaondoa macho
yako ya rohoni, maono ya Kimungu yanapotea, mtazamo wa Kimungu unapotea,
mipango ya Kimungu inapotea.
Ndio maana unakuta mtu ameolewa ameokoka, au ameoa huku ameokoka,
akifika ndani ya ndoa maono ya Kimungu yanapotea, na utumishi wake
unazama. Anabaki kusema ‘Bwana asifiwe’, kama bado anaweza akaendelea
kusema ‘Bwana asifiwe’, lakini ndani ya moyo amenyonywa kiroho na hakuna
kitu.
Sasa labda na ninyi ni mashahidi, wewe angalia vijana ambao wameoa na
kuolewa, angalia kama bado wanao moto ule ule wa utumishi, ambao
walikuwa nao kabla hawajaingia kwenye ndoa. Wengine wanabaki
kumsingizia Mungu ya kuwa, ameesbadilishia huduma, wakati sio Mungu,
kumbe ni mume wake amembadilishia huduma, au ni mke wake tu
amembadilishia huduma! Maana hakuhesabu gharama ya ndoa kwenye wito
wake.
Kwa mfano; Mke wako anakutaka nyumbani, huduma inakutaka kila siku
uwepo barabarani, usije ukafikiri ni kitu kirahisi hicho. Utafika mahali
lazima uamue, unataka kumpendezesha mke wako au unataka kumpendezesha
Mungu.Haya si mambo ambayo ni rahisi kuyaweka vizuri na kuyaanisha bila
msaada wa Mungu. Na kama alikuwa anajua anaolewa wapi, kusumbuliwa suala
la kusafiri kwako kwenye huduma lisingekuwepo, angekua anakutia moyo na
kukuombea, na kukusindikiza siku nyingine. Lakini inapofika anaanza
kupata shida, maana yake kuoana kwenu kuna kasoro mahali, na kumekuwa
mzigo.
Somo hili bado linaendelea. Usikose sehemu ya Sita ya somo hili hapo kesho.