Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ) Dayosisi ya Kaskazini limeitaka serikali na jamii kwa ujumla kuweka sheria madhubuti zitakazowalinda watu wenye ulemavu dhidi ya unyanyapaa.
Katibu mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini bwana Julius Mosi ametoa kauli hiyo wakati akikabidhi viti mwendo nane kwa watu wenye ulemavu vilivyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Gabriella Children Rehabilitation center katika kijiji cha Uhuru kata ya Arusha chini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.
Bwana Mosi amesema kutokana na kuendelea kubaguliwa kwa watu wenye ulemavu na kunyimwa haki zao za msingi ni vyema serikali ikaweka mkazo wa kuwalinda watu hao ikiwa pamoja na kuwapatia elimu maalumu itakayowawezesha kutumia viungo vyao ili waweze kujitegemea.
Nae mkurugenzi wa shirika la Gabriella Children Rehabilitation centre lenye makao yake mjini linalojihusisha na utoaji huduma kwa jamii kwa watu wenye ulemavu Bi.Brenda Shuma, amesema shirika lake litaendelea kutoa misaada kwa watu wenye ulemavu ili kuwajengea uwezo wa kutumia viungo vyao katika kufanya kazi mbalilimbali za kujiletea maendeleo.