Advertise Here

Tuesday, February 25, 2014

Safu ya James Kalekwa: Mwisho tangu Mwanzo: Usuri wa njozi kwenye maisha binafsi Part 3


James Kalekwa
Kufuatilia sehemu ya pili ya somo Bofya Hapa

Njozi huweka boma au mipaka ya kieneo au aina ya watu unaopaswa kuwahudumia.
Ukiisoma vyema njozi ya mtume Paulo kwenye Matendo ya Mitume 26:15-18 ambayo yeye huiita “maono ya mbinguni” utagundua ya kwamba kuna aina fulani ya watu ambao Paulo anatumwa kwao, “… nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao…”  Wagalatia 2:7, “bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa.” Kutahiriwa na kutokutahiriwa ni lugha iliyotumika kueleza wayahudi (wanaotahiriwa) na watu wa mataifa (wasio tahiriwa)… Lugha ina mzizi toka kwenye agano la Mungu na Ibrahimu ambalo liliwekwa kwa tohara kwahiyo kutahiriwa kukawa ishara ya kuwa mtu yu katika agano na Mungu, Yehova. Kwahiyo mtume Paulo anapokea njozi maalum kwa ajili ya watu wa mataifa - hakuwa mtume kwa ajili ya watu wote!
Moyoni mwangu nilikuwa na maswali mengi sana ya kwamba ni kwanini Mungu anaachilia njozi ndani ya watu kwa ajili ya eneo fulani la kijiografia ama kwa ajili ya aina fulani ya watu? Wakati nikitafakari juu ya hayo ndipo ufahamu ukaniijia ya kwamba Mungu pekee ndiye Alfa na Omega; mwanzo na mwisho yaani hana mwanzo wala hana mwisho na pia Mungu yupo kila mahala kwa wakati mmoja (omnipresent). Lakini mwanadamu kwa asili anafungwa na hayo… Hawezi kuwepo kila mahala, kila wakati; hawezi kuwa kila kitu kwa kila mtu! Hivyo ni lazima mipaka hiyo iwe ndani ya njozi laasivyo njozi haitatimia… haitaufikilia mwisho wake!
Muhubiri 10:8 anasema mtu atakaye bomoa boma (boma la wakati na kijiografia ama asili fulani ya watu) nyoka atamwuma! Hebu tusome hii kwenye maandiko kisha tujifunze jambo katika mifano hiyo. Ndani ya kitabu cha Waamuzi sura ya 13 mpaka sura ya 16 kuna habari ya ndugu mmoja anaitwa Samsoni ambaye Biblia inamweleza kama mnadhiri wa Mungu. Ukisoma utaona jinsi Roho wa Mungu alivyokuwa akimshukia kwa nguvu… nguvu za kimwili kwasababu kusudi la kuzaliwa kwake lilikuwa ni kuwakomboa waisraeli kutoka kwenye uonevu wa Wafilsiti; kwahiyo ilikuwa ni sababu ya kivita hivyo alizihitaji nguvu hizo Waamuzi 13:5, “Kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.”. Hapo nimetamani uone kutoka kwenye maandiko jinsi malaika alivyoeleza lengo la kuzaliwa Samsoni. Kusudi lililonyuma ya kuzaliwa na kuishi kwa Samsoni… Hiyo ndiyo ilikuwa njozi ya maisha yake binafsi iliyounganikana na maisha ya taifa lake! 


Ukisoma habari zake kwenye sura nilizozitaja hapo juu utagundua kuwa karibia mara zote Samsoni alizitumia nguvu zake kutetea mahusiano (mapenzi) yake… Basi! Na mbaya zaidi ni kwamba Samsoni alienda kuoa nje ya taifa la Israeli kwahiyo alipokuwa anatumia nguvu zake kutetea mahusiano yake alikuwa ni nje ya kusudi la kuzaliwa kwake (out of scope). Alikuwa anatumia kitu sahihi kufanya kitu kisicho sahihi… Alitumia nguvu alizopewa na Mungu kuwapiga maadui wa taifa la Israeli; lakini kilichomsukuma kupigana na maadui haikuwa ni ukombozi wa taifa. Kwa maana nyingine ni kwamba mahusiano ilikuwa ni mlango wa kutokea (exit door) wa Samsoni na bila kujua alijikuta yuko nje ya boma. Alianza kupigana kukomboa mahusiano yake na kumbe Mungu alimkusudia apigane kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti. Hivyo alitumia nguvu nyingi sana lakini nje ya boma. Mwisho wake ulikuwa ni kutobolewa macho na kuteswa na Wafilisti kwa kupanga njama na mkewe Delila. Samsoni alikufa kifo cha kimasikini sana (alikufa akiwa mtumwa, akiwa ametobolewa macho, pasipo kutimiza ukombozi aliokusudia Mungu)! Alienda nje ya mipaka, alienda nje ya boma, alienda nje ya “scope” ya njozi yake. Kanuni inasema “…na mwenye kubomoa boma, nyoka atamwuma.”


Kuna mtumishi mmoja wa Mungu alitoa ushuhuda ambao uliyagusa maisha yangu sana. Ndugu huyo ameitwa na Mungu kufundisha neno la Mungu kwa watoto wa Mungu ili wakue katika kumjua Mungu na ameitwa maalum kwa ajili ya watu wa taifa husika barani Afrika. Udhihirsho wa Mungu ni mkubwa katika mafundisho yake! Watu wa nchi moja ya Amerika ya Kaskazini wakapenda sana huduma yake na wakatamani sana kufanya naye kazi ya Mungu. Wao walimuandalia kanisa kulea kama mchungaji wa kanisa la mahala husika na kuwa askofu wa hilo dhehebu. Walimwandalia malipo mazuri, nyumba nzuri na uhakika wa watoto wake kusoma, angepata huduma za afya, bima n.k (social security). Lakini jibu la yule mtumishi wa Mungu wa nchi ya Afrika ni kwamba angeenda kuhudumu nao wale watumishi, angekuwa nje wa “boma” la wito wa huduma yake. Angekuwa nje ya kusudi/njozi ya utumishi alioitiwa… Asingekuwa mwalimu wa neno la Mungu kama alivyo Afrika, kule angekuwa mchungaji na askofu na angekuwa mbali na watu alioitiwa kuwafundisha. Kama Paulo alivyoitwa kwa ajili ya watu wa mataifa, mtumishi yule aliitwa kwa ajili ya watu wa taifa lake la Kiafrika! Angebomoa boma la njozi yake… Nini kingetokea? “…na mwenye kubomoa boma, nyoka atamwuma.” Nilijifunza jambo la msingi sana kuhusu njozi katika ushuhuda huu. Watu wengi wangeweza kutoa visingizio kuwa “si unajua Mungu ni yule yule… si unajua kote, Amerika na Afrika, ni shambani mwa Bwana?... Si andiko limetuagiza twende ulimwenguni mwote?”. Kumbuka nilichokufundisha juu ya mipaka imbatanayo na njozi… Huwezi kuwa kila mahala kwa wakati mmoja, huwezi kuwa kila kitu kwa wakati mmoja na huwezi kuwepo milele hapa duniani. Visingizio vyote hivyo, tena ndugu wengine hutumia maandiko kuhalalisha utovu wa kinidhamu juu ya njozi (manipulation). Lakini hiyo haizuii ukweli kwamba nje ya boma ni kutafuta “kutobolewa macho.” Mungu akusaidie kuelewa jambo hili muhimu sana!

Somo hili litaendelea Jumatatu ijayo
Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa neno la Mungu. 
+255 714 762 669
+255 754 917 764
jameskalekwa@gmail.com