Advertise Here

Wednesday, February 19, 2014

Safu ya James Kalekwa; Mwisho tangu Mwanzo: Usuri wa njozi kwenye maisha binafsi. - Part 2

James Kalekwa
Msisitizo wa mwenendo wa somo:
Kusudi – ni sababu kuu ya kuwepo kwako. Hii hujibu swali la “Kwanini ninaishi?” mfano: Ninaishi ili kuudhihirisha utukufu wa Mungu kwenye kizazi changu.

Maono – ni taswira/picha kubwa uionayo juu ya mwisho wa maisha yako. Ni mkusanyiko wa mwisho wa maisha yako. Hii hujibu swali la “ninakwenda wapi?” mfano: … Kumtukuza Mungu kwa kufanya ugunduzi, uvumbuzi na utatuzi chanya wa mahitaji ya kizazi changu.

Dhamira – ni namna gani utafanya ili kuyafikia maono hayo kivitendo. Hii hujibu swali la “Namna gani nitatekeleza?” Mfano: … Kufungua taasisi ya utafiti wa uwezo wa mwanadamu na uelimishaji wa vijana.

N.B Unaweza kuwa na dhamira zaidi ya moja… Hakuna ukomo ilimradi tu dhamira zinafanikisha ufikiaji wa maono yako.

Malengo/Mipango – ni kuweka namna/njia za kivitendo na zinazopimika ili kufanikisha dhamira yako/zako Mfano: … Kufanya usajili wa taasisi yangu ifikapo March 28 ili kuanza utendaji rasmi.

Mkakati – ni mchanganuo wa hatua kwa hatua na uratibu wa rasilimali ili kufanikisha malengo yako. Hii hujibu maswali mengi “Nifanye nini, nifanye wapi, wakati gani?...” Mfano:

Taswira: Chombo cha Kusudi
Moyoni mwangu nimewiwa kuweka jambo hili kwa msisitizo mkubwa sana juu ya “Chombo cha kusudi”. Jifunze kutoka kwenye taswira hiyo na kutafsiri kwenye maisha yako binafsi.

Usuri ni nini?
Usuri (essence) ni jibu moja juu ya mjumuiko wa maswali mengi juu ya jambo, hoja, kitu au mtu fulani. Ni mara nyingi sana utawasikia watu wakitoa maelezo ya kina juu ya utumizi wa kifaa fulani cha umeme. Na kwa wanafunzi ni jambo lililozoeleka kukariri tafsiri (definition) na sifa za kitu au jambo fulani. Kuna aina ya watu ambao huvutika kufahamu sifa za kimwonekano za jambo fulani pasipo kujua tafsiri au utumizi wake.

Kwa ujumla wake, usuri hujibu maswali yahusianayo na maana na tafsiri ya jambo, sifa za kimwonekano, utumizi na huenda mbali na kujibu kwanini jambo fulani lipo na ni kwanini lipo vile lilivyo!
Kwahiyo, usuri wa maono si tafsiri/maana ya maono, si sifa za maono, si mwonekano na wala si utumizi wa maono…. Bali ni mjumuiko wa hayo yote! Karibu ujifunze kwa upana na urefu ujumla wa jambo hili muhimu sana katika maisha ya mwanadamu yeyote.

Njozi (Maono) huleta “mipaka” ya maisha
Ili kuupanua wigo wa kujifunza na kuvuta maarifa kutoka katika andiko hili, nitaleta tafsiri mbalimbali za lugha ya kiingereza na kuzitafsiri ili kutusaidia kupata upana wa maana ya hekima hizi.
“Where there is no revelation, people cast off restraint…”  (NIV)
“Where there is no prophetic vision the people cast off restraint…” (ESV)
Tafsiri yangu ya ujumla “Pasipo maono, watu hukosa/huvuka mipaka…”
Ukisoma kwenye historia ya agano la kale utaona kuwa miji mikubwa ilikuwa imezingirwa na kuta kubwa sana kuilinda miji hiyo; Mfano mji wa Yeriko, Yerusalemu. Hata kwenye historia ya kale, nchi kama China ya kale (Ancient China) utaona ujezi wa ukuta wa namna hiyo, ukuta mkuu wa China (The Great wall of China) ni moja kati ya kuta maarufu sana za miji.

Sababu kubwa ya ujenzi wa kuta hizo ilikuwa ni kuleta ulinzi wa uhakika kwa waishio ndani ya kuta hizo dhidi ya maadui walio nje ya kuta hizo. Ukuta uliweka mipaka baina ya walindwao dhidi ya wasiolindwa na ukuta huo; raia dhidi ya maadui wa jamii husika.

Mhubiri 10:8, “Mwenye kuchimba shimo atatumbukia ndani yake; Na yeye abomoaye boma, nyoka atamwuma.”
Njozi huweka bayana mipaka ya mtu ama jamii ibebayo njozi hiyo. Kimsingi, njozi kama ilivyo ni mipaka tayari. Njozi inaweka ukuta wa muda na wakati (season) ya kukamilika kwake, kwahiyo unapaswa kujua kuwa huna muda wote duniani kutimiliza njozi hiyo… Njozi imefungwa ndani ya muda. Kwenye kitabu changu cha kwanza nimeeleza kwa upana na kwa lugha nyepesi kuhusu sifa ya muda ya njozi. Njozi zote zina ukomo wa muda na kuna sababu katika hilo.
Ukisoma Habakuki 2:3, “ Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwakuwa haina budi kuja, haitakawia.” Utaona Mungu anasema na huyu ndugu kitu cha msingi sana juu ya “wakati ulioamriwa” na anasisitiza kuhusu mitazamo miwili; mtazamo wa kibinadamu na mtazamo wa kiMungu.

Kwamba katika macho ya kibinadamu njozi inaweza kuonekana inakawia lakini katika macho ya Mungu ipo katika wakati kwakuwa haina budi kuja. Hebu tazama hii sentensi ambayo Roho Mtakatifu aliweka kwa msisitizo sana ndani ya moyo wangu “…ijapokawia, ingojee; kwakuwa haina budi kuja, haitakawia.”.

Ukitazama utagundua hii ni kama sentensi yenye kujipinga yenyewe kwasababu inazungumza mawazo mawili tofauti yasiyoafikiana “… ijapokawia…. haitakawia”. Kitu gani ninataka uone katika eneo hili ni tofauti ya kutazama muda wa njozi iliyomo ndani ya mwanadamu na Mungu. Isaya 55:8-9, “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu ya nchi.

Kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.” Mungu anataka kusema namna ya kufikiri kwake ilivyo tofauti na juu ya namna yetu. Rejea Mhubiri 3:1, “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.” Na muendelezo wa mifano ya kila jambo na wakati wake mpaka mstari wa 8.

Somo hili litaendelea Jumatatu Ijayo
  
Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764