Advertise Here

Sunday, March 31, 2013

Ibada ya Pasaka katika Kanisa la New Vine Christian Centre.

LEO katika Kanisa la New Vine Christian Centre, kulikuwa na Ibada ya Pasaka iliyofanyika Kanisani hapo kuanzia Saa 3:00 Asubuhi hadi Saa 5:45 Asubuhi.
Pastor Goodluck akiwa Madhabahuni
Hizi ni picha za baadhi ya matukio yaliyokuwa yakiendelea Kanisani hapo siku ya leo.
Baadhi ya Waimbaji wa NVCC Praise Team
Mtumishi Jema kama kawaida yake kwenye Keybord
Tenzi za Rohoni pia zilitumika kuleta Uwepo wa Mungu
Mmiliki wa Chombo cha Habari cha Mjap Inc, Baraka Samson akiwa Madhabahuni
Bila huyu Jamaa Setting ya Vyombo haijakamilika. Steve akiwa kwenye Mixer
Neno la Mungu lilitolewa na Mtumishi wa Mungu Eliud Mwasenga likiwa Kichwa Kinachosema, "Kuishi Maisha Mapya ndani ya Kristo".
Mtumishi wa Mungu, Eliud Mwasenga
Kanisa la New Vine Christian Centre lililoko Tema Hotel - ukumbi Mkubwa, Nyegezi Jijini Mwanza, chini ya Mtumishi wa Mungu Pastor Goodluck Kyara, huwa linakuwa na Ibada kila Jumapili kuanzia Saa 3:00 Asubuhi - Saa 5:45 Asubuhi.
Baadhi ya Watu waliohudhuria Ibada leo
Sikiliza sehemu ya Mahubiri ya Jumapili ya leo ya Pasaka yaliyotolewa na Mtumishi wa Mungu Eliud Mwasenga


Je! Ungependa kupata CD za Mahubiri haya ili ukue zaidi kiroho? Piga Simu sasa Namba; 0754 435951.

Sasa Tazama Sehemu tu ya Wimbo wa Kuabudu ulioimbwa na New Vine Christian Centre - Praise Team, katika Ibada ya leo ya Pasaka

Friday, March 29, 2013

Muuaji wa Padri Evarist Mushi akamatwa.

MTU anayesadikiwa kuwa ndiye Muuaji wa Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki Mjini Zanzibar, amekamatwa alasiri hii Maeneo ya Kariakoo Zanzibar.

Jeshi la Polisi limethibitisha kukamatwa kwa Mtuhumiwa huyo na kwenda nae kituoni kwa ajili ya Mahojiano zaidi.

Padri Evarist Mushi aliuawa Mwezi uliopita kwa kupigwa risasi akiwa kwenye gari lake kuelekea Kanisani kwenye Ibada ya Jumapili.

Tutakupasha habari kamili pindi zitakapotufikia. Endelea kutembelea Mtandao huu.

Source: Issa Michuzi

Wimbo Mpya wa Deitrick Haddon - Have Your Way.

Thamani ya Kifo cha Yesu pale Msalabani.

 
Shaloom Mpendwa!

Ni jambo la pekee tena kwa Mungu kutufikisha katika maadhimisho ya kumbukumbu za kifo chake na kufufuka kwake yaani pasaka. Kwa kifupi nimeona niandike ujumbe huu ili kukumbushana mambo muhimu kwa habari ya Pasaka.
   
Ni muhimu sana kukumbuka kwamba Yesu alikufa pale msalabani kwa sababu kubwa mbili moja ni ili kurejesha mahusiano ya Mungu na mtu kwa lengo la kumsaidia mtu aishi hapa duniani kwa kusudi la Mungu na pili ili tupate wokovu na kisha kuurithi uzima wa milele.

Biblia katika kitabu cha Mathayo 26:53-54 inasema ‘Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?’ Kutokana na andiko hili ni vema tukajifunza kwamba;
  • Upendo wake (Yesu) ndio uliomsukuma kuyatoa maisha yake kwa ajili yetu.
  • Yesu alikuwa na uwezo wa kuangamiza askari waliokuja kumkamata, lakini hakufanya hivyo ili andiko/kusudi la Mungu lipate kutimizwa.
  • Ndani ya ufahamu wa Bwana Yesu kulikuwa na mwanadamu, ndio maana kwa kuangalia ‘future’ ya mwanadamu na kusudi la uumbaji wa Mungu ilimlazimu kupitia njia ngumu ya msalaba ili atupate mimi na wewe.
Naam ndugu zangu tujiulize, ni upendo wa namna gani wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Biblia inasema katika kitabu cha Waebrania 2:1-3 Kwa hiyo imetupasa kuyaangalia zaidi hayo yaliyosikiwa tusije tukayakosa. Kwa maana ikiwa lile lililonenwa na malaika lilikuwa imara, na kila kosa na uasi ulipata ujira wa haki, sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wakovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia’

Katika kuendelea kuonyesha thamani ya kifo cha Yesu pale msalabani Yohana naye aliandika akasema ‘Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata  akamtoa Mwanawe pekee, ila kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye’ Yohana 3:16-17.

Jambo la muhimu ni kwamba Bwana Yesu alikufa na kufufuka ili awalete wengi kwenye ufalme wake. Hivyo basi mpenzi msomaji nakusihi usiichezee neema hii, nakusihi usomapo ujumbe huu wewe ambaye hujaokoka, fanya maamuzi ya kuokoka na wewe unayemjua Mungu maanisha katika wokovu wako.

Twaliabudu na kulisifu jina lako wewe uliyeutoa uhai wako kwa ajili yetu ee Bwana. Ahsante kwa siku njema ya leo ambayo Bwana umeifanya kwa ajili yetu ee Mungu.

Basi ndugu zangu tunapoadhimisha sherehe hizi za pasaka tusiifanye kazi ya Yesu pale msalabani kuwa ni bure, bali kuanzia sasa tusienende kama wamataifa waendavyo bali kama wana wa nuru.

Familia yangu pamoja nami tunawatakia heri ya pasaka, ‘Bwana Mungu awabarikie na kuwalinda’.

Mwl. Patrick Samson Sanga
+255 755 816 800

Wednesday, March 27, 2013

Kardinali Pengo atoa Mwongozo kwa Mapadri.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, akiendesha ibada takatifu ya kubariki mafuta ya Pasaka na kurudiwa kwa kiapo cha mapadri, iliyofanyika Jana katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph
KIONGOZI wa Kanisa  Katoliki nchini, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, amewataka mapadri wa Kanisa hilo kuwa kioo kwa matendo mema kwa kila wanachokifanya kwa wengine.

Kardinali Pengo aliyasema hayo jana wakati wa misa ya sherehe ya Sakramenti ya Upadri na kubariki mafuta ya Pasaka katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini humo.

Alisema ni lazima kuwa watimilifu wa kibinadamu kwa kupitia njia ya sadaka, mateso na kifo hivyo kuwataka kuwafundisha yaliyo mema na yenye kumpendeza Yesu Kristu.

“Ili kufikia ukamilifu hatuwezi kukwepa misalaba, waumini mnatakiwa kutuombea ili kuweza kumwakilisha Yesu Kristu kwa matendo yaliyo mema na ya kumpendeza,” alisema Kardinali Pengo.

“Hivi sasa  shida na mahangaiko ya dunia ni mengi  lazima  kumwonyesha Yesu ili aweze kutusadia na kushinda. Tukianza kuangalia chanzo cha matatizo na mahangaiko yalivyo hivi sasa hatuwezi kufika na tutaangamia,” alisema Kardinali Pengo.

Alisema njia nyingine zozote ambazo zinashabikia kama anasa na ukatili haziwezi kufanikiwa, hivyo aliwataka Mapadri hao kuwahubiria amani waumini.

- Mwananchi -

Facebook na Watumishi wa Mungu leo.

Nafasi za Kazi News of Victory International Magazine.

Kwa Wakristo Wote wa Madhehebu Yote
kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Congo DRC, Burundi, South Africa, 
Canada, U.K, U.S.A etc

1. Waandishi (Journalists)-  4 Posts
a.  Awe Ameokoka (Born Again Christian)
b.  Awe mwenye umri wa miaka 23- 45
c.  Mwenye kuweza kuandika na kuongea Kiswahili vizuri na Kiingereza
d.  Mwenye Shahada (Degree) ya  Uandishi kutoka Chuo kinachotambulika nchini au nje ya nchini

2. Sales and Marketing - 4 Posts
a.  Awe Ameokoka (Born Again Christian)
b.  Awe mwenye umri wa miaka 23- 45
c.  Mwenye kuweza kuandika na kuongea Kiswahili vizuri na Kiingereza
d.  Mwenye Stashahada (Degree) au Diploma ya Biashara na Masoko

3. Secretary and Administrator - 2 Posts
a.  Awe Ameokoka (Born Again Christian)
b.  Awe mwenye umri wa miaka 23- 45
c.  Mwenye kuweza kuandika na kuongea Kiswahili vizuri na Kiingereza
d.  Mwenye Diploma au Cheti cha Secretarial Katibu Muhtasi

4. Sales Representative - 10 Posts (Inside and outside Tanzania)
a.  Awe Ameokoka (Born Again Christian)
b.  Awe mwenye umri wa miaka 23- 45
c.  Mwenye kuweza kuandika na kuongea Kiswahili vizuri na Kiingereza
d.  Mwenye Degree au Diploma Biashara na Masoko

5. Distributor - 1 Post
a.  Awe Ameokoka (Born Again Christian)
b.  Awe mwenye umri wa miaka 23- 45
c.  Mwenye uzoefu wa kutosha unaozidi Miaka 2

6. Subscriber Officer - 15 Posts
a.  Awe Ameokoka (Born Again Christian)
b.  Awe mwenye umri wa miaka 23- 45
c.  Mwenye kuweza kuandika na kuongea Kiswahili vizuri na Kiingereza

7. Volunteers - 8 Posts (Inside and Outside Tanzania)
a.  Awe Ameokoka (Born Again Christian)
b.  Awe mwenye umri wa miaka 23- 45
c.  Mwenye kuweza kuandika na kuongea Kiswahili vizuri na Kiingereza

Tuma barua pepe ambatanisha CV na Nakala ya Vyeti vyako na tuma kwenye barua pepe: nicekennedy@gmail.com



Au fika katika ofisi zetu
AG PRESS HOUSE
Mbezi Beach Makonde Junction
Near Siloam Church
Kwa maelezo zaidi piga namba: +255 768 444 555

- Uncle Jimmy -

Solomon Mukubwa na Faraja Ntaboba wawasili Tanzania kwa Tamasha la Pasaka.

Mwimbaji Faraja Ntaboba kutoka DRC akizungumza kitu mbele ya Waandishi wa Habari Jana
WAKATI muimbaji Sipho Makhabane wa Afrika Kusini akitarajiwa kutua nchini siku ya Ijumaa wiki hii, waimbaji wa nyimbo za injili kutoka Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wamewasili jana jijini Dar es Salaa, tayari kwa ajili ya kushiriki katika Tamasha la Pasaka, litakaloanza Machi 31 kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati Maalumu inayoratibu tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama aliwataja waimbaji waliowasili jana kuwa ni Solomoni Mukubwa (Kenya) na Faraja Ntaboba (DRC).
Msama aliwataka wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa injili kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo, ambalo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ili kuunga mkono juhudi za kampuni yake kuandaa tamasha hilo kwa malengo mbalimbali ikiwemo kueneza injili ya Mungu na kusaidia makundi maalumu.
Mwimbaji Solomon Mukubwa kutoka Kenya
Kuhusu waimbaji, Msama alisema kuwa hadi kufikia Ijumaa, wakali wote wa nyimbo za injili kutoka nje watakuwa wamewasili jijini tayari kwa tukio hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Dar es Salaam na mikoa yote ambayo tamasha huilo litarindima.
 
Aidha, mkali wa aina hiyo ya muziki kutoka Kenya, Mukubwa, alisema kuwa amejiandaa vya kutosha katika tamasha la mwaka huu ambalo limebeba ujumbe wa Upendo na Amani.


“Wakati wa Uchaguzi wa Nchini Kenya tuliimba na kuhamasisha Amani na Upendo na kwa kupitia tamasha hili tutaimba nyimbo za kuhamasisha Amani na Upendo hapa Tanzania,” alisema Mukubwa.

Muandaaji wa Tamasha hilo, Bw. Alex Msama
Naye mwimbaji kutoka DRC, Ntaboba alisema kuwa, watu wajitokeze kwa wingi katika tamasha hilo na kupata burudani itakayokwenda sambamba na mafundisho ya dini.

Msama aliongeza kuwa idadi ya waimbaji imeongezeka baada ya kujitokeza kwa nyota mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Ntutuma kutoka Kenya, ambapo baada ya tamasha hilo kutikisa kwenye jijini Dar es Salaam, itakuwa zamu ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Mwanza kabla ya mashambulizi kuhimishiwa mkoani Mara.

Tuesday, March 26, 2013

Kanisa la Overcomers lamuandalia Tuzo Lowasa.

Waziri Mkuu wa Zamani, Edward Lowasa
KANISA la Overcomers lililopo mkoani Iringa, limeandaa tuzo maalumu kwa ajili ya kumtunuku Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, kutokana na mchango wake alioutoa katika jamii.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Boaz Sollo, alisema jamii ya wakazi wa Mkoa wa Iringa inatambua mchango wa Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli.

 
Dk. Sollo alisema kuwa tuzo hiyo itampa moyo wa kuendelea kushiriki zaidi katika shughuli mbalimbali za kijamii sambamba na kuiendeleza injili kama ambavyo amekuwa akifanya.

“Hii tuzo itamuongezea ujasiri wa kujituma katika kuisaidia jamii, sambamba na kuchangia ujenzi wa makanisa katika mikoa mbalimbali bila kujali wanaomkatisha tamaa ili kumrudisha nyuma.

“Tumeandaa tuzo maalumu kwa ajili ya kiongozi huyu ambaye haipiti wiki moja anasikika akifanya kazi za kijamii, habagui, hachagui na wala hana upendeleo,” alisema Dk. Sollo.

Aliongeza kuwa tangu alipojiuzulu uwaziri mkuu, hajawahi kuutembelea mkoa huo jambo linalowafanya wakazi wa mkoa huo kuwa na hamu ya kumuona kutokana na jitihada zake za kujihusisha katika masuala ya kijamii.

Alisema tuzo hiyo itatolewa mwezi ujao wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo na kituo cha redio ya dini ya Overcomers, ambayo ni maarufu kwa mikoa ya kusini.

Wakizungumza na Gazeti la Mtanzania kuhusu tuzo hiyo, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Iringa wamelipongeza kanisa hilo kwa kuandaa tuzo maalumu kwa ajili ya kutambua mchango wa kiongozi huyo.

- Mtanzania -

Kupotea kwa Askofu Mkoani Njombe, Utata watawala.

Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Moses Kulola
SAKATA la kupotea kwa Askofu wa Evangelism Assemblies of God Tanzania (EAGT), Lomanus Lukosi (60), anayeishi mjini Makambako Wilaya ya Wanging’ombe mkoa wa Njombe, limezua mkanganyiko kutokana na kauli zinazotolewa na kanisa hilo na Jeshi la Polisi.
 
Mkanganyiko huo unatokana na viongozi wa Jeshi la Polisi na kanisa hilo kwa nyakati tofauti kusema askofu huyo alipatikana jana na anawasiliana na familia yake kutoka sehemu alikojificha kwa ajili ya kufanya maombi ingawa hajaonekana hadharani.
 
Katibu Mkuu wa EAGT, Askofu Brown Mwakipesile, alisema baadhi ya viongozi wa kanisa hilo akiwamo katibu wa askofu huyo wamepewa jukumu la kushughulikia suala la kupotea Askofu Lukosi.
 
Alisema hadi jana Askofu Lukosi amekuwa akiwasiliana na familia yake kutoka mahali alikojificha kwa ajili ya maombi.
 
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Moses Kulola, alipotafutwa jana kuelezea tukio hilo, simu yake ilipokelewa na mtu ambaye alijibu kuwa askofu hajajulishwa na wasaidizi wake kuhusiana na tukio hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani, alisema  askofu huyo hajapatikana ingawa anaendelea kuwasiliana na familia yake akiwa katika eneo ambalo halijulikani.
 
Naye Mchungaji Asimbagwe Mwaisabila wa kanisa hilo, akizungumza na NIPASHE kutoka Sumbawanga alisema amewasiliana na viongozi wenzake waliopo Makambako ambao walimweleza kuwa amepatikana.
 
“Mimi ni mmoja wa watu tuliokuwa tunafuatilia suala hili, nimewasiliana na wenzangu wanasema askofu amepatikana ingawa sijafahamu kama ni kweli au la maana wanasema anawasiliana na familia yake,” alisema.

- Nipashe -

Nitamtambuaje Mke ambaye Mungu ameniandalia?

SWALI
Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu!
Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa ajili yenu kwa huduma mnayoitoa ambayo imekuwa msaada katika maisha yangu kama mkristo na kama mwanajamii. Mungu awabariki sana.


Pili naomba msaada wa maarifa juu ya namna ya Kumtambua mke ambaye Mungu ameniandalia. Nimefanya maombi ya kumuomba Mungu mke mwema tangu septemba 2008 hadi sasa lakini bado sijapokea majibu ya maombi yangu. Ninaamini ninasumbuliwa na Tatizo la upokeaji wa majibu ya maombi yangu jambo ambalo linahatarisha ustawi wangu kiroho.


Naomba kwa manufaa ya wengine pia ambao wana tatizo kama langu. Asante sana na Mungu awatimizieni haja za mioyo yenu na kuimarisha huduma yenu ili watu wengi zaidi waimarike kiroho.


Naitwa Lucas


Majibu;

Hello Lucas, tunakusalimu kwa jina la Bwana, ahsante kutuombea, kututia moyo na kwa swali lako ambalo naamini majibu yake yatawafaa wengi kama ulivyoshauri katika swali lako.


Kaka Lucas swali lako ni pana sana na ‘it is more personal’ kimajibu, lakini namshukuru Roho Mtakatifu anayeweza kutupa majibu ya kutufaa .Katika swali lako nimegundua mambo mawili ya msingi ambayo natakiwa kuyatolea ufafanuzi, moja ni namna unavyoweza kumtambua mke ambaye Mungu amekuandalia na pili namna bora ya kuomba yenye kuleta matokeo.


Katika kujibu maswali haya mawili nitazungumzia mambo manne yafuatayo ambayo naamini baada ya kuwa umeyasoma haya utapata ufahamu wa kukusaidia katika kufanya maamuzi hayo yanayokukabili;


Jambo la kwanza; Mungu hatumii njia au mfumo wa aina moja katika kukujulisha wewe mwenzi wa maisha yako (Isaya 55:8).

Oktoba 2006 naliandika kitabu kuhusu Njia kumi za Kibiblia zitakazokusaidia kumjua na kumpata mwenzi wako wa maisha. Katika ukursa wa nne wa kitabu hicho ndipo nilipoandika wazo hili hapo juu, kwamba, Mungu hatumii njia au mfumo wa aina moja katika kumjulisha mtu mwenzi wake wa maisha.


Nimeona hata sasa nianze na msingi huu na hii ni kwa sababu vijana wengi hujaribu kuuliza wanandoa waliotangulia kwamba waliwapataje wenzi wao wa maisha kwa dhana ya uongozi wa Mungu? Kutokana na majibu ambayo vijana hao hupewa wengi humuomba Mungu na wanasubiri, Mungu aseme nao kwa njia ile aliyotumia kusema na mtu mwingine.


Kibiblia wazo hili siyo sahihi kwani, Mungu ana njia nyingi sana za kusema na watu wake katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na nani atakuwa mwenzi wako wa maisha. Kwa mtu mmoja Mungu anaweza akasema naye kwa ndoto, mwingine kwa sauti yake, na mwingine kwa maono, mwingine kwa mafunuo, mwingine kwa amani ya Kristo, mwingine kwa kutumia watumishi/wachungaji nk

Jambo ninalojaribu kukuonyesha hapa ndugu Lucas ni kwamba ‘Mungu ana namna yake ya kukusaidia kumtambua mwenzi wako wa maisha, ambayo si lazima ifanane na ya mtu mwingine’.

Na mara nyingi namna/njia hiyo haitofautiani sana na ile ambayo Mungu hutumia kusema nawe katika mambo mbalimbali. Hivyo tafuta kujua njia ambayo Mungu huwa anatumia kusema na wewe katika mambo mbalilmbali, naam kwa hiyo aweza kusema na wewe hata kuhusu mwenzi wako.


Jambo la pili; Jenga na kuboresha mahusiano yako na Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu ndiye aliyepewa jukumu la kuwa Msaidizi wako hapa duniani katika kufanya maamuzi mbalimbali. Watu wengi leo wanakwama au wanajikuta wamefanya maamuzi mabaya kwa kosa la kutokumshirikisha Roho Mtakatifu awasaidie. Mwambie Roho Mtakatifu nahitaji mwenzi(Mke), nisaidie kumtambua yupi ni wa kwangu, naomba uongozi wako. Roho Mtakatifu kwa hakika atakuongoza katika njia sahihi (Zaburi 32:8).

Jambo la msingi ni kwa wewe kuboresha mahusiano yako na yake ili kuruhusu mawasilano mazuri kati yenu. Kumbuka mawasilano hutegemea mahusiano. Na jambo la msingi katika kuboresha mahusiano ni utakatifu na kutenga muda wa kuzungumza naye kwa njia ya maombi na neno.


Jambo la tatu; Jifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie kuhusu mwenzi wa maisha yako.

Hili ni jambo lingine la msingi kuzingatia. Endapo umeamua kufuata au kutafuta kumjua mwenzi wako kutoka kwa Bwana, basi ni vema ukaruhusu mapenzi yake juu yako yatimie. Wengi huenda mbele za Bwana wakimuuliza jambo hili lakini anapoleta wazo/jibu lake juu ya nani anafaa, wengi wakishamtazama huyo muhusika kimwili na kwa vigezo vyao humkataa na kusema si Mungu. Ni vizuri ukafahamu kwamba, kama Mungu ndiye aliyemleta mtu wa kwanza kwako na wewe kwa sababu zako binafsi ukasema huyu si wa kutoka kwa Bwana, maana yake umemzuia  Mungu asikusaidie kwenye hilo eneo, na hivyo usitegemee kusikia tena kutoka kwake, labda mpaka ujue kosa lako na kuomba toba.


Kumbuka usimuombe Mungu akujulishe mwenzi wako wa maisha wakati moyoni mwako tayari kuna mtu au watu ambao umeshadhamiria kutaka mmoja wao awe mwenzi wako, Mungu hawezi kusema hapo. Ikiwa unataka Mungu ahusike mpe asilimia mia moja hatafanya makosa kama Mwandamu.


Jambo la nne; Jifunze kuomba kimaswali

Najiribu kufikiri kwa nini umeomba tangu Septemba 2008 hadi sasa Mungu asijibu? Kwa ufahamu nilionao katika Kristo nina hakika yeye alisha-kujibu ila wewe ndiyo hukuelewa kwamba alijibu. Nina uhakika huo kwa sababu mtu amwendeaye Mungu kutaka kujua jambo, Mungu humjibu mtu huyo ili kumsaidia asipotee katika jambo hilo.


Naamini shida ipo kwako, huenda jibu ulilokuwa unataka wewe ni kuambiwa fulani ndiye mwenzi wako, kumbe kwa Mungu huenda alikuwa anasema huu si muda wake endelea kuomba maana kwa kila jambo kuna majira yake. Zaidi huenda shida iko kwenye namna unavyoomba na namna unavyopokea, au kuelewa Mungu anapoleta jibu.


Ili kuweza kupata ufumbuzi juu ya jambo hili jifunze kutumia mfumo wa maswali katika maombi yako, naamini utaona matokeo yake. Jifunze kuyatengeneza maombi yako kimaswali, omba huku ukitaka kujua/ukitafuta ufumbuzi wa lile unaloliombea kwa Mungu.

Swali limejibiwa na;
Mwl. Patrick Samson Sanga

+255 755 816 800

Sifa Group Foundation yahitaji Milioni 16 kusaidia Watoto yatima.

Mkurugenzi wa Sifa Group Foundation, Sifa John
Sifa Group Foundation ni taasisi iliosajiliwa kisheria, inajishugulisha na maswala ya kusaidia watoto yatima na watoto wa mazingira magumu. Pia kituo hiki husaidia vijana wasio na ajira ili wapate cha kufanya na wasiwe tegemezi.
Mkurugenzi wa Sifa Group Foundation, Sifa John akiwa Ofisini kwake
Kituo hiki kilichopo Bunju B, Mtaa wa Sun Nsiro - Jijini Dar es salaam na kilichoanzishwa na Mwimbaji wa Nyimbo za Injili toka Nchini Tanzania Sifa John, mpaka sasa kimekwisha saidia vijana kumi na tatu(13) kwa kuwapa mafunzo ya ushonaji na sasa wamejiajiri wenyewe. Vijana wengine saba(7) wamejua computer, na vijana wa tano(5) wanajishughulisha na miradi ya chips na vinywaji.
Darasa la Cherehani linalomilikiwa na Sifa Group Foundation
Pia kituo hiki kina jumla ya watoto 105 ambao ni yatima na wale wanaotoka kwenye mazingira magumu. Vijana hawa wanasaidiwa katika swala zima la elimu, chakula na mavazi. Na kwa wale ambao hawajawahi kusoma kabisa, kituo kimewatafuta walimu na kimeanzisha madarasa ambayo vijana hao wanapewa elimu.
Baadhi ya Watoto wanaohudumiwa na Sifa Group Foundation wakipokea zawadi ya Nguo kutoka kwa Mkurugenzi wa kituo hicho Sifa John
Watoto 17 kati ya hao huishi hapo hapo kituoni na wengine hurudi majumbani kwao jioni. Mkurugenzi wa kituo hicho Sifa John anasema, "Pamoja na kuruhusu watoto hawa warudi Majumbani kwao, roho yangu huniuma sana kwa sababu najua mahali wanakoenda kulala palivyo pabaya, ila sina jinsi sababu sijapata nyumba kubwa ya kuwatosha, lakini niko katika kutafuta jinsi ya kununua kiwanja ambacho kipo tayari na kinahitaji pesa taslimu Sh. Milioni kumi na Sita, ili tuweze kujenga shule pamoja na hosteli kwaajili ya kulala watoto hawa".
Hivi ndivyo Sifa Group Foundation inavyohakikisha kuwa Watoto wanaoishi kwenye Mazingira Magumu wanapata Elimu.
"Pia maombi yangu kwa mtu yeyote yule mwenye roho ya Huruma juu ya Watoto hawa, atowe msaada wowote alionao ili tuweze kupata mahali pa kuwaweka watoto hao 115, na waweze kusoma na kuishi maisha mazuri kama wanayoishi watu wengine" Aliongeza Sifa John.
Mkurugenzi wa Sifa Foundation, Sifa John(Wa Pili Kulia) akiwa na Baadhi ya watu walinaojitolea Misaada mbalimbali katika kituop hicho
Kwa msaada wowote, Tumia namba hizi;
Tigo Pesa: 0652 562347
M-Pesa: 0766 91 37 80.
 Account No: 010 - 00 175 951 (Benki ya Posta)
email: sifagroupfoundation13@yahoo.com

Mungu akubariki sana wewe utakayeguswa kwaajili ya jambo hili.

Monday, March 25, 2013

Usikose Kusikiliza kipindi cha "Alive Xpress Show Time".

Usikose kusikiliza kipindi cha Alive Xpress Show Time kupitia Radio ya Kikristo ya Hhc Alive Fm(91.9Mhz) kwa Wakazi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa, Kila Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia Saa 8 kamili Mchana hadi Saa 10 Kamili Jioni.

Sikiliza Hhc Alive Fm Online Kupitia;
www.hhcalivefm.org

Saturday, March 23, 2013

Historia ya Mwimbaji Sipho Makhabane.

Sipho Makhabane
Sipho Makhabane, Mwimbaji mwenye jina kubwa barani Afrika, ambapo umaarufu wake umepatikana kutokana na uwezo wake wa kutunga nyimbo zenye ujumbe wa hali ya juu wa kumsifu na kumuabudu Mungu.

Kutokana na uwezo wake huo mashabiki wengi wa muziki wa Injili wamekuwa wakimfananisha na wanamuziki mahiri kama Joyous Celebration ama Sfiso Ncwane.
  Makhabane mwenye umri wa miaka 45 ni mmoja wa magwiji wa uimbaji nchini Afrika Kusini, na ameshiriki katika shughuli mbalimbali za kiroho na kijamii. 

Kutokana na kutingwa na shughuli zake mwaka 2010 alitangaza kuachana na kazi ya kuimba, hata hivyo mwaka 2012 aliushangaza ulimwengu kwa kuachia albamu yake mpya iliyokubalika na watu wengi.

Historia ya maisha yake inaonesha kuwa ni mtu aliyekulia katika muziki huo, na kutokana na ugumu wa maisha uliokuwa ukiikabili familia yake, Makhabane alilazimika kuacha shule akiwa darasa la tano na akiamua kufanya kazi katika shamba la miwa la Kaaruls huko Mpumalanga kama ilivyokuwa kwa mwimbaji mwingine nguli Rebecca Malope.
  Makhabane alifanya hivyo walau aweze kupata fedha ya kuwasaidia wazazi wake pamoja na ndugu zake ambao walikuwa wakimtegemea yeye.

 Alipotimiza  miaka 17, alihamia kwenye kazi za ujenzi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Afrika Kusini ya Kruger.

Akiwa huko alifanya kazi ya kuwasaidia mafundi waliokuwa wakijenga nyumba kambini hapo na alipotimiza miaka 21 alikuwa tayari na ujuzi wa kutosha katika kazi ya ujenzi na akapata kazi katika eneo la Pienaar.

Mwaka 1986, Makhabane alipata ofa nzuri katika kampuni ya Telkom kama fundi, lakini katika kuhangaika kwake alijikuta akiishia kwenye muziki wa Injili.

Hata hivyo hakuwa akijua kuwa nyota ya mafanikio yake ilikuwa kwenye huduma hiyo ya uimbaji na badala yake alikuwa akifanya muziki wa kujifurahisha zaidi na si wa biashara.

Mwaka 1990, wakati huo akiwa na umri wa miaka 25, Makhabane alifunga ndoa na binti aliyekuwa na umri wa miaka 18.

Baada ya hapo ndipo alianza kazi ya kununua na kuuza kazi za muziki ndani na nje ya nchi ya Afrika Kusini.

Kutokana na kuona muziki umeanza kuingia kwa kasi kwenye akili yake, Makhabane aliamua kuachana na kazi ya ufundi mitambo ya simu na kujikita kwenye muziki.

Katika kuhakikisha anapunguza wizi wa kazi zake, mwanamuziki huyo aliamua kusambaza kazi zake mwenyewe, lakini kikwazo kwake kikawa ni namna ya kuwavutia wasambazaji waliokuwa tayari kununua kazi kutoka kwake.

Kazi yake iliyomfanya kukubalika ilianza kusikika kwenye redio ya Swazi ambayo inajulikana zaidi kwa jina la Ligwalagwala FM, ambapo kibao kilichomtambulisha ni kile cha Ngitinikela Kuwe.
Hatimaye mwaka 1996, Makhabane aliamua rasmi kuifanya kazi hiyo ya muziki wa Injili na kuacha kazi aliyokuwa akiifanya kwenye kampuni ya simu.

 Mwaka huo huo aliachia album yake iitwayo “Yek’intokozo” wimbo ambao mpaka leo unakumbukwa na mashabiki wake kwani ndio ulimtambulisha vema, ingawa tayari alishatoa album nyingine mbili miaka ya 1993 hadi 1999 za ‘Thum'umlolo” na “Jesu Uliqhawe”. 

Mwaka 1998, kupitia kampuni ya CCP Records aliachia album yake ya nne iitwayo “Uyigugu” iliyofanya vema kabla ya mwaka uliofuata kuachia nyingine iitwayo “Makadunyiswe,”. 

Mwaka 2001, alifyatua album ya Calvary ambayo iliuza kufikia kiwango cha juu na mwaka uliofuata (2002), aliachia albamu  nyingine ya ‘Akukhalwa’ ambayo ilitikisa kama album ya “Yek’intokozo,” akiuza zaidi ya nakala 70,000.

Mwaka 2003, Makhabane aliachia album ya ‘Moya wami’ ambayo pia iliuza zaidi ya nakala 70,000. 

Kutokana na umahiri wake, Makhabane ameweza kushirikishwa katika album na waimbaji wakongwe wa nchini kwake kama Jabu Hlongwane, Marehemu Vuyo Mokoena, Lundi, Hlengiwe Mhlaba na wengine wengi. 

Pia akiwa nyuma ya mafanikio ya waimbaji lukuki kama Hlengiwe Mhlaba, Ncandweni Christ Ambassadors, Shongwe na Khuphuka Saved Group. 

Nje ya uimbaji, Makhabane ni mtayarishaji wa kazi za muziki wa injili akiwa daraja la waimbaji wengine kutokana na kuwika vilivyo kupitia kazi zao zilizoandaliwa na gwiji huyo.
 
Sipho Makhabane ni mmoja kati ya Waimbaji watakaohudumu siku ya Tamasha la Pasaka la Mwaka huu litakalofanyika Uwanja wa Taifa.

Tuesday, March 19, 2013

Mtawa wa Kanisa Katoliki apigwa Risasi na Kuporwa Mil. 20.

Mtawa Shobana Synd akiwa amelazwa baada ya kujeruhiwa kwa Risasi
WATU wanaoaminika kuwa ni majambazi, wamemjeruhi kwa kumpiga risasi Mtawa wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Shobana Synd na kumpora kiasi kikubwa cha fedha.

Habari kutoka kwa wenzake zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas zinasema kuwa mtawa huyo raia wa India kutoka Shirika la Notre Dame, alishambuliwa kabla ya kuporwa fedha hizo.

Kwa mujibu habari hizo, mtawa huyo aliyekuwa akitoka benki, alijeruhiwa kwa risasi mbili wakati akisubiri kufunguliwa geti la kuingia katika Shule ya Msingi Notre Dame.

Ingawa Watawa hao hawakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha zilizoporwa, habari zinasema ni zaidi ya Sh20 milioni zilizochukuliwa benki kwa ajili ya malipo na shughuli mbalimbali za shule hiyo.

Shule ya Msingi ya Notre Dame iliyoko eneo la Njiro, jijini Arusha inamilikiwa na shirika hilo la Watawa ambao wengi wao wana asili ya Asia ambako mtawa huyo, Shobana ndiye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo. “Alipigwa risasi mbili, moja kwenye mguu wa kushoto uliovunja mfupa na nyingine ilipenya kwenye nyama za mkono wa kushoto ambako kwa bahati haijagusa mfupa...Tunamshukuru Mungu anaendelea vizuri,” alisema mmoja wa watawa kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

Akizungumza katika wodi ya Hospitali ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), alikolazwa, mtawa huyo alisema: “Ninamshukuru Mungu kwa kuninusuru katika kifo...Walinirushia risasi kadhaa wavamizi hao.

“Ninamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea, si ujanja wala uwezo wangu kuendelea kuwa hai hadi leo baada ya mashambulizi yale ya risasi. Ninawaombea msamaha na rehema wahusika ili waache uovu na kurejea katika njia ya haki.”

Kamanda Sabas mbali na kukiri kutokea kwa tukio hilo alishindwa kulizungumzia kwa undani kwa maelezo kuwa muda huo alikuwa akiendesha gari na kuahidi kulitolea ufafanuzi leo.

Kumekuwa na matukio kadhaa ya wateja wanaochukua fedha kutoka benki mjini Arusha kuvamiwa na kuporwa fedha, matukio ambayo yanazua hisia ya kuwapo mtandao wa uhalifu unaoshirikisha baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Mwaka jana, wafanyakazi wawili wa Shirika la Here’s Life Africa Mission linalomilikiwa na Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Stanley Hotay waliochukua fedha katika moja ya benki hizo walivamiwa na kuporwa zaidi ya Sh10 milioni.

Tayari uongozi wa benki zilipochukuliwa fedha hizo umeanza uchunguzi kuhusu jambo hilo kwa nia ya kubaini kwa nini taarifa za wateja wanaochukua fedha zinafika kwa majambazi ambao huwapora njiani au baada ya kufika ofisini kwao.

 - Mwananchi -

Monday, March 18, 2013

Pinda akusanya Milioni 31 Harambee ya Kanisa Dar.

Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameongoza harambee ya papo kwa papo na kufanikiwa kukusanya sh milioni 31.5 zikiwa ni ahadi na fedha taslimu kwa ajili ya ukarabati wa Kanisa Katoliki la Mashahidi wa Uganda la Magomeni, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo jana kabla ya kuendesha harambee hiyo, Waziri Mkuu aliusifu uongozi wa kanisa kwa kuamua kufanya upanuzi wa kanisa hilo, ili liweze kuhudumia waumini wengi zaidi.

“Nia yao ni nzuri sana na wameona mbali mapema. Magomeni hii ya leo si ya wakati ule, na wala haitakuwa hivi katika miaka mingine 50 ijayo. Zamani usingeweza kuona hata ghorofa moja hapa Magomeni, lakini sasa hivi maghorofa hayahesabiki,” alisema.

Aliwasisitiza waumini hao kujitoa kwa ajili ya kazi ya Bwana kwa sababu hakuna sadaka ambayo ni ndogo.

“Hakuna sadaka iliyo ndogo mbele ya Mungu, kikubwa ni dhamira tu. Kanisa ni letu na litajengwa na sisi waumini ili mradi kila mmoja wetu aseme kanisa hili nitalijenga,” alisisitiza.

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na waumini hao, Baba Paroko wa kanisa hilo, Padri Sixfrious Rwechungura, alisema wameanza kazi ya ukarabati tangu Agosti 15 mwaka 2011 na kwamba hadi sasa wamekwishakusanya sh milioni 350 kutokana na nguvu za waumini wenyewe.

Alisema wanahitaji sh milioni 300 ili kukamilisha kazi hiyo ambayo inapaswa kukamilika katika miaka miwili ijayo ili iendane na maadhimisho ya miaka 50 ya kanisa hilo.

Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu na mkewe Tunu Pinda waliahidi kuchangia sh milioni 10 na wakatoa sh milioni mbili za kianzio.

- Tanzania Daima -

Sunday, March 17, 2013

Maganga James Gwensaga: Kutoka kuwa Mpiga Debe mpaka kuwa Meneja wa vituo viwili vya Radio za Kikristo.

Maganga James Gwensaga
Jina lake kamili ni Maganga James Gwensaga Almaarufu kama President. Ni mtoto wa pekee kwa Baba yake Mzee Julius Mashenene Gwensaga na Mama yake, ingawa kwa upande wa Baba ana dada zake wanne na kwa upande wa Mama ana wadogo zake wanne pia.

Alizaliwa mkoani Morogoro kijiji cha Kichangani, wakati Mama yake akiwa ni mluguru wa Mikese, na Baba yake akiwa ni Msumbwa wa Geita.

Baada ya kuzaliwa Mkoani Morogoro, Baba yake mzazi Mzee Julius Mashenene Gwensaga ambaye ni marehemu kwa sasa, alipata uhamisho wa kikazi kutoka Morogoro kwenda Mkoani Iringa.
Maganga akiwa katika Shughuli za uchoraji enzi hizo
Toka walipofika Iringa baba yake alikaa kwa muda wa miaka mine tu na kufariki na kumuacha Maganga akiwa mikononi mwa mama yake wa kufikia ambaye alimlea toka wakati huo, baada ya mama yake mzazi kukataa kuondoka na baba yake Maganga kutoka Morogoro kwenda Iringa.

Baada ya baba yake kufariki ambaye alikuwa ni mwajiliwa wa Wizara ya ujenzi kitengo cha Ufundi katika Kiwanda cha Karatasi cha Mgororo kilichopo Mkoani Iringa, ililazimika kurudi Dar es salaam kwani uongozi wa kiwanda cha karatasi cha mgororo hakikuwa na mkataba na wao isipokuwa baba yake ambaye alishafariki.

Kutoka Iringa walienda Dar es salaam, na mwaka 1989 Maganga akaanza darasa la kwanza katika shule ya msingi Mianzini iliyopo Mburahati Mianzini.

Akiwa hapo shule ya msingi, Maganga alishiriki michezo mbalimbali na jambo analokumbuka akiwa darasa la nne alichaguliwa kujiunga na bendi ya shule jambo ambalo halikuwezekana kwa mwanafunzi yeyote wa darasa la nne kwani ilikuwa ni mpaka ufike darasa la sita ndipo ujiunge na Bendi ya Shule.

Alipomaliza darasa la Saba Maganga hakuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya serikali na hivyo kulazimika kusoma kwenye shule za kulipia(Private School), ambapo alijiunga na elimu ya sekondari kwa masomo ya jioni.
Enzi hizo Maganga akiwa anafuga rasta
Alimaliza elimu ya sekondari mwaka 1999 na kuanza kufuga nywele rasmi kama Rasta. Mwaka 2000 aliingia katika masuala ya uandishi wa habari na uchoraji wa katuni wakati huo akichorea gazeti la maisha na sanifu ya jijini Dar es salaam.

Mbali na uchoraji wa katuni katika Magazeti, lakini pia alikuwa ni mwandishi wa hadithi mbalimbali za maandishi katika gazeti la Majira.

Maganga anasema, “Namshukuru sana dada yangu Juliana Gwensaga aliyekuwa akinitia moyo katika fani hii ya uandishi wa habari.”

Mwaka 2005 Maganga alikata Rasta zake zote na kubaki na nywela za kawaida tu baada ya kufuga Rasta hizo kwa miaka 6. Ilipofika Mwaka 2007 Maganga alikutana na mwanadada Peresia Shilla na kukubaliana kuishi pamoja kama Mke na Mume, na kweli mwaka huo huo walifunga ndoa na kwa sasa wana watoto wawili wote wa kiume ambao ni Brian(mkubwa) na Brighton(mdogo).
Maganga akiwa na Mkewe Peresia Shila siku ya Harusi yao
Kwa mara ya kwanza alikutana na Askofu Magike wa Jijini Mwanza mwaka 2005 jijijni Dar es salaa, wakati huo Maganga akiwa ni msanii wa uchoraji na alikuwa na kibanda chake cha uchoraji maeneo ya mbezi mwisho jijini Dar es salaam.

Wakati akifanya shughuli hiyo ya uchoraji, pia Maganga alikuwa akihubiri Injili katika kituo cha mabasi cha mbezi baada ya kuokoka, huku akiwa ni mwajiriwa katika shule ya msingi St. Ann’s kama mwalimu wa somo la uchoraji.

Baada ya kukutana na Askofu Magike katika moja wapo ya mikutano ya Injili hapo Dar es salaam, Askofu Magike alimuomba Maganga ampigie picha za video katika mkutano wake wa Injili wa Jijini Dar na baada ya mkutano huo, alimuomba tena ampigie picha za video kwenye harambee ya kuchangia uanzishwaji wa radio ya Kikristo ya Living Water katika Jiji la Mwanza.

Baada ya harambee hiyo haukupita muda mrefu, Akofu Magike akamuita Maganga Jijini Mwanza akimwambia kuwa ile radio waliyokuwa wanaifanyia harambee imeanza kuruka hewani hivyo kama anaweza aende Mwanza.

Kweli Maganga alienda Mwanza na kuiacha familia yake Jijini Dar lakini baadaye ilikuja kujiunga naye ambapo mpaka sasa yuko nayo huko jijini Mwanza.
Watoto wa Maganga. Brighton(Kushoto), na Brian(Kulia)
Maganga anaongeza kwa kusema kuwa ” Baada ya muda flani nilichaguliwa kuwa Meneja wa kwanza hapo Living Water na baadaye nikaacha kazi na kwenda katika Radio nyingine ya Kikristo ya  Hhc Alive Fm ya Jijini Mwanza pia nikawa Meneja katika kituo hicho. Badae nikatoka na kwenda Afya Radio kama Mtangazaji wa kawaida na ndipo nikarudi tena Living water na kuwa Meneja kwa mara nyingine tena katika kituo hicho cha Radio. Hapo sikukaa sana tena ndipo Mwanzoni mwa Mwaka huu 2013 nikarudi Hhc Alive Fm na kuwa Meneja tena”

“Nimejifunza kutokukata tamaa katika maisha hasa nikikumbuka toka wakati ule nikiwa mchoraji, kwa kweli kuna wakati ilipita wiki nzima bila kupata kazi, na kuna kipindi nilifanya mpaka kazi ya kupiga debe ili walau Mkono uende kinywani. Lakini kwa sasa namshukuru Mungu hata kama sina gari, lakini la ofisi lipo natembelea ingawa naamini la kwangu linakuja.” – Aliongeza Maganga.
Maganga akiwa katika Studio za Afya Radio
Kwa sasa Maganga ni Station Manager wa radio ya kikristo ya Jijini Mwanza ya Hhc Alive Fm (91.9Mhz) “Sauti ya Tumaini” na pia anajiandaa kuchukua masomo ya Diploma ya uandishi wa habari katika chuo cha uandishi wa habari na utangazaji cha Arusha baada ya kusoma Certificate ya Uandishi wa Habari katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal kilichopo Jijini Dar es salaam.

- To God Be The Glory -