Advertise Here

Tuesday, March 26, 2013

Kupotea kwa Askofu Mkoani Njombe, Utata watawala.

Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Moses Kulola
SAKATA la kupotea kwa Askofu wa Evangelism Assemblies of God Tanzania (EAGT), Lomanus Lukosi (60), anayeishi mjini Makambako Wilaya ya Wanging’ombe mkoa wa Njombe, limezua mkanganyiko kutokana na kauli zinazotolewa na kanisa hilo na Jeshi la Polisi.
 
Mkanganyiko huo unatokana na viongozi wa Jeshi la Polisi na kanisa hilo kwa nyakati tofauti kusema askofu huyo alipatikana jana na anawasiliana na familia yake kutoka sehemu alikojificha kwa ajili ya kufanya maombi ingawa hajaonekana hadharani.
 
Katibu Mkuu wa EAGT, Askofu Brown Mwakipesile, alisema baadhi ya viongozi wa kanisa hilo akiwamo katibu wa askofu huyo wamepewa jukumu la kushughulikia suala la kupotea Askofu Lukosi.
 
Alisema hadi jana Askofu Lukosi amekuwa akiwasiliana na familia yake kutoka mahali alikojificha kwa ajili ya maombi.
 
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Moses Kulola, alipotafutwa jana kuelezea tukio hilo, simu yake ilipokelewa na mtu ambaye alijibu kuwa askofu hajajulishwa na wasaidizi wake kuhusiana na tukio hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani, alisema  askofu huyo hajapatikana ingawa anaendelea kuwasiliana na familia yake akiwa katika eneo ambalo halijulikani.
 
Naye Mchungaji Asimbagwe Mwaisabila wa kanisa hilo, akizungumza na NIPASHE kutoka Sumbawanga alisema amewasiliana na viongozi wenzake waliopo Makambako ambao walimweleza kuwa amepatikana.
 
“Mimi ni mmoja wa watu tuliokuwa tunafuatilia suala hili, nimewasiliana na wenzangu wanasema askofu amepatikana ingawa sijafahamu kama ni kweli au la maana wanasema anawasiliana na familia yake,” alisema.

- Nipashe -