Advertise Here

Tuesday, March 12, 2013

Mambo yazidi kunoga Tamasha la Pasaka.

Bw. Alex Msama
KWAYA ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration ni miongoni mwa burudani zitakazokuwepo kwenye Tamasha la Pasaka Machi 31, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama jana ilieleza kuwa makundi hayo ya jijini Dar es Salaam tayari yamethibitisha ushiriki wao pamoja na mwimbaji mahiri Upendo Kilahiro ambaye pia atashiriki.


“Niseme mambo yanaenda vizuri na leo (jana) kuna msanii tunamalizana naye kutoka Afrika Kusini, nina imani wakati wowote kuanzia Jumanne (leo) tutamtangaza kwa mashabiki wetu, nia ni kulifanya tamasha liwe zuri zaidi,” ilisema taarifa hiyo.

Wasanii wengine wa Tanzania watakaoshiriki tamasha hilo ni Rose Muhando, John Lissu na Upendo Nkone, wakati wa nje ya Tanzania ni Ephraim Sekeleti wa Zambia anayetamba na albamu zake za Acha Kulia na Mungu Mwenyewe.

Wasanii wengine wa nje watakaokuja ni Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya, ambapo pia mwaka huu kuna ingizo jipya ambalo ni kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kigali Rwanda inayotamba na albamu ya Mtegemee Yesu.

Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam Machi 31 na litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, wakati Aprili 3 ni Uwanja wa Samora mkoani Iringa na Aprili 6 itakuwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Tamasha la mwaka jana liliwashirikisha waimbaji mahiri kama Rose Muhando, Rebecca Malope, Christina Shusho, Nkone, Kilahiro, Mukubwa, Atosha Kissava, Sekeleti, kundi la Glorious Celebration, kwaya ya Kinondoni Revival na Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka DRC.

- Habari Leo -