Advertise Here

Tuesday, February 4, 2014

Safu ya James Kalekwa: Ongeza Maana/Thamani kwenye maisha yako kwa kuwa na malengo na kuyaelekea. - Part 5

James Kalekwa
Mifano hai ya watu waliotutangulia

Bwana Yesu
         Bwana wetu Yesu Kristo aliacha enzi na utukufu wake huko mbinguni na kuja duniani kufa badala yetu ili atukomboe kutoka katika laana ya dhambi.Ukitazama katika upana wa yale aliyoyafanya Yesu akiwa duniani utaona kuwa jambo jingine alikuja kuweka msingi wa maisha (kielelezo) ambayo watu wote waliomwamini wanapaswa kuyaishi kwa lugha ya kiiengereza tungeweza kusema Yesu ni role model wa maisha ya imani hii tuliyonayo!

Bwana Yesu hakuishi maisha ya kubahatisha, bali alikuwa na malengo; hebu jiulize nini kilimfanya aanze huduma akiwa na umri aliokuwa nao (miaka 30) na wala si vinginevyo? Kwanini alichagua wanafunzi kumi na mbili na si ishirini, watano au arobaini? Kwanini alikufa wakati huo na si wakati mwingine? (Wakati mwingine Wayahudi walikuja kumkamata Yesu ili wakamshitaki kisha wamuue lakini mwenyewe alisema wakati wake haujafika, akapita katikati yao na kuwaacha)

Ukisoma kwa umakini maombi ya Bwana Yesu kwaajili ya kanisa lake katika Yohana 17:1-26, utaona mambo ya uhakika juu ya vitu alivyokuwa akivifanya mstari 4, "Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye."

Bwana Yesu anaupata wapi ujasiri wa kujua kazi amemaliza wakati alijua wazi kabisa kuwa kuna watu wengi tu walikuwa hawajaokoka bado? alikuwa hajafika sehemu zingine mbali na Mashariki ya kati (Afrika alikuwa bado hajafika,Asia,Ulaya n.k), sasa kwa hali ya kawaida Yesu alikuwa bado hajamaliza kazi lakini malengo yote yanapaswa kuwa na ukomo wa muda.

Hapo baadaye katika sura hii kwa kadri ya neema ya Kristo nitakufundisha mambo yakuzingatia unapoweka malengo na sifa za malengo mazuri. Nakushauri uzisome kwa upya tena injili nne kwa lengo la kutazama maisha ya Bwana Yesu na malengo.

Mtume Paulo
Wafilipi 3:12
"Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwaajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu."
 
2Timotheo 4:6
"Kwa maana,mimi sasa namiminwa,na wakati wa kufariki kwangu umefika.Nimevipiga vita vilivyo vizuri,mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda;baada ya hayo nimewekewa taji ya haki,ambayo Bwana mhukumu wa haki,atanipa siku ile;wala si mimi tu,bali na watu wote waliopenda kufunuliwa kwake."

Huwezi kusema umefika au la iwapo hujui unakwenda wapi, vilevile huwezi kukaza mwendo kuelekea kule usikokujua.  “Kuna umuhimu gani wa kupiga mbio, iwapo hauko katika njia sahihi?"

Kuna kitu kinachomfanya Mtume Paulo awaandikie Wafilipi kwamba bado hajafika na anakaza mwendo na anamwandikia Timotheo, mwanae katika imani tuliyonayo kwamba mwendo ameumaliza kwa tafsiri nyingine ni kwamba hakazi tena mwendo; na kitu hicho ni malengo.

Je, wajua Malengo hukamilishwa kwa mikakati???
Sifa kubwa ya malengo ni kuzaa msukumo ndani mwa yule ayabebae wa kuyatekeleza. Kama malengo hayakusukumi kuanza utendaji, bado hayajawa malengo. Hii ni kwasababu malengo hayajikamilishi menyewe bali hukamilishwa kwa mikakati.

Mkakati ni mbinu, hatua madhubuti, wajibu, jukumu… ni utendaji/utembeaji kuelekea kwenye malengo husika. Kwa ujumla wake, mkakati ni mchanganuo wa wajibu/majukumu, wahusika, muda wa utekelezaji na rasilimali zinazohitajika kwaajili ya kukamilisha lengo fulani.

Luka 14:18
"Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumaliza?"

Bwana Yesu anatutambulisha kwenye wazo moja la msingi sana ambalo tunapaswa kujifunza kwalo kwa moyo na nguvu zetu zote. Anazungumza kwa lugha ya kawaida sana kwa kutumia mfano wa Ujenzi.

Hakuna mtu anayeanza shughuli ya Ujenzi bila kukaa chini na kuhesabu gharama na kuona kama anavyo vya kuumaliza! Yesu anaposema “kuhesabu gharama.” Anamaanisha si tu fedha kama ambavyo wengi hudhani moja kwa moja… Unaweza kuwa na fedha lakini huna muda, watu, nguvu kazi, nafasi n.k kwahiyo lazima tuelekeze akili zetu kumuelewa Yesu kwa kina na mapana.

Je, unavyo vya kutosha kukamilisha malengo yako? Jibu la swali huli huzaliwa kwa jinsi ambavyo utatumia muda kufanya uchambuzi na kutengeneza mkakati.

Kuna watu wengi sana nimewashuhudia na marafiki zangu kadhaa wamenaswa kwenye mkwamo ambao hata mimi hapo awali nilijikuta nimekwama na hata sasa ninajuhudi za kupigana vita kepuka mkwamo huo… kuanza jambo na kutolikamilisha!

Mkakati unakusaidia kujinasua kutoka kwenye mkwamo huo. Ninaomba uambatane nami kuchanganua mambo muhimu ndani ya mkakati.

Wajibu/Jukumu – Huu ni mchanganuo wa kazi ndogo ndogo ili kulielekea lengo husika 
Wahusika – Ndani ya mkakati unapaswa kuainisha nani atahusika kufanya nini. Ni muhimu sana mkakati ufikie hatua ya kugawa majukumu na wajibu kwa muhusika fulani kwaajili ya utendaji. Kutokana na aina ya malengo, vyaweza kuwepo vigezo vya kumbebesha mtu fulani wajibu au jukumu: mfano upatikanaji wake, kipaji, uwezo, uzoefu, ujuzi n.k

Muda/Wakati – Hii ni rasilimali muhimu amabayo kila mtu amepewa sawasawa. Kila mtu ana masaa ishirini na nne  (24) ndani ya siku moja, siku saba ndani ya wiki moja. Kinachojenga tofauti miongoni mwetu ni namna tunatumia muda wetu.

Ni LAZIMA ufanye maamuzi ni muda kiasi gani utahitajika kwaajili ya kuleta utimilifu wa jukumu fulani. Usidhani utafanya jambo moja muda wote! Kwahiyo, ni lazima kwa mfano kusema “Nitaandaa rasimu ya mafundisho/kitabu ndani ya wiki ya kwanza ya mwezi wa pili yaani tarehe 1- 7 Februari.”

Au unaweza kutumia Mchanganuo wa jedwali kama nilivyofundisha hapo awali na nitaweka mfano huo tena baada ya Maelezo haya juu ya mkakati. Usipochanganua muda hiyo ni dalili ya kuanza kutumia vibaya muda wako, utaanza kufanya chochote wakati wowote… jukumu la tisa utaanza nalo, utajikuta unatamani kufanya jukumu la nne, mara unaona jukumu la saba linaibuka likifuatiwa na jukumu la kwanza.

Hutakuwa na mtiririko maalum! Kwahiyo utajikuta katika ya mwaka hujafanya chochote cha maana zaidi ya kurukaruka tu huku na kule.

Rasilimali fedha – Masikioni mwa watu wengi sana ukisema rasilimali, huja Taswira ya fedha. Lakini kwangu binafsi hii huja kama rasilimali ya mwisho… Kwa mfano, unadhani unahitaji fedha kiasi gani kuandika kitabu???

Hauhitaji hata senti moja kuandika kitabu ila kuchapisha kitabu ndiyo unahitaji pesa… Sasa,  ni hekima sana kujua ya kwamba kabla ya kitabu kuchapishwa, kwanza huandikwa! Kwahiyo, usisingizie fedha… Kaa chini uandike. Anza kufanya yaliyo ndani ya uwezo wako kwanza.

Mkakati mzuri ni ule ambao hukusukuma kufanya Mchanganuo wa rasilimali fedha. Hii hupelekea kujua ni fedha kiasi gani zitahitajika ili kukamilisha jukumu fulani. Lakini zaidi ya hapo ni lazima kujua kiasi hicho cha fedha kitahitajika kwa wakati gani.

Vilevile, ni muhimu kuainisha vyanzo vyako vya mapato (jinsi gani fedha hiyo itapatikana) – mshahara, faida ya biashara, gawio, mkopo, changizo (harambee), ufadhili n.k hii itakusaidia sana kutembea kwa Uhakika na kutoshangazwa na mambo mengi (not to be caught by surprise).

Nguvu kazi – Huu ni uwezo ulifichika ndani ya mtu (hazina). Uwezo huu huyaleta mawazo katika uhalisia… Husababisha vitu kuwa halisi. Ni mjumuisho wa ujuzi, Uzoefu, ufahamu na nguvu. Kwa mfano, ili uwe na kitabu au mafundisho kama haya ni lazima uandishi, mitindo ya uandishi na utumuzi wa lugha viingie kazini.

Lazima kalamu na karatasi au ipad, kompyuta mpakato n.k vitumiwe na mtu ili kuzalisha matokeo. Ile Akili, fikra na mawazo ndiyo nguvu kazi. Lazima mkakati wako ukusukume kutambua na kuyachambua haya kinagaubaga.

Kumbuka, unafanya uchambuzi wote huo kwa lengo kuu la kujibu swali Je, unavyo vya kutosha kukamilisha ujenzi wa mnara?

Hongera, sasa waweza kufanya tathmini!
Huwa ninapenda chanagamoto moja… Je, ni wakati gani sahihi kusema “huu ni mwaka mpya”? Je, ni mwanzo au mwisho wa mwaka? Wengi husema mwaka ni mpya mwanzoni mwa mwaka, nadhani kwasababu ya kubadilisha kalenda. Lakini kimsingi, mwaka unakuwa mpya au la baada ya kuwa umefanya tathmini… na tathmini hufanyika mwishoni mwa mwaka.

Ninachotamani kujenga ndani ya moyo wako ni kwamba kila baada ya msimu, muda au wakati fulani ambao mwenye malengo amejiwekea, ndipo Uhitaji wa kufanya tathmini! Tathmini ni tafakari ya ndani kuhusiana na malengo ambayo umejiwekea. Lazima ujipime ni kwa kiwango gani umeyafikia malengo husika.

Kama umeyafikia lazima ujiulize mambo ambayo umejifunza, mambo yatokanayo, na mengineyo kutoka kwenye malengo hayo. Vivyo hivyo kama hukufanikiwa kuyafikia malengo yako.

Maisha ya vijana wengi wa zama zetu, hata baadhi ya watoto wa Mungu (watu waliookoka) huwa hawafanyi tathmini. Kwahiyo wanajikuta wakitembea vilevile kila siku. Huwezi kufanya tathmini mpaka umekuwa na malengo!

Kwa ujumla wake, kutathmini ni KUJIPIMA! Na hii yote hukupa kujitambua, kufahamu wazi wazi juu ya mwenendo/njia zako.

Hagai
“Zitafakarini njia zenu,"
“Lengo”  si kuwa na malengo bali kuwa na matokeo:

Kitu cha muhimu kufahamu baada ya kuweka malengo yako vizuri na kuainisha jinsi gani utayafikia yaani dhima(mpango),basi napenda kukumbusha kulenga matokeo na si kulenga dhima/mpango. Maana yangu ni kwamba usifanye tu utekelezaji eti kwa vile ndivyo ulivyouainisha,bali lenga kuleta matokeo yanayoonekana na yanayodumu.

Kwa kutumia mfano wetu wa kuihubiri injili kwa watu 1000 nchini Tanzania katika wilaya 4 kwa mwaka,usihubiri tu ili kufikia watu 1000,kisha iweje?kwahiyo lazima ulenge matokeo,baada ya hapo nini kinafuata.Siyo watu 1000 kwa lengo la kuja kuandika wakati wa tathmini,kumbe hakuna matunda yoyote.Bwana Yesu alilenga matokeo ndiyo maana matunda yake yapo mpaka hivi leo.Lenga kuleta matokeo wala si kukamilisha mipango!

Usuri wa malengo: Ufahamu wa ndani zaidi
Ndugu msomaji na mfuatiliaji wa mafundisho yetu, kama ungetamani kuona maisha yako yakiwa na matunda na maana sana. Ninakushauri utafakari sana juu ya kufanya uamuzi wa kumwamini Yesu Kristo, yaani kuokoka. Hii si dini wala dhehebu, bali ni kumwamini Yesu moyoni na kumkiri, sawasawa na neno lake, kisha kutembea sawasawa na ukiri huo. Yesu ameyapa maisha yetu thamani kubwa na yeye ndiye chanzo cha hekima, maarifa na ufahamu wote. Hivyo, ukiokoka ni mtaji mkubwa sana kuyaishi mafundisho haya.

Pia, kama utahitaji kumwalika ndugu James Kalekwa kuwa mwalimu, mnenaji, mwezeshaji kwenye kongamano, warsha au semina; ama unahitaji kujua namna gani ya kupata vitabu au mafundisho zaidi… Fanya hivyo kupitia mawasiliano yaliyoambatanishwa katika tovuti hii.

- Mwisho wa Somo -

 Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764