Advertise Here

Wednesday, November 27, 2013

Uzima wa Milele katika Damu ya Yesu Kristo - Mwl. Christopher Mwakasege (II).

Na Mwl. Christopher Mwakasege
- Inaendelea -

Yesu Kristo alisema ukiula mwili wake na kuinywa damu yake, yeye atakaa ndani yako na wewe utakaa ndani yake unapokea uzima wake wa milele unaokuvika tabia ya Uungu.

Haya ndiyo yaliyotokea kwa huyu mtoto mdogo wa umri wa miaka kumi na miwili. Huyu mtoto alipompokea Yesu Kristo na kuokoka – Kiroho aliula mwili wa Yesu na kuinywa damu yake – akapokea uzima wa milele, Yesu Kristo aliingia ndani ya mtoto, na mtoto akaingia ndani ya Yesu Kristo – yote yalifanyika kwa Uwezo wa Roho Mtakatifu.

Unadhani mtoto huyu alipata wapi ujasiri wa kufanya sala yeye mwenyewe, kitu ambacho alikuwa anaogopa kufanya kabla hajaokoka?

Jibu lake ni – Damu ya Yesu Kristo! Imeandikwa hivi; “Basi ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu…….” (Waebrania 10:19).

Niliwahi kukaribishwa katika mkoa mwingine kuhubiri katika Kanisa fulani, nakumbuka kuwa nilihubiri juu ya Bartimayo yule kipofu aliyeponywa na Yesu Kristo kule Yeriko. Nilipomaliza mahubiri nilikaribisha watu waje mbele wale wanaotaka kuokoka na kuombewa magonjwa. Watu wengi waliokoka na pia kuponywa maradhi yaliyokuwa yanawasumbua.

Baada ya wiki moja kupita, alikuja mtu mmoja nyumbani kwangu tukasalimiana na nikamkaribisha aingie ndani. Alipokwisha kukaa kwenye kiti, akaniuliza akasema; “ Mlimpa kitu gani ndugu (alitaja jina lake) siku mlipokuja kuhubiri kanisani kwetu – maana mimi sikuwepo.

Nikamuuliza, “Kwani kumetokea nini?
Yule mgeni akasema; “Huyo ndugu alikuwa hawezi kunywa chai ya maziwa wala maziwa – akinywa maziwa alikuwa anaugua. Nilishangaa siku moja alifika nyumbani, nilipomkaribisha chai ya rangi alikataa, akasema sasa anakunywa chai ya maziwa bila shida yoyote.

Nilipomuuliza ameanza lini kunywa chai ya maziwa, akasema tangu baada ya maombi ya Jumapili pale Kanisani. Lakini pia, niliona tabia yake imebadilika. Alikuwa hachani nywele- sasa anachana. Alikuwa mlevi sana – sasa haonji tena pombe. Alikuwa mchafu, hajijali – nilishangaa kumwona amevaa nguo safi. Ni kitu gani mlimpa?

Nikamjibu nikasema; “ Sisi tulichokifanya ni kuhubiri habari za Yesu Kristo na uwezo wake. Ndugu yako alifungua moyo wake siku ile, akampokea Yesu Kristo moyoni mwake ili awe Bwana na Mwokozi wake akaokoka. Pia tukamuombea tatizo la ugonjwa alilokuwa nalo na Bwana akamponya”.

Ni jambo la kumsifu Mungu sana katika Kristo, kwa sababu baada ya huyo ndugu kuokoka, na maisha yake kubadilika – sasa hivi ana kazi nzuri ya kuajiriwa na pia, ni mhubiri wa injili. Jina la Bwana libarikiwe!

Huwezi ukampokea Yesu Kristo moyoni mwako na bado ukawa na tabia uliyokuwa nayo zamani. Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako – unapokea Uzima wa milele unaokupa tabia ya Uungu.
Yesu Kristo alisema hivi; “ Amini, amini, nawaambieni, msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake hamna Uzima ndani yenu…..Aulaye mwili wangu na kuinywa DAMU YANGU hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa pekee yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote…….Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa” (Yohana 6:53,56; Yohana 15:4,5,7)

Mtume Paulo alisema; “ Hata imekuwa, mtu akiwa NDANI YA KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2 Wakorintho 5:17).

Mtume Paulo alisema hivi katika waraka wake wa pili kwa watu wote, sura ya kwanza mstari wa tatu na wa nne; “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima wa utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo atumetukirimia ahadi kubwa mno, za THAMANI, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa WASHIRIKA WA TABIA YA UUNGU, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa”.

- Mwisho -