Advertise Here

Thursday, November 14, 2013

Kardinali Domenico kuzikwa leo.

KARDINALI
Kardinali Mstaafu Domenico
MWADHAMA Kardinali mstaafu wa Kanisa Katoliki nchini Italia, Domenico Bartolucci (Pichani) aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96, anatarajiwa kuzikwa leo.

Kwa mujibu wa taarifa, Kardinali Bartolucci ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa kwaya ya kanisa dogo la Sistine jijini Vatican City, amefariki Novemba 11.

Katika salamu zake za rambirambi, Kiongozi wa Kanisa hilo, Papa Francis alisema alikuwa mtu wa upendo na padri aliyeheshimika na waamini.

Baba Mtakatifu alisema marehemu atakumbukwa kwa safari yake ndefu ya kutangaza Neno la Mungu kupitia utunzi wake wa nyimbo za dini.

“Marehemu Kardinali Bartolucci alikuwa ni mtu aliyejitoa kwa moyo wake wote kwa ajili ya kumtukuza na kumsifu Mungu,” alisema Papa Francis.

Taarifa iliyopatikana makao makuu ya kanisa hilo inasema, Mkuu wa makardinali, Angelo Sodano leo anatarajiwa kuongoza ibada ya maziko katika Kanisa Kuu la St. Peter’s Basilica.

Baada ya ibada hiyo, Baba Mtakatifu anatarajiwa kujiunga na maelfu ya waomboezaji wanaotarajiwa kufika kumsindikiza mpendwa wao katika safari ya mwisho.

Kihistoria, akiwa tayari mwanafunzi wa muziki alipata daraja la upadri mwaka 1939 sanjari na Diploma ya muziki kutoka Chuo cha Muziki Florence.

Mwaka 1942 alikwenda jijini Roma nchini Italia kuongeza ujuzi wake katika muziki na kwa muda mfupi alianza kuongoza kwaya katika Kanisa la St. John Lateran.

- Jambo Leo -