Advertise Here

Monday, November 4, 2013

Mashabiki wamlilia Rebecca Malope Tamasha la Krismasi.

Rebecca Malope
MASHABIKI wengi wa muziki wa injili nchini wameomba malkia wa muziki huo nchini Afrika Kusini, Rebecca Malope, asikose katika Tamasha la Krismasi mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, hadi sasa katika maombi wanayoyapokea, wadau wengi wamekuwa wakimpigia chapuo Malope, ambaye amewahi kuja nchini kutumbuiza kwenye Tamasha la Pasaka.

“Homa ya Tamasha la Krismasi imeanza kupanda, mashabiki wamekuwa wakiomba safari hii tusiache kumualika Malope, yapo maombi mengi, lakini hilo la Malope linaongoza, kwamba lazima awepo tamasha la Krismasi Dar es Salaam,” alisema Msama.

Malope amewahi kutamba na albamu za ‘Saturday Nite’ (aliyoitoa Januari 1, 2009), ‘Hlala Nami’ (Novemba 11, 2003), ‘Siyabonga’ (Desemba 21, 2000), ‘Free at Last’ (Novemba 18, 1997), ‘African Classics’ (Mei 5, 2009), na ‘Greatest Hits’ (Januari 10, 2006).

Tamasha la Krismasi linaloandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila mwaka, linatarajiwa kufanyika Desemba 25 jijini Dar es Salaam.

Aidha, Msama alibainisha kuwa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Krismasi, imeamua lifanyike Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Desemba 25 na siku inayofuata wataangalia mkoa gani waupe heshima.

Alisema hilo litakuwa tamasha kubwa la nyimbo za kumsifu Mungu na litakuwa na tofauti kubwa ukilinganisha na mengine yaliyowahi kuandaliwa na kampuni yake.

-  Tanzania Daima -