Advertise Here

Wednesday, November 6, 2013

Mh. Leonidas Gama kuwa Mgeni Rasmi Tamasha la Miujiza chini ya Umoja wa Makanisa Kilimanjaro.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mh. Leonidas Gama
MKUU wa Mkoa (RC) wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha la sherehe za miujiza linalotarajiwa kuanza saa tisa hadi saa 12 jioni.

Tamasha hilo la siku tano linaloanza leo, limeandaliwa na Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste (PCT) Kilimanjaro kwa kushirikiana na Shirika la Sos Mission kutoka Sweden.

Mhubiri wa kimataifa, Johannes Amritizer, atahubiri na kuendesha kongamano la masuala ya uongozi kwa watumishi mbalimbali wa taasisi binafsi na za serikali katika Uwanja wa Mashujaa ulioko mjini Moshi.

Akizungumza mjini Kilimanjaro, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Askofu Samweli Yohana, alisema maandalizi yote yamekamilika na waumini kutoka madhehebu mbalimbali watahudhuria tamasha hilo.

Alisema lengo la  tamasha hilo ni kuliombea taifa amani na mshikamano pamoja na kuwahimiza watu kutii sheria bila shuruti.

Askofu Yohana alisema tamasha hilo litakalomalizika Novemba 10, mwaka huu  litahudhuriwa na wageni 120 kutoka Marekani.

Alisema waimbaji mbalimbali ikiwamo kwaya ya waumini kutoka madhehebu maarufu kama Mass wataimba katika tamasha hilo.

Pia alitoa wito kwa wakazi wa Moshi pamoja na mikoa ya jirani kuhudhuria tamasha hilo la miujiza ambalo halina kiingilio chochote.

- Tanzania Daima -