Advertise Here

Monday, October 28, 2013

Biashara ya Madawa ya Kulevya, Viongozi wa Dini wataja Majina 61.

Viongozi wa dini wametaja majina 61 ya vinara wanaojihusisha na dawa za kulevya nchini ambao wanatarajia kuwaburuza katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), mjini The Hague, Uholanzi kujibu tuhuma zao.

Majina hayo yametajwa na Kamati ya Maadili na Haki za Jamii kwa Viongozi wa Dini na Wananchi nchini, ambapo miongoni mwao wamo wabunge wa majimbo na viti maalum, mawaziri, viongozi wa dini na wafanyabiashara.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kipendekoste, William Mwamalanga, alisema kuwa, majina hayo yalipatikana Jumanne wiki hii kupitia mkutano wa siri wa viongozi wa dini wa madhehebu ya kiislam na kikristo 134 kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na Pemba.

Mkutano huo ambao ulifanyika kwa siku mbili kuanzia Oktoba 21, mwaka huu hapa jijini Dar es Salaam uliwakilishwa na viongozi wawili wa dini kila mkoa isipokuwa Rukwa ambapo hapakuwa na mwakilishi.

Alisema ulifanyika kwa siri ili kutotoa mwanya wa kuingiliwa na mifumo isiyo rasmi ambayo ingevuruga adhima yao.

Kuhusu upatikanaji wa majina, mchungaji huyo alisema ulitokana na utafiti walioufanya ndani na nje ya nchi.

Pia alisema taarifa nyingine walizipata kupitia kwa wasiri wao kutoka ndani ya jeshi la polisi nchini na vyanzo mbalimbali vya habari kutoka nje ya nchi.

Akizungumzia mkutano huo, alisema lengo lake lilikuwa ni kutathmini biashara za dawa hizo ambazo alieleza ni tishio linaloangamiza kwa kasi kubwa vijana na kusababisha nchi kuingia kwenye aibu duniani.

Mchungaji Mwamalanga alisema katika mkutano huo walitoka na maazimio mawili likiwamo la kuwafikisha mahakamani wahusika na kufanya kampeni za siri kupita kwenye majimbo sita ya wabunge (majina tunayo) waliotajwa.

Alisema lengo la kampeni hiyo ni kuwaeleza wananchi tabia za wawakilishi wao ili mwaka 2015 waweze kuchagua viongozi bora wenye uchungu na nchi yao, wakereketwa wa amani na watakaochochea watu kujituma na kufanya kazi kwa bidii.

Alisema wakati wa uchaguzi mkuu wawakilishi wa mkutano huo, watapita tena majimboni kuwataja wahusika kwa majina.

Kuhusu viongozi wa dini ambao nao wametajwa kujihusisha na biashara hiyo, mwenyekiti huyo alisema, mkutano umewataka wafuate mfano wa Mchungaji Donald Mwakisambwe wa kanisa la Kiinjili la Kipentekoste nchini, ambaye aliacha kwa ridhaa yake.

Aidha, kamati hiyo imetoa siku 71 kuanzia Jumanne ya wiki hii kwa wahusika wote 61 kujisalimisha wenyewe kwa Rais Jakaya Kikwete.

“Wakati mchakato wa kuyapeleka majina haya ICC ukiendelea tunawataka wahusika wajisalimishe kwa Kikwete kwa kuwa orodha hii tuliyonayo (akitaja majina yao) ni miongoni mwa wale waliotajwa kwenye orodha aliyokabidhiwa Rais wakati ule, wakijisalimisha tutajua kupitia wasiri wetu,” alisema na kuongeza:

“Vinara hawa ambao Watanzania wamekuwa wakiwaita ‘vigogo wa dawa za kulevya’ hawapaswi kuitwa jina hili, hawa ni wahuni na wauaji, tusiwape majina mazuri ambayo yanawatukuza ndiyo maana biashara hii inakuwa kwa kasi,” alisema.

Kuhusu Watanzania 175 waliokamatwa nchini China ambao wanasubiri adhabu ya kunyongwa na wengine waliowahi kukamatwa nchi nyingine duniani alisema, utafiti waliofanya unaonyesha kuwa wengi wao hutumwa na wakubwa hapa nchini na kuahidiwa fedha nyingi.

- Nipashe -