Advertise Here

Thursday, October 31, 2013

Tamasha la Krismasi kufanyika Uwanja wa Taifa.

Bw. Alex Msama
TAMASHA la Krismasi 2013 limepangwa kufanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Desemba 25.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, ilieleza awali mikoa sita iliomba kuwa mwenyeji wa tamasha hilo, lakini kamati yake imeteua Dar es Salaam iwe ya kwanza.

“Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Krismasi imeamua lifanyike Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, halafu Desemba 26 tutatizama mkoa mwingine. Tunaomba mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono,” alisema Msama.

Alisema awali walipokea maombi kutoka kwa wadau mbalimbali wa muziki wa Injili nchini wakiomba lifanyike katika mikoa yao, ambayo ni Mbeya, Mwanza, Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Shinyanga.

Tamasha la Krismasi linaandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila mwaka.

Kwa mujibu wa Msama, wanataka Tamasha la Krismasi liwe bora zaidi kuliko la Pasaka kwa kualika wasanii maarufu kutoka nje na ndani ya Tanzania.

Alisema hilo ni tamasha kubwa la nyimbo za kumsifu Mungu na litakuwa na tofauti kubwa kulinganisha na mengine yaliyowahi kuandaliwa na kampuni yake.

- Tanzania Daima -