Advertise Here

Sunday, October 20, 2013

Kanisa Dar lachomwa Moto.

Kanisa la Baptist Vingunguti
KANISA la Baptist, lililoko Vingunguti jijini Dar es Salaam limechomwa moto usiku wa kuamkia Jana ambapo vitambaa na madhabahu vimeteketea kwa moto.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Marietha Minangi amesema kuwa, tukio hilo limetokea usiku wa saa nane, na hadi anazungumza na mwandishi, hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Kamanda Minangi alisema, ilikuwa mapema mno kuhusisha tukio hilo na tofauti za imani za kidini. Alisema, polisi wanaendelea na uchunguzi.
 
Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo, Hezron Mwaisemba alimwambia mwandishi wa habari hizi kanisani hapo, kuwa wakiwa wamelala usiku kama saa nane na robo hivi, binti mwenye umri wa zaidi ya miaka ishirini aliwaamsha na kuwaambia kuwa, ameambiwa kanisa linawaka moto.

“Tuliamka na kuelekea kanisani, tukakuta kweli kanisa linaungua. Yule binti alituambia aligongewa dirisha na motto wa jirani akamwambia kuwa kanisa linawaka moto. Basi, tulipofika hapa tukakuta meza moja pamoja na ile ya madhabahuni vimeteketea kabisa.

"Tulikuta kisu na kiberiti na pembeni pale kulikuwa na moto walikusanya maboksi wakayachoma, naona lengo lilikuwa kuteketeza kabisa jengo hili. Kwa bahati nzuri tulifanikiwa kuzima moto kwa kutumia mchanga,” alisema Mchungaji Mwaisemba.

Mchungaji huyo alisema kuwa, tangu kanisa hilo lijengwe mahali pale mwaka 1992 limekuwa na uhusiano mzuri na majirani, hivyo wameshangazwa na kitendo hicho.

“Sijui huyo mtu au watu waliofanya kitendo hiki walikuwa na sababu gani. Sisi hapa tuna uhusiano mzuri sana na jamii yote hapa Vingunguti,” alisema.

Mchungaji huyo alisema kuwa, thamani ya vitu vilivyoungua moto inaweza kufika shilingi 200,000/=.

Hata hivyo, Mchungaji Mwaisemba alilalamika kuwa, ukiacha tukio hilo la kuchomwa moto kanisa lake lenye waumini wapatao 150 linakabiliwa na matukio mengi ya wizi, ambapo watu wasiojulikana wamekuwa wakifika kanisani hapo usiku na kuiba vitu mbalimbali ikiwemo viti vinavyotumiwa na watoto wa shule ya awali inayomilikiwa na kanisa.