Advertise Here

Friday, December 28, 2012

Kanisa kufukua Makaburi 15 kupisha Ujenzi wa Hospitali Dar.

UONGOZI wa Kanisa la Katoliki, Parokia ya Kinyerezi  Dar es Salaam unalazimika kugharimia ufukuaji wa makaburi zaidi ya 15 ya Waislamu yaliyopo kwenye kiwanja namba 1370 kitalu B  kilichopo katika Kata ya Kinyerezi , baada ya kupewa kwa  shughuli za kijamii.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Venance Kweka alisema wanalazimika kugharimia ufukuaji wa makaburi hayo ili yaweze kuhamishwa kutoka katika kiwanja kupisha shughuli nyingine za kijamii kama Ujenzi wa hospitali katika eneo hilo. 
Alisema tayari wamejiandaa kugharimia shughuli hiyo kwa kuwa makaburi hayo ndiyo pekee yanayokwamisha  kuanza kwa mikakati ya ujenzi wa hospitali hiyo, ambayo kanisa linaamini itakuwa ni msaada mkubwa kwa kinamama na watoto  wanaoishi katika eneo hilo la Kinyerezi.  
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa Halmashauri ya Ilala Gabriel Fuime, ilifafanua kuwa itasimamia zoezi  hilo kwa  Sheria ya Serikali za Mitaa( Mamlaka na Miji) ya mwaka 1982, kanuni ya mwaka 2008 namba 4 c ambako itatumia wataalam wake. 
Fuime katika taarifa yake hiyo alisisitiza ndugu na jamaa wa waliozikwa katika eneo hilo kuwasiliana na Afisa Mtendaji wa Kata ya Kinyerezi wakiwa na barua ya utambulisho kutoka kwenye ofisi ya Serikali ya mtaa wanaoishi kabla ya Januari 20 mwaka 2013.
Alibainisha kuwa makaburi hayo yanatarajiwa kuhamishiwa kwenye makaburi ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala yaliyopo kata ya Kitunda eneo la Mwanagati  Februari 9 mwaka 2013 baada yataratibu zote kukamilika.
- Juma Mtanda -