Advertise Here

Monday, November 11, 2013

Lowassa achangisha Milioni 600 Mfuko wa Elimu KKKT.

Edward Lowassa
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ameelezea kusikitishwa kwake na kiwango duni cha elimu katika shule za sekondari za kata na hata baadhi ya vyuo vya elimu ya juu.

Akizungumza katika harambee ya kuchangia Mfuko wa Elimu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema kiwango cha elimu katika shule hizo kinamsikitisha kwani ni cha chini.

“Napenda niseme wazi kuwa kiwango cha elimu katika shule zile za kata na baadhi ya vyuo vikuu kwa kweli ni cha chini, hili mimi linanisikitisha sana kwa sababu elimu bora ni mkombozi kwa mtoto wa Kitanzania,” alisema.

Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli na muasisi wa shule hizo za kata, alipongeza kanisa kwa kusaidia juhudi za serikali katika kuimarisha na kuboresha elimu ambapo shule nyingi za kanisa zimekuwa na kiwango cha juu cha elimu.

“Sasa napenda Watanzania kupitia kwenu niwaonyeshe hawa marafiki zangu ambao wamekuwa wananisindikiza katika harambee, maana kumekuwa na maneno maneno,” alisema.

Lowassa alitoa kauli hiyo baada ya wakili maarufu, Sadock Magai kuwasilisha michango ya marafiki wa mwanasiasa huyo katika harambee hiyo.

Marafiki hao walichangia sh milioni 50. Mbali ya wakili Magai, wengine ni Lawrance Masha, Innocent Macha, Bashir Awale, Hamis Kindoroko na Lemmy Bathelemew.

Lowassa pia alisindikizwa na mbunge wa Segerea ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga aliyechangia sh milioni 3 na mbunge wa Kinondoni, Idd Azan aliyechangia sh milioni 2.

“Nampongeza na kumshukuru sana Mh. Idd Azan kwa kuja kwake kunisindikiza na kuchangia, hii ndiyo Tanzania ninayoijua, isiyo na dini, watu wa dini zote mnashirikiana,” alisema.

Katika harambee hiyo, jumla ya sh milioni 615 zikiwa ni fedha taslimu pamoja na ahadi zilipatikana na kuvuka lengo ambalo lilikuwa sh milioni 250.

- Tanzania Daima -