Advertise Here

Friday, November 1, 2013

Kanisa ladaiwa kupokonya ardhi.

WANAKIJIJI zaidi ya 75 wa Kata ya Nyalikungu katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, wameulalamikia uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga kwa kuwapokonya eneo lao la kilimo lenye ukubwa wa ekari 600.

Kwa mujibu wa nakala za mahakama, wanakijiji hao awali walifungua shauri la madai namba 6 la mwaka 2012 kudai eneo hilo na kushinda kesi hiyo lakini hadi sasa uongozi wa kanisa haujawakabidhi eneo hilo.

Hata hivyo baada ya wanakijiji kushinda kesi hiyo, kanisa nalo lilikata rufaa ambapo hukumu ilitolewa kuwa hakuna mshindi bali kinachohitajika ni maelewano baina ya pande hizo mbili.

Wanakijiji hao ambao waliwakilishwa na Charles Ndaha, ambaye katika shauri hilo alidai kuwa eneo lenye mgogoro kati yao na jimbo liko katika Kata ya Nyalikungu ambalo kanisa linadaiwa kuvamia kwa kujenga Shule ya Seminari ya Shanwa.

Kutokana na sintofahamu katika kesi hiyo, wanakijiji waliamua kukaa kikao cha pamoja kujadili hatima ya mashamba yao na kukubaliana kulifuatilia suala hilo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mjumbe aliyehudhuria mkutano huo, Richard Masele, alisema tangu eneo hilo lichukuliwe na kanisa wanakijiji hawaruhusiwi kulima wala kukatisha.

Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Maswa, Elikana Duda, alisema kwa njia ya simu kuwa wananchi wana haki ya kumiliki eneo hilo, kwamba tatizo ni kudanganywa kwa aliyekuwa Mkuu wa mkoa wakati wa kutoa vibali.

Alisema kesi ilisikilizwa na wananchi walishinda lakini suala hilo lilikuwa gumu, kwani baadaye waliliingiza kidini, licha ya wamiliki halali kujulikana kuwa ni wananchi.

- Tanzania Daima -