Advertise Here

Monday, September 24, 2012

Mwl. Christopher Mwakasege: Mambo ya Msingi ya Kutafakari kabla ya kufanya Uamuzi wa Kuoa/Kuolewa - IV.

JAMBO LA NNE
Uamuzi wa kuoa au kuolewa ni muhimu uwe mwangalifu nao,
kwa sababu utakufanya uwajibike zaidi.

Kama hujawa mtu wa kuwajibika, basi, hujawa tayari kuwajibika, kwa hiyo usiingie kwenye ndoa! Kuoa au kuolewa kunakufanya uwajibike zaidi, maana yake ni kutafuta wajibu mkubwa zaidi.

1Timotheo 5:8 anasema, “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiye amini”, maana yake ni mbaya kuliko mtu ambaye hajaokoka. Afadhali mtu yule ambaye hajaokoka. Huyo ambaye ameokoka, lakini hatunzi watu wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, maana yake amemkana Yesu; ni mbaya kuliko hata mtu ambaye hajaokoka.

Hii inaonyesha ya kuwa unaweza ukaingia kwenye ndoa ukapoteza wokovu wako, ukakosa kwenda mbinguni, si kwa sababu umefanya dhambi ya uasherati, lakini kwa sababu umeshindwa kutunza watu wa nyumbani mwako, na kwa ajili hiyo unahesabika kuwa umeikana imani.

Ukiangali kwenye Tito.2:3-5 anasema, “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu, wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema, ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao, na kuwa wenye kiasi, na kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe, ili neno la Mungu lisitukanwe”.

Unaweza ukaona kabisa ya kwamba Timotheo, anazungumza habari za vijana wa kiume waliooa na wanafamilia, au umeoa na hujapata mtoto. Unao watu nyumbani mwako, inawezekana ni msichana umeolewa, huu mstari pia unakubana. Ukienda kwenye kitabu cha Tito, Tito anaandika moja kwa moja habari za wanawake wazee, ili wawasaidie wanawake vijana, maana yake wasichana ambao ndio wameolewa tu. Anasema, “Wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao”.

Usingetegemea msichana aambiwe awapende watoto wao, hutaona mwanaume anaambiwa awapende watoto, bali anaambiwa awalee watoto. Mwanamke anaambiwa awapende watoto, ni kitu ninashangaa kila siku; maana nisingetegemea mama aliyepata uchungu wa kuzaa aambiwe ampende mtoto. Watu waliookoka wengi hasa wanapoingia kwenye ndoa, wanaingia kienyeji – kienyeji tu, hawajali ya kwamba kuna kuwajibika.

Huwa ninawaambia vijana siku zote, hata kama mlikuwa mmezoea kutokula nyumbani mwako, (maana kijana akiwa bado hajaoa, anaweza akakaa wiki au wiki mbili, jiko lake halijawahi kupika kitu); kijana akiwa bado hajaoa, hakimsumbui ana hela au hana hela, ataishi. Chakula kikiisha anaenda kutembelea ndugu na jamaa, kama hawataki kumpa chakula, atakaa hapo mpaka amekula na ndipo aondoke. Akikosa kabisa atajitia moyo kwa Bwana kwamba amefunga, na kumbe ameshinda njaa!

Wakati mwingine mambo yakimzidia, na hana sabuni ya kufulia nguo anasema hajali, kwa hiyo anaendelea, hana shida, anabadilisha nguo sio kwa sababu amefua, lakini anabadilisha ili angalao jasho liweze kupungua hasa mnuko wake, kwa hiyo anaitundika mahali ipigwe upepo usiku; na baada ya siku mbili anavaa hiyo hiyo tena!

Huwa ninawaambia vijana siku zote kama hauko tayari kuwajibika, usioe. Kwa sababu kama umeoa, haijalishi ya kwamba unafunga au hufungi, chakula lazima kiwemo nyumbani mwenu. h haleluya! Na ukishaoa tu, maana yake umeitangazia dunia nzima ya kuwa umeamua kuwajibika, na unaweza ukatunza mke. Mambo ya kwenda kuomba -omba msaada tena inakuwa ni kitu ambacho si wakati wake sasa. Maana unaposema, mimi nimeamua kuoa, maana yake umekubali kuwajibika –na hii ni pamoja na kumlisha na kumtunza mke wako.

Ndio maana ukienda kwenye makabila mengine wanakuambia, ‘kijana unataka kuoa umejenga nyumba?’ Nimeona makabila mengine wanauliza, ‘kijana wewe utaoaje wakati hata nyumba huna?’ Ndio maana vijana wanazuiwa kuoa wakiwa shule, kwa nini, kwa sababu katika ndoa watahitaji kuwajibika. Sio kwa sababu wakiwa shule hawawezi kuoa, ila ni kwa sababu wanajua suala la kuoa sio kitu cha mchezo, linahitaji mahali ambapo unahitaji kuwajibika. Ndani yako lazima uwe umekubali kuubeba wajibu uliomo katika ndoa!

Na kama ni msichana unataka kuolewa ukubali kuwajibika basi la sivyo usikubali kuolewa kama hujawa tayari kuwajibika. Tito anawaambia wazi kabisa, ya kuwa wafanye kazi nyumbani mwao wenyewe. Lakini sasa unataka hata kama umeolewa, uishi maisha kama msichana, na hiyo ni hatari sana. Ukiingia kule ndani ya ndoa kuna mabadiliko. Wakati ule ulikuwa unaosha vyombo vichache maana ni vya kwako peke yako, sasa na mume wako yuko, na marafiki zake wamekuja –vyombo vya kuosha vitaongezeka, na kuwajibika kwako kunaongezeka.

Ilikuwa inakusumbua kupika, unapika mara moja kutwa, na siku hizi wataalamu wametuletea kitu kinaitwa ‘hot pot’, kwa hiyo hii mambo ya kupasha pasha moto chakula siku hizi wakati mwingine hayahitajiki. Mtu ameweka chakula chake anakifunika vizuri, anakuja jioni anakuta bado cha moto. Lakini ninakuambia labda umeingia umeolewa na mtu ambaye ni mtumishi, ana wageni nyumbani kwake kama kituo cha polisi, kila baada ya dakika mbili amekuja na wageni wengine.

Labda mume wako ni mkarimu sana, kila mgeni akija anakuambia, “fulani chai vipi?” Huko jikoni ‘unauma vidole’ maana umeshaingia jikoni kuanzia asubuhi; labda saa hiyo ni saa tano, na umeshaingia jikoni kupika mara nyingi, maana wageni wanapishana kila wakati. Kila saa ‘chai, chai’, unatamani uondoke ili usiendelee kupika, lakini umebanwa – ndio kuolewa kwenyewe huko. Ukiamua kuolewa kuwajibika kwako jikoni kutoangezeka zaidi.

Huwezi ukaamua tu saa yoyote ukasema, mimi nataka kwenda kutengeneza nywele, huo muda wa uhuru wa jinsi hiyo umekwisha, ukitaka kwenda kutengeneza nywele lazima uage, huwezi ukaondoka tu saa yoyote unayotaka, kila kitu kinabadilika. Kuna masuala ambayo utahitaji kuwajibika nayo pale nyumbani, huwezi kukwepa! Na kuna mambo mengine hakuna mtu mwingine ambaye atafanya kwa niaba yako; kama usipotaka kuyafanya wewe.

Ndio maana watu wanafika mahali, msichana anaolewa lakini wiki ya kwanza tu anataka msichana wa kazi wakati, hana hata mtoto mdogo. Unataka msichana wa kazi wa nini, huo ni uvuvi tu. Lazima uwe mwangalifu, wewe umeolewa tu, unataka msichana wa kazi, wa nini? Unaweza ukajitetea na kusema ni kukusaidia kazi – kazi zipi? Unaweza ukajitetea na kusema, aa! Unajua ninachelewa sana kutoka kazini, angalao nikute mtu wa kupika. Mimi ninakumbia unaanza vibaya. Kama ndiyo kwanza umeolewa tu, na unataka wakumpikia chakula mume wako awe ni msichana wa kazi, basi unaanza vibaya.

Wakati huo ndio saa ya kumtayarishia mume wako mapishi ambayo hajawahi kuona kwenye nyumba ya baba na mama yake! Akikaa mwenyewe huku anakula awe anasema, ‘ahsante Yesu kwa kunipa msichana wa namna hii!’ Kwa sababu hajawahi kuona chakula kizuri cha namna hiyo ulichompikia – hata hoteli hajawahi kukipata!

Lakini unaanza tu maisha ya ndoa na kumbandikia mume wako watu wa kumhudumia, mimi ninakuambia unaanza vibaya, huko unakoelekea na ndoa yako sio kuzuri. Uamuzi wa kuoa au kuolewa usiucheezee, kaa chini, fikiri kwanza na kuomba kabla hujaamua.

Somo hili bado linaendelea. Usikose sehemu ya Tano ya somo hili hapo kesho.