Advertise Here

Friday, September 7, 2012

Mahakama Mkoani Arusha yaitupilia mbali kesi ya Kanisa Anglikana.

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha, imetupilia mbali kesi ya kupinga kusimikwa kwa Askofu Stanley Hotay kuwa askofu wa Kanisa la Anglikani Dayosisi ya Mlima Kilimanjaro, iliyofunguliwa mahakamani hapo na waumini watatu wa kanisa hilo.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Fatma Massengi, aliyesikiliza shauri hilo la madai namba 118/2011 na jinai namba 48/2011 yaliyofunguliwa na waumini wa kanisa hilo, Parokia ya Mtakatifu James, Lothi Oilevo, Godfrey Mhone na Frank Jacob, dhidi ya bodi ya wadhamini wa kanisa hilo pamoja na askofu huyo.

Hata hivyo baadaye mahakama ilimuengua kwenye shauri hilo Mhone baada ya kushindwa kukidhi vigezo kisheria.

Katika hukumu yake jana, Massengi alisema kuwa alifikia uamuzi wa kuliondoa shauri hilo mahakamani hapo bila gharama wala kutoa maagizo yoyote baada ya kuridhika na pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa wadaiwa, Albert Msando na Joseph Thadayo.

Mawakili hao walidai kuwa mahakama hiyo haina nguvu kisheria kusikiliza shauri hilo kwani katiba ya kanisa hilo iko wazi kuwa masuala yote ya uchaguzi ndani ya taasisi hiyo yatashughulikiwa na ngazi mbalimbali ndani ya kanisa, ambapo mamlaka ya mwisho ya rufaa ni nyumba ya maaskofu wa kanisa hilo inayojumuisha maaskofu kutoka dayosisi zote.

Jaji Massengi alisema kuwa hata mambo yanayobishaniwa kisheria hayapo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali yako kwenye Katiba ya Kanisa la Anglikani, ambayo mahakama hiyo haina nguvu kisheria kuyaingilia.

Aliongeza kuwa kutokana na msingi huo mahakama haiwezi kuingilia suala hilo huku akikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa wadai hao walifanya makosa ya kisheria kwenye hati ya kufungua madai mahakamani hapo ambapo badala ya kuandika namba ya usajili wa bodi ya udhamini ya kanisa waliweka namba ya cheti cha usajili ya kanisa SO 4757.

Katika kesi ya msingi wadai hao kwa pamoja waliomba mahakama itoe tamko kuwa Hotay waliyedai alidanganya katika cheti chake cha kuzaliwa cha Februari 12, 2010 na kwamba cheti hicho kilitolewa kwa njia ya udanganyifu, hivyo mchakato wote wa uchaguzi ukiwamo wa Aprili 15 mwaka huu uliomweka madarakani ni batili.

Wadai hao kupitia wakili wao, Meinrad D’Souza, walidai kuwa Katiba ya Kanisa la Anglikani, inaeleza kuwa mchungaji wa kanisa hilo anayeweza kufikiriwa kutwaa cheo hicho cha juu, anatakiwa awe na miaka kati ya 40 na 60 wakati inadaiwa mchungaji huyo mwaka jana alikuwa ana miaka 38 .

Katika kesi yao ya pili, waliiiomba mahakama kuzuia sherehe za kusimikwa kwake zilizopangwa kufanyika Juni 12 mwaka huu jijini Arusha, hadi kesi zote zitakaposikilizwa na kutolewa maamuzi na mahakama hiyo.

Aidha, shauri hilo lilisimama kwa muda baada ya Juni 10 mwaka huu, Jaji Sambo aliyekuwa akisikiliza shauri hilo kutoa amri ya zuio la muda kuzuia Hotay asisimikwe kushika wadhifa huo katika sherehe zilizopangwa kufanyika siku mbili baadaye ili kumwezesha kutoa uamuzi wa mapingamizi hayo Juni 13, mwaka huu.

Licha ya zuio hilo, sherehe za kusimikwa Hotay ziliendelea na akapewa daraja la uaskofu bila kupangiwa kituo rasmi cha kazi, hatua iliyoibua mvutano mkali wa kisheria kati ya kanisa hilo na Idara ya Mahakama baada ya Jaji Sambo kutoa amri ya kukamatwa Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini , Dk. Valentino Mokiwa na askofu Hotay ambao walikata rufaa Mahakama ya Rufani.

Tanzania Daima