Advertise Here

Monday, January 21, 2013

Waumini KKKT Usharika wa Mjini Kati Arusha, wagoma kusali Kanisani.

Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Arusha wakiandamana kwenda Usharika wa Mjini Kati ambako ni ofisini kwa Mchungaji wa Usharika huo, Titus Laroya kupinga kile walichodai ni ufisadi katika ujenzi wa Kanisa hilo jana. (Picha na John Mhala).
Washarika wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati wakiwa kwenye Maandamano kuelekea Usharika wa Mjini Kati kwenye Ofisi ya Mchungaji wa Usharika huo.
KATIKA hali isiyo ya kawaida waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Usharika wa Mjini Kati Arusha, wamesusia Ibada ya Jana Jumapili kushinikiza kupata taarifa ya fedha ya ujenzi wa Kanisa la Usharika huo.
 
Tofauti na ilivyo kila Jumapili, jana waumini hao baada ya kujikusanya katika viwanja vya Kanisa linalojengwa  na kufikia zaidi ya 500, waliamua kuandamana hadi ofisini kwa Mchungaji wa Usharika huo, Titus Laroya kumtaka aeleze fedha za ujenzi wa kanisa hilo zilikokwenda.
 
Wakizungumza na mwandishi, waumini hao wamedai wamekuwa wakichangia ujenzi huo kwa miaka miwili sasa lakini hawaoni hatua zinazolingana na michango yao na kwa sasa ujenzi umesimama.
 
Wakiwa na mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali, baadhi ya waumini hao walibeba vifaa vya ujenzi vilivyodaiwa kununuliwa na Mchungaji  Laroya na kuvipeleka katika ofisi hiyo kwa madai kuwa ni feki na, havifai kwa matumizi ya ujenzi wa kanisa hilo.
 
Awali waumini hao walifika katika viwanja vya kanisa hilo saa 12.30   kuhudhuria ibada ya kwanza, lakini hali ilikuwa ya wasiwasi na baada ya muda walihamasishana kugoma kuingia kanisani.
 

Kutokana na hali hiyo ya wasiwasi huku wakionekana wazi kuwa na jazba, Mchungaji huyo aliamua ‘kuingia mitini’ kimya kimya huku akiacha gari lake katika maegesho ya kanisa hilo.
 
Baada ya kugoma kuingia kanisani na bila kumuona Mchungaji, ilipofika saa 1.45 waumini hao walifikia uamuzi wa kuandamana kwenda Ofisi ya Mchungaji Laroya iliyopo mbali kidogo na kanisa hilo, katikati ya Jiji la Arusha, Barabara ya  Goliondoi meta  chache karibu na Ofisi Kuu ya Dayosisi.
 
Polisi walifika katika kanisa hilo wakati waumini hao wakijiandaa kuandamana na kuangalia hali halisi na kuwaacha waumini hao kuendelea na maandamano huku wakiimba nyimbo mbalimbali za mapambio za  kupiga vita ulaji na ufisadi unaoshika kasi katika Kanisa hilo kwa sasa bila viongozi wa juu kuchukua hatua.
 
Akizungumza na mwandishi mara baada ya kumalizika kwa maandamano hayo, mmoja wa waumini hao,  Elibariki Mbise alisema tangu waanze kutoa michango ya ujenzi wa kanisa hilo kwa zaidi ya miaka miwili na nusu, hakuna kinachoendelea na kila wakiuliza wanatishiwa kutengwa katika usharika huo.
 
Mbise alidai mbali ya vitisho hivyo, kibaya zaidi ni hatua ya Kamati ya Ujenzi wa Kanisa hilo kukosa taarifa juu ya kiasi kilichopatikana kwa muda wote huo kwa kuwa majukumu hayo yanafanywa na Mchungaji Laroya mwenyewe.
 
Alidai Kamati ya Ujenzi na baadhi ya wazee wa usharika huo wakihoji mara kadhaa juu ya michango na sadaka za ujenzi wa kanisa hilo, wamekuwa wakitishiwa kutengwa hatua inayoonesha kuwa Kanisa linaendesha shughuli zake kibabe na si kwa uwazi kwa manufaa ya wote.
 
Msharika mwingine, Richard Mollel alidai kinachowaudhi   ni Mchungaji Laroya kuacha kuendelea na ujenzi wa kanisa hilo kwa muda wa miaka miwili na zaidi na kununua vifaa ‘feki’ kwa gharama kubwa huku baadhi  ya vifaa hivyo vikiozea ndani ya stoo ya kanisa hilo.
 
Mollel aliendelea kudai kuwa Mchungaji huyo kambadilisha mhandisi wa awali aliyekuwa akijenga kanisa hilo na kumtafuta wa kwake bila kuitaarifu Kamati ya Ujenzi ambayo haijui sababu za kutimuliwa kwa mhandisi wa awali.
 
‘’Hapa Kamati ya Ujenzi ni hewa kwa sababu haijui chochote na kila kitu anafanya Mchungaji, sasa ndio maana tumeamua kumpelekea vifaa vyake vyote feki ofisini kwake na tunataka maelezo ya kiasi cha fedha kilichopatikana kwa muda wa miaka hiyo miwili vinginevyo hakitaeleweka, ’’alidai Mollel.
 
Mchungaji Laroya pia anatuhumiwa na Kwaya ya Vijana ya Uinjilisti ya Usharika huo kwa kula fedha za harambee ya ununuzi wa basi la kwaya zaidi ya Sh milioni 80 zilizochangwa mara tatu kwa nyakati tofauti; mara mbili harambee ikiongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Makuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri.
 
Baada ya kubanwa na wana kwaya hao, Mchungaji Laroya aliwapooza wanakwaya hao kwa kuwanunulia basi chakavu lenye thamani ya Sh milioni 60 lakini basi hilo lilisusiwa na kwaya hiyo na hadi leo limeegeshwa katika uwanja wa Kanisa hilo la Mjini Kati.
 
Juhudi za kumpata Mchungaji Laroya kuzungumzia
shutuma hizo zilizoelekezwa kwake, zilishindikana baada ya simu yake ya mkononi kufungwa kutwa nzima ya jana huku akiwa haonekani ofisini kwake kila alipotafutwa.

- Habari Leo -

Saturday, January 12, 2013

Kuna Kuinuka tena katika Jina la Yesu.

 
"Kwa kuwa japo mtu mwenye haki huanguka mara saba, huinuka tena, lakini waovu huangushwa chini kwa maafa" -Mithali 24:16.

Mambo ambayo yamekuwa na tabia ya kuisonononesha mioyo ya wanadamu na pale tunapoona kuwa tumeshindwa kufanya jambo fulani tulilokusudia, na pale ambapo tumejikuta tukitenda mambo yasiyofaa katika sehemu mbalimbali za maisha yetu. Kwa wana wa Mungu, pale tunapomkosea Mungu kwa namna mbalimbali, mara nyingine tunakata tamaa na kuona kuwa hatuwezi kabisa kuishi katika uhusiano mzuri na Mungu wetu.

Kwa ujumla, kuna mambo kama haya ambayo yanatukatisha tamaa ya kuendelea mbele katika mambo ya mafanikio yetu. Ni wazi kuwa, tukiendelea kuyatafakari mambo hayo tuliyoshindwa, na tukaendelea kukata tamaa, basi hiyo itachangia sana sisi kukosa morale ya kusonga mbele na kufanikiwa katika maisha yetu.

Watu wengi wamekuwa wakifanya uamuzi wa kumkabidhi Mungu maisha yao yote na kuamua kuishi maisha yao kwa uongozi wa Neno la Mungu na kumcha Mungu kwa mioyo yao yote, lakini mara majaribu yajapo baadhi hushindwa kuhimili majaribu hayo na hivyo kujikuta wanaanguka katika dhambi.

Katika hali kama hiyo, watu wengi hukata tamaa na kuona kuwa hawawezi kabisa kuishi kwa kumcha Mungu, na hata wengine kusema kuwa haiwezekani kuokoka ukiwa hapa duniani. Kwa ujumla wake, kuvunjika moyo limekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa wana wa Mungu ulimwenguni pote.

Lakini je, Neno linasemaje kuhusu watu wanaojaribu kufanya jambo jema na kuanguka? Je, inawaruhusu kukata tamaa na kuamua kurudi nyuma? Hebu tutafakari maandiko yafuatayo: "Kwa kuwa japo mtu mwenye haki huanguka mara saba, huinuka tena,lakini waovu huangushwa chini kwa maafa" -Mithali 24:16.

Katika mstari huu, Neno latuambia kuwa, mtu mwenye haki anaweza akaanguka (akashindwa kutimiza jambo fulani katika maisha yake) hata mara saba, lakini katika mara zote hizo huinuka tena. Neno halisemi kuwa baada ya kuanguka mtu huyo ataendelea kubaki chini, bali, huinuka tena.

Mtu huyo aliyenenwa katika mstari huo hapo juu, yeye anapoanguka hiyo huwa ni nafasi ya kujifunza zaidi kutokana na kuanguka kwake ili asianguke tena,na kisha huinuka tena. Hujifunza kutokana na makosa.

Je, umejaribu kufanya bidii kuimarisha uhusiano wako na Mungu (maombi, kusoma Neno, kuhudhuria Ibadani) lakini mara nyingi umekuwa ukianguka dhambini na sasa umekata tamaa? Je, kuna mambo ambayo umeshindwa kuyatimiza katika mipango ya maisha yako na sasa umekata tamaa?

Je, kwa makosa uliyoyatenda huko nyuma moyo wako umehuzunika na umekataa tamaa hata ya kunia kutenda makubwa katika mwaka huu wa 2012? Kama ni ndiyo, basi hili ni Neno la Bwana kwa ajili yako siku ya leo: "Inuka tena". Kumbuka huo mstari tuliosoma "Kwa kuwa mtu mwenye haki huanguka mara saba,huinuka tena."

Jipe moyo katika Yesu Kristo, jitie nguvu katika Bwana upate morali ya kusonga mbele tena na kutenda makuu katika mwaka huu. Jifunze kutokana na makosa yako na kisha inuka uendelee mbele. Mwombe Mungu na umwamini tena mwaka huu naye atakusaidia na kukufanikisha, mradi tuu usizimie moyo.

Wewe ni Askari wa Kristo na mwana wa Mungu aliye hai, usivunjike moyo kamwe, Amen?

TUOMBE ...
"Baba katika Jina la Yesu Kristo, nakushukuru sana kwa ajili ya Neno lako hili uliloniletea kwa njia hii. Baba, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutenda mambo makuu katika maisha yangu. Asante kwa yale yote ambayo nimeweza kuyatenda kwa mafanikio, na ninaomba unipe macho ya rohoni, nipate kujifunza kutokana na makosa yote niliyoyafanya katika maisha yangu na niweze kuwa bora zaidi. Ninaomba unipe nguvu kwa Jina la Yesu Kristo, ili nisizimie moyo kamwe kwa sababu ya madhaifu yangu, bali nipate kuwa hodari katika Bwana na nitende makuu kwa uwezo wako Mungu Baba. Nimeomba haya na kuamini, katika Jina la Yesu Kristo, Amen."

- Frank Lema -

Monday, January 7, 2013

Hosanna Christian Centre yafanya Tamasha Kubwa la Kumshukuru Mungu kwa Kuiona 2013.

Revival Mission Band wakihudumu
SIKU ya Jana katika Kanisa la Hosanna Christian Centre lililoko maeneo ya Kilimahewa Jijini Mwanza chini Mtumishi wa Mungu, Bishop irene Nzwalla, kulifanyika Tamasha kubwa la Kusifu na Kuabudu likiwa na Lengo la Kumshukuru Mungu kwa Kuiona 2013, kwani ni Neema ya Kipekee sana.
MD Adolph Robert Nzwalla chini ya Uwepo wa Mungu
Twakuabudu Bwana.................
Uweponi Mwake
Vikundi mbalimbali pamoja na Band mbalimbali za Muziki wa Injili zilishiriki huku Hosanna Praise Team chini ya Music Director(MD) na Mtangazaji wa radio ya kikristo ya Alive Fm, Adolph Robert Nzwalla wakiongoza Sifa na Kuabudu.
Sehemu ya Hosanna Praise Team
Uliniweka Tumboni Mwa Mama yangu ili Nitumike kama Chombo........
Dada huyu aliimba Siku ya Jumapili akiwa ni Mjamzito wa Miezi 9, na Siku ya leo amejifungua salama mtoto wa Kiume. Ni Jambo la Kumshukuru sana Mungu!
Baadhi ya Band za Muziki wa Injili zilizoshiriki ni kama Revival Mission Band pamoja na Exellence Band zote zikiwa ni za Jijini Mwanza. Pamoja na Pastor David Yared.
Pastor David Yared akihudumu
Katikati, ni Mzee wa Juu ya Mataifa Almaarufu Joel Kaema(Mtangazaji Alive Fm)
Papaa Noel Mlabwa Kutoka katika Kundi la "Brothers" la Jijini Mwanza
 Mbali ya Tamasha hilo pia Jana ilikuwa ni siku Maalum ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi katika Kanisa hilo. Jiwe hilo liliwekwa na Mchungaji kiongozi wa kanisa hilo Bishop Irene Nzwalla.
Bishop Irene Nzwalla
Moja ya Vichwa vyenye Vocal Kali sana Jijini Mwanza
Sephone Sospeter kama kawaida yake