Advertise Here

Tuesday, December 10, 2013

Cheka na Mc Pilipili - Episode 3.

Leo ni Siku ya Jumanne na Kama kawaida siku ya Jumanne huwa tuna kitu kinaitwa "Cheka na Mc Pilipili".

Hivi unatambua kuwa Mc Pilipili ni Muhubiri na ni Mchungaji??? Sasa leo katika "Cheka na Mc Pilipili" tunakuletea moja ya Mafundisho ya Neno la Mungu ya Mc Pilipili, alipofundisha kupitia Kipindi cha Gospel Hits cha Sibuka Tv.

Haya Kazi kwako sasa kutazama

Monday, December 9, 2013

Mchungaji Gwajima kuhubiri Injili kwa Helikopta.

WAKATI viongozi wa madhehebu ya dini ya Kikristo nchini, wakionekana kushindana kwa utajiri, hali inayowafanya waishi `kifalme’ na kufungua miradi, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema hana mpango wa kufungua biashara, zaidi ya kujikita na mahubiri ya Injili.

Aidha, amesema Mungu anaendelea kumbariki katika kazi yake, ndiyo maana mambo yake yanamnyookea, akitolea mfano kuwa baada ya kumiliki nyumba, magari na fedha za kutosha, sasa amembariki na kumpa helikopta atakayoitumia kufikia waumini wake wa ndani na nje ya nchi.

Usafiri huo wa angani, utaongeza idadi ya vyombo vya usafiri vya Mchungaji huyo, ambaye anatajwa kuongoza kwa utajiri miongoni mwa viongozi wa madhehebu ya Kikristo nchini, kwani anamiliki magari kadhaa, likiwamo lakifahari aina ya Hummer lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni kwa simu, Gwajima ambaye alikuwa anaendesha mikutano ya kueneza Neno la Mungu katika mikoa mbalimbali ikiwamo Kilimanjaro na Tanga, alisema helikopta imeshanunuliwa na matarajio yake ni kwamba, baada ya kukamilika taratibu zote za kisheria nchini, itawasili.

“Sipendi kusema mambo yangu sana, lakini kwa kuwa umeuliza naweza kugusia kidogo, ni kweli nina mpango wa kuanza kuhubiri Injili kwa helikopta, na kama ilivyo kwa gari, nayo hii nimepewa na watu wa Mungu walioguswa na huduma yangu Japan."

“Itafika nchini wakati wowote mambo ya kisheria yakikamilika, huu si wakati wa kuizungumzia sana maana bado haijafika,” alisema Gwajima ambaye gari lake aina ya Hummer liliwahi kuzua gumzo, wengine wakimhusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ingawa anapuuza madai hayo.

Mchungaji Gwajima, alieleza wazi kuwa utajiri wake unatokana na baraka anazopewa na anaowahudumia ndani na nje ya nchi na pia kazi yake ya kufundisha anayoifanya ughaibuni.

Aidha, kutokana na utajiri anaosema unatokana na baraka za Mungu, Mchungaji Gwajima anamiliki nyumba ya ghorofa nne eneo la Mbezi Beach katika Manispaa ya Kinondoni, ingawa haijakamilika.

Pia, amewanunulia wachungaji wake 40 magari ya kutembelea kwa bei tofauti, yakiwamo ya chini ya Sh milioni 10 na mengine ya zaidi ya Sh milioni 20.

“Lakini nina wachungaji wa ngazi mbalimbali, hawa ni wale wa juu, wengine wachungaji wadogo wapo zaidi ya 670, hawa ni watenda kazi muhimu na wanatofautiana kwa ngazi zao, ndiyo maana kazi ya Mungu inasonga mbele hata nisipokuwapo,” alisema.

Mbali na magari ya wachungaji, pia amenunua mabasi 20 ya kubeba waumini kutoka na kwenda kanisani, yakianzia maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Alithibitisha kuwa, kila moja limegharimu kati ya Sh milioni 80 na 100. Mbali ya Mchungaji Gwajima, viongozi wengine wa makanisa wanaotajwa kuwa na utajiri mkubwa wa mali na fedha ni Nabii na Mtume Josephat Mwingira wa Kanisa la Efatha anayemiliki benki, mashamba makubwa na mali nyingine, Mchungaji Getrude Lwakatare wa Mikocheni B Assemblies of God anayemiliki mtandao wa shule za St. Mary’s nchini.

Wengine ni Askofu Zachary Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Anthony Lusekelo `Mzee wa Upako’ wa Kanisa la Maombezi `GRC’ na Mtume Onesmo Ndegi wa Kanisa la Living Water Center ‘Makuti Kawe’.

- Habari Leo -

Sunday, December 8, 2013

Viongozi wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani wamsifu Mzee Nelson Mandela.

Marehemu Nelson Mandela
Viongozi wakuu wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Duniani katika salam zao za rambi rambi kwa wananchi wa Afrika ya Kusini, wamemsifu Mzee Nelson Mandela, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95, kuwa ni kati ya watu walioacha mfano wa kuigwa kwa Jumuiya ya Kimataifa katika Karne ya ishirini na moja.

Ni kiongozi aliyesimamia kweli za maisha, akatetea haki na amani na kuhakikisha kwamba, demokrasi inapatikana na ubaguzi wa rangi unatokomezwa nchini Afrika ya Kusini. Ni kiongozi na mpigania haki ambaye alijikita zaidi katika majadiliano kama njia ya kufikia amani ya kweli badala ya kutumia silaha. Kwa miaka 27 akatupwa kizuizini, hadi alipoachiliwa huru kunako mwaka 1990, mchango mkubwa wa Kampeni ya Kimataifa. Mwaka 1993 akapewa tuzo ya amani duniani na kugawana na mpinzani wake Bwana Frederick W. de Klerk, watu ambao wameandika historia mpya ya Afrika ya Kusini.

Tata Madiba alipochaguliwa kuwaongoza wananchi wa Afrika ya Kusini, akataka kuona: utawala wa sheria na kwamba, ubaguzi wa rangi ulikuwa hauna tena nafasi kwa wananchi wa Afrika ya Kusini, bali wote kujitambua kwamba, ni wananchi wanaotegemeana na kusaidiana katika medani mbali mbali za maisha, kwa kuheshimu utu wa kila mtu na wala si rangi ya ngozi! Kila mtu akapata nafasi ya kushiriki maisha katika Afrika ya Kusini huru na mpya zaidi.

Kama Rais wa kwanza mzalendo, akagundua umuhimu wa upatanisho kama njia ya kuponya makovu ya chuki na ubaguzi wa rangi na kwamba, upatanisho ndiyo iliyokuwa njia pekee ya kudumisha misingi ya haki na amani ya kudumu. Watu wakapewa fursa ya kutubu na kuomba msamaha; ukweli ukafahamika na watu wakawa huru! Ndiyo maana watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaomboleza kwa kifo cha Mzee Madiba, mtu wa watu, liyeteseka kifungoni kwa miaka 27 na amevumilia pia mateso ya ugonjwa wake, hadi mauti yalipomfika hapo tarehe 5 Desemba 2013.

Hakuona kwamba uongozi ni kitu cha kung'ang'ania sana, akaamua kwa utashi wake kamili kung'atuka kutoka madarakani, viongozi wengine wakaendeleza pale aklipoachia Mzee Nelson Mandela. Apumzike kwa amani.

- Radio Vatican -

Mkutano wa Ufufuo na Uzima sasa kuhamia Morogoro.

Mch. Josephat Gwajima
Baada ya mikutano iliyovunja rekodi kwa idadi ya watu yaani Arusha, Moshi na Tanga; sasa kanisa la Ufufuo na Uzima linahamishia mikutano yake mkoani Morogoro ambapo Mchungaji Gwajima ambaye pia ni mchungaji kiongozi wa kanisa hilo anatarajiwa kuhubiri kwa siku nane mfululizo.

Pamoja Mchungaji Gwajima atafuatana na timi ya watendakazi zaidi ya mia tatu na waimbaji maarufu wa injili kama Flora Mbasha, John Lisu, Jackson Benty na Mwanamapinduzi Band.

Mkutano huo wa kwanza kufanyika Morogoro kwa kanisa la Ufufuo na Uzima unatarajiwa kushuhudia misukule wakirudi, wagonjwa kupona, viwete kutembea na mambo mengine mengi ya ajabu.

Usikose kuhudhuria na wewe ili kupokea muujiza wako.

- Ufufuo na Uzima -

Wednesday, December 4, 2013

Papa Francis adaiwa kutoroka Vatican usiku.

Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amedaiwa kutoroka usiku Makao Vatican ili apate fursa ya kwenda kutoa misaada kwa walemavu na watu wasiojiweza.

Tetesi za Papa Francis kuwatembelea maskini hao usiku kwa kujificha zimekuja baada ya mahojiano yaliyofanywa na Askofu Mkuu, Konrad Krajewski ambaye kazi yake kubwa ni kukusanya fedha toka kwa wasamaria wema na kuwapelekea maskini.

Imeelezwa kuwa Askofu Krajewski amekuwa akiambatana na Papa Francis wakati mwingine na kwenda kuwapa misaada maskini maeneo ya vijiji, mjini Vatican.

Askofu Krajewski alisema tangu zamani alipokuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Buenos Aires, Papa Francis amekuwa akipenda kwenda mijini nyakati za usiku na kuwatembelea wenye shida mbalimbali.

“Amekuwa akionyesha dalili ya kupenda kunisindikiza kwenda kuwapa misaada maskini, pindi nikiondoka kwenda kufanya kazi hiyo,” alisema Padri Krajewski.

Hata hivyo, alipoulizwa iwapo Papa aliwahi kwenda naye nje ya mji kwa ajili hiyo, Askofu Krajewski, alisita kujibu swali hilo.

Wakati huohuo, gazeti la Huffington Post limeripoti kuwa walinzi wa Uswisi, wamethibitisha kuwa Papa amekuwa akizunguka maeneo mbalimbali usiku akiwa amevalia mavazi ya kawaida ya wachungaji na kuwapa misaada, wanaume na wanawake wenye shida mbalimbali.

Tangu kuteuliwa kwake, papa Francis amevipamba vichwa vya habari duniani baada ya kuonekana akijaribu kuvaa kofia za polisi wa zimamoto, kuwaruhusu vijana wadogo wa kiume kuibusu miguu yake na kuwapigia simu waumini wake na kuzungumza nao.

Hivi karibuni, aliripotiwa katika vyombo vya habari akiwabusu na kuwafariji waumini walemavu katika Kanisa la Mtakatifu Peter, huku taarifa nyingine zikionyesha kuwa ametuma fedha zake binafsi kwa wahamiaji na wanaohangaikia mafao yao.

Alipokuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Buenos Aires, Papa Francis alifahamika kwa kutoroka usiku na kuwatafuta watu, kuzungumza nao na wakati mwingine kuwanunulia chakula.

Mapapa wengine waliopita pia wametajwa kutoroka usiku, kwa mfano papa John wa X111 alikuwa na tabia ya kutoroka usiku na kwenda mitaa ya Rome kufurahia uzuri wa jiji hilo, wakati Papa Pius wa X11 alivalia kama Mfaransa wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kwenda mipakani kuwasaidia Wayahudi wa Kirumi kisha kuwaweka katika sehemu salama.

- Mwananchi -

Tuesday, December 3, 2013

Daddy Owen kufunga ndoa mapema mwakani.

Daddy Owen. Photo-niaje
Daddy Owen
Mwimbaji Maarufu wa Muziki wa Injili toka Nchini Kenya Daddy Owen, ametangaza rasmi kufunga ndoa na Mchumba wake Fridah Wambui.

Daddy Owen amefikia Uamuzi huo baada ya kukamilisha taratibu zote za kimila, na kwasasa wanasubiri kupangwa kwa tarehe rasmi ya kufungwa kwa ndoa yao, huku akisema kuwa matarajio yao ni kufunga ndoa hiyo mapema Mwakani.

Monday, December 2, 2013

Tazama Video Mpya ya Mwimbaji Benjamin Dube.

Hii ni Video Mpya ya Wimbo wa Mwimbaji Benjamin Dube wa Afrika Kusini ujulikanao kama "Give Me Direction"