Advertise Here

Friday, November 29, 2013

Waziri Mkuu aongoza Mazishi ya Askofu Simalenga.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiweka Shada la Maua katika Kaburi la Marehemu Askofu Simalenga
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda jana aliongoza mamia ya watu kwenye ibada ya maziko ya Askofu wa saba wa Dayosisi ya South West Tanganyika ya Kanisa la Anglikana nchini, Askofu John Simalenga iliyofanyika Njombe mjini.

Waziri Mkuu akiaga Mwili wa Marehemu
 Katika ibada hiyo iliyofanyika jana, Waziri Mkuu alisema Dayosisi imepoteza mhimili muhimu lakini akawataka wawe na umoja na upendo huku wakiendelea kumtumainia Mungu.

“Mhashamu Baba Askofu Simalenga alisimikwa Julai 6, 2008. Ni miaka mitano tu ya utumishi kwenu na alikuja wakati ambapo Dayosisi hii ilikuwa imekaa kwa miaka 10 bila ya kuwa na kiongozi. Siku anawekwa wakfu nilikuwepo na ninakumbuka mlimuomba asaidie kuleta mshikamano,” alisema Waziri Mkuu.
Ibada ikiendelea
 Aliendelea kusema, “Nawaomba wanadayosisi muwe na upendo na mshikamano mkubwa miongoni mwenu hadi hapo Mungu atakapotupatia kiongozi mwingine. Tumuombe Mungu ili kiongozi huyu ajaye apatikane kwa njia ya amani.

Alimuomba mke wa marehemu, Martha pamoja na watoto wa marehemu kupokea msiba huo kwa mikono miwili na kuahidi kuwaombea faraja kwa Mwenyezi Mungu.
Mwili wa Marehemu ukiwekwa Kaburini
Waziri Mkuu ambaye alishiriki maziko kwa niaba ya Serikali, alitumia fursa hiyo kuwapa pole maaskofu, mapadri, watawa na familia zikiwa ni salamu maalumu kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye alisema yuko ziarani kwenye Mkoa mpya wa Simiyu.

Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Kusini ilipo Dayosisi hiyo, akitoa salamu za rambirambi alisema wana Njombe wamepungukiwa na nguvu kwa kuondokewa na kiongozi huyo wa dini.

“Alisaidia kuleta umoja hapa kwetu, tumempoteza mtu muhimu sana katika harakati za maendeleo ya wilaya yetu na mkoa kwa ujumla. Alisaidia kuleta umoja na upendo na sisi tuwe na upendo na amani, tuendelee kumuomba Mungu hadi tutakapoletewa msimamizi mwingine,” alisema Makinda.
Waziri Mkuu akiweka udongo katika Kaburi la Marehemu
 Katika mahubiri yake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Jacob Chimeledya alitaka waumini wote kumtazama Mungu na wamtegemee kwa sababu licha ya kwamba wanampenda askofu wao, ameona ni vema ampunzishe mtumishi wake.

“Sote tunajua kuwa katika kipindi chake, Dayosisi hii ilitulia kabisa je tutaruhusu kuondoka kwake kuzue tena chokochoko? Msiba huu usifike mahali ukaanza kututenganisha na kutoa mwanya wa kuanza kunyoosheana vidole. Tumuombe Mungu atusaidie afute machozi yetu,” alisema.

Askofu John Andrea Simalenga alizaliwa Novemba 30, 1953 na kufariki Novemba 24, 2013 baada ya kuugua kwa siku mbili. Novemba 22, mwaka huu alijisikia vibaya na alipopimwa alikutwa na malaria, kisukari na shinikizo la damu.

Alilazwa Hospitali ya Kibena, Njombe na kuruhusiwa siku iliyofuata lakini Novemba 24 alizidiwa tena na kuaga dunia. Ameacha mjane na watoto wanne.

- Habari Leo, Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu -