Advertise Here

Sunday, November 10, 2013

Kanisa Katoliki kufanya Sherehe Kubwa Miaka 75 ya Mkapa.

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa
KANISA Katoliki nchini limemuandalia sherehe kubwa itakayoambatana na misa ya shukrani, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, wakati wa kutimiza miaka 75 ya kuzaliwa kwake.

Taarifa ya serikali iliyotolewa jana kwa waandishi wa habari, imeeleza kuwa Rais Mkapa atafanyiwa ibada maalumu ya misa ya shukrani, ambayo lengo lake litakuwa kumpongeza na kumuombea maisha marefu siku ya maadhimisho ya kuzaliwa kwake.

Taarifa hiyo ya serikali imeeleza kuwa ibada ya misa ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa Mkapa itafanyika keshokutwa katika Kanisa Katoliki Upanga, Jijini Dar es Salaam na itahudhuriwa na maaskofu wote wa Kanisa Katoliki hapa nchini.

Inaeleza zaidi kuwa sambamba na maaskofu wa Kanisa Katoliki, Rais Jakaya Kikwete naye amealikwa katika sherehe hizo pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali na waliokwishastaafu.

Inatarajiwa pia watu mashuhuri waliopata kufanya kazi na Mkapa katika kipindi cha utawala wake, ndugu na marafiki zake wa muda mrefu nao watahudhuria misa na sherehe hiyo.

Watu walio karibu na familia ya Mkapa, wamekaririwa wakieleza kuwa tayari familia hiyo ilikuwa imekwishaanza kusambaza mialiko kwa watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wa kitaifa na wale wa kimataifa, ambao wana uhusiano wa karibu wa kikazi na kibinafsi na Mkapa.

Hii ni mara ya kwanza kwa familia ya Rais Mkapa kutangaza hadharani kufanya maombi maalum ya kukumbuka kuzaliwa kwa kiongozi huyo, ambapo tangu awe madarakani mpaka anamaliza uongozi wake, haikuwahi kufanyika misa ya aina yoyote ya kumuombea kwa ajili ya siku yake ya kuzaliwa.

Maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ni utamaduni uliorithiwa kutoka mataifa ya Ulaya Magharibi, ambapo sherehe za Novemba 12 za Mkapa kutimiza miaka 75 zinafahamika zaidi kwa jina la Diamond Jubilee.

Sherehe nyingine kama hizo zimepata kufanyika wakati Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipokuwa akiadhimisha miaka 75 ya kuzaliwa kwake mwaka 1997, zilizofanyika kijijini kwake Mwitongo, Butiama.

Katika sherehe hizo, Mwalimu Nyerere alizawadiwa zawadi mbalimbali, ikiwemo baiskeli aina ya swala, ambayo aliitumia hadi mwisho wa uhai wake katika shughuli zake za kilimo kijijini kwake Butiama.

- Rai Jumapili -