Advertise Here

Wednesday, November 13, 2013

Dk. Bilal azindua Maendeleo Bank ya KKKT.

Dr. Mohammed Gharib Bilal
MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, amezindua Benki ya Maendeleo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani huku akiitaka kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya fedha nchini.

Akizungumza wakati wa hotuba ya uzinduzi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam jana, Dk. Bilal alisema changamoto tatu zinazoikabili sekta ya fedha ni uhaba wa matawi ya benki vijijini, kiwango kikubwa cha riba na mikopo ya masharti magumu inayowakwamisha watumiaji.

Dk. Bilal alisema ujio wa Mendeleo Bank uwe chachu ya kushinda vita katika kukabiliana na changamoto hizo ili kutanua wigo wa ongezeko la watumiaji wa huduma za kibenki na kuharakisha maendeleo ya Mtanzania na taifa kwa jumla.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Meya wa Ilala, Jerry Silaa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadick na Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene aliyeupongeza uongozi kwa wazo la kuuza hisa ili kupata mtaji wa kuanzishia benki.

Akimkaribisha Dk. Bilal, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa, alisema Maendeleo Bank inaamini kuwa fedha ni damu ya uchumi duniani, hivyo imejizatiti kuongeza idadi ya watu ndani ya mtandao wa fedha ili kuharakisha ukuaji wa maendeleo.

“Sisi tupo tayari kwa jukumu hilo na tutakabiliana na changamoto hiyo, lakini tunaiomba serikali kupigania uimara wa taasisi za kifedha ili kuzipa nguvu katika kuharakisha maendeleo ya Watanzania na taifa,” alisema Dk. Malasusa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Bank, Ibrahim Mwangalaba, alimshukuru Dk. Bilal kuzindua benki hiyo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, na kwamba Watanzania watakaojiunga watafanya uamuzi sahihi.

- Salum Mkandemba -