Advertise Here

Saturday, November 2, 2013

Asilimia 80 ya Mapato ya Tamasha la Krismasi kujenga kituo cha Wasiojiweza.

Bw. Alex Msama
Maandalizi ya msimu wa sikukuu yameanza na kwa mara ya kwanza mwaka huu kutakuwa na Tamasha la Krismasi ambalo litazunguka katika mikoa kadhaa nchini.
 
Mwandaaji ambaye pia huandaa Tamasha la Pasaka, Alex Msama amesema amefikia uamuzi huo kutokana na msukumo wa mashabiki wa burudani ya nyimbo za Injili ambao wamekuwa wakitaka awaandalie kitu kingine.

“Marafiki wa Tamasha la Pasaka walinishauri niandae jingine wakati huu wa Sikukuu ya Krismasi kwa kuwa ni wakati wa mapumziko marefu na ni mwisho wa mwaka,” alisema Msama.

“Mwishoni mwa mwaka watu wengi husafiri kuelekea makwao hivyo kulifanya Dar es Salaam peke yake kutawanyima watu wengi uhondo huo.”

Pia waandaaji wa Tamasha hilo la Krismasi wametangaza kuwa asilimia 80 ya mapato yatakayokusanywa kwenye tamasha hilo mwaka huu yatatumika kwenye ujenzi wa kituo cha wasiojiweza Pugu jijini Dar es Salaam.

Tamasha la Krismasi linaloandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila mwaka, linatarajiwa kufanyika Desemba 25 jijini Dar es salaam.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, ilieleza kuwa asilimia nyingine 20 itatumika kulipia ada yatima wanaosoma shule mbalimbali hapa nchini.

“Asilimia 80 ya mapato tutaipeleka kwenye ujenzi wa kituo chetu cha wasiojiweza tunachotarajia kukijenga Pugu, Dar es Salaam, huwa hatubahatishi tunapodhamiria jambo letu,” alisema Msama.

Kwa mujibu wa Msama, hivi sasa wanasubiri hati kutoka Wizara ya Ardhi kuhusiana na umiliki wa eneo hilo, na kwamba suala hilo litakapokamilika ndipo mchakato wa ujenzi utakapoanza, na wana imani jambo hilo halitachukua muda mrefu.

Alieleza kuwa wakati wanaanzisha Tamasha la Pasaka mwaka 2000, dhamira yao ilikuwa kila mwaka kusaidia wasiojiweza.

“Niwashukuru wadau mbalimbali waliotusaidia kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho na mpaka sasa tuna karibu sh milioni 120. Gharama nzima ya ujenzi ni kati ya sh milioni 800 hadi bilioni moja utakapokamilika.

“Dhamira yetu ni kuwa na kituo ambacho kitasaidia Watanzania wa mikoa mbalimbali ambao hawana uwezo katika masuala ya mavazi, elimu, vyakula na mengine mengi,” alisema Msama.

Alieleza kuwa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Krismasi imeamua lifanyike Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Desemba 25 na siku inayofuata watatazama mkoa gani waupe heshima.

Alisema hilo litakuwa tamasha kubwa la nyimbo za kumsifu Mungu na litakuwa na tofauti kubwa ukilinganisha na mengine yaliyowahi kuandaliwa na kampuni yake.

- Mwananchi & Tanzania Daima -