Advertise Here

Monday, November 11, 2013

Tamasha la Krismasi kubisha Hodi Morogoro.

Alex Msama
MKOA wa Morogoro nao umeteuliwa kufanyika Tamasha la Krismasi Desemba 26.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, ilieleza kuwa wametoa nafasi kwa Morogoro kutokana na kukidhi vigezo mbalimbali ambavyo kamati yake inavitumia.

“Tamasha la Krismasi litafanyika Desemba 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

“Tumeamua hivyo kutokana na sababu mbalimbali, lakini pia tumezingatia kuwapa nafasi wasanii wakimaliza tamasha la Dar es Salaam wapate muda wa kupumzika kisha wataondoka asubuhi taratibu kuelekea Morogoro, ambako hakuna umbali mrefu. Hivyo Morogoro wajipange kutupokea,” alisema Msama.

Tamasha la Krismasi linaandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila mwaka.

Kwa mujibu wa Msama, wanataka Tamasha la Krismasi liwe bora zaidi kuliko la Pasaka kwa kualika wasanii maarufu kutoka nje na ndani ya Tanzania. Tayari msanii Upendo Nkone ameshathibitisha kushiriki tamasha hilo kubwa la nyimbo za kumsifu Mungu.

- Tanzania Daima -