Advertise Here

Wednesday, November 20, 2013

Uzima wa Milele katika Damu ya Yesu Kristo - Mwl. christopher Mwakasege (I).

Na Mwl. Christopher Mwakasege
“Basi Yesu akawaambia, Amini, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kunywa damu yake, hamna Uzima ndani yenu. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao UZIMA WA MILELE; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli; na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yohana 6:53-57).

Mtu ambaye ameula mwili wa Kristo na kuinywa damu yake ile iliyomwagika msalabani, ni yule ambaye anakaa ndani ya Yesu Kristo, na Yesu Kristo anakaa ndani yake. Kwa maneno mengine amepokea uzima wa Mungu, ambao ni uzima wa milele. Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako unapokea uzima wa milele; kwa kuwa, “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu” (Yohana 1:4).

Inatupasa tukumbuke ya kuwa, kwa mtu mmoja Adamu, dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.

Pia, inatupasa tukumbuke ya kuwa, “ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika UZIMA kwa yule mmoja, Yesu Kristo” (Warumi 5:17).

Dhambi inapoingia mahali inaleta mauti, magonjwa, uasi, ubishi, umaskini na kutokufanikiwa. Uzima wa milele unapoingia ndani ya mtu unaleta, – Uzima, uponyaji, amani, upendo, utajiri na kufanikiwa na baraka zingine za Mungu. 

UZIMA WA MILELE NA UPONYAJI

Kabla sijampokea Yesu Kristo moyoni mwangu awe Bwana na Mwokozi wangu, nilisumbuliwa sana na magonjwa.

Nakumbuka nilikuwa nasumbuliwa na maumivu ya kichwa mara kwa mara. Nilipokwenda kupimwa hospitali kwa daktari, niliambiwa nina ugonjwa wa vidonda vya tumbo ‘Ulcers’ na pia ‘High blood pressure’. Nilipewa dawa za kutumia, na pia niliambiwa nisile vyakula vya aina fulani maana vitaniongezea ugonjwa.

Niliyafuata masharti ya daktari, na nilipata nafuu kidogo. Lakini kitu cha kushangaza ni kwamba mara kwa mara magonjwa yalinirudia na kunisumbua sana – sikujua kitu cha kufanya. Baada ya miaka kadha neema ya Bwana ilifuniliwa moyoni mwangu, nikaokoka baada ya kutubu na kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wangu. Mabadiliko yaliyotokea katika maisha yangu ni makubwa mno. Wakati huo nilikuwa sijajua ni kitu gani kimetokea – lakini nilijua kuwa ninaishi maisha mapya.

Nilishangaa kuona kuwa miezi kadhaa imepita bila kusumbuliwa na magonjwa. Kichwa hakikiniuma tena, moyo uliacha kwenda mbio tena vyakula vingine nilivyokatazwa nisile na daktari havikunidhuru nilipovila tena kama mwanzo. Nilijua hakika kuwa nimepona!

Wakati huo sikuweza kufahamu kitu kilichotokea hata nikapona mara moja namna hiyo. Lakini kwa kadri ambavyo Roho Mtakatifu alivyoendelea kunikuza katika wokovu nilikuja kufahamu ya kuwa MSAMAHA WA DHAMBI UNAONGOZANA NA UPONYAJI WA MWILI.

Kabla ya mwanadamu kutenda dhambi, hakukuwa na magonjwa. Dhambi ilipoingia ilileta na magonjwa pia. Sadaka ya uhai wa Yesu Kristo msalabani ilileta msamaha na ondoleo la dhambi na madhara yake yote ikiwa ni pamoja na MAGONJWA.

Unapompokea Yesu Kristo moyoni mwako kuwa Bwana na Mwokozi wako, unampokea MPONYAJI. Roho wa Uzima wa milele anayeingia kutawala maisha yako, ni Roho wa Uponyaji anayefukuza magonjwa yote ndani yako na kukupa afya.

Ndiyo maana imeandikwa hivi; “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea (Yesu Kristo) wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na KUYACHUKUA MAGONJWA YETU” (Mathayo 8:16,17). Soma pia (Isaya 53:4,5)

Kwa kuwa alichukua dhambi zetu, dhambi hizo zimeondolewa kwetu, na tumepokea utakatifu wake. Kwa kuwa alichukua magonjwa yetu, hakuna sababu ya sisi kuendelea kuumwa kwa kuwa tumepokea uponyaji wake. Ndiyo maana imeandikwa hivi;

“Yeye mwenyewe (Yesu Kristo) alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti; ili tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na KWA KUPIGWA KWAKE MLIPONYWA” (1Petro 2:24).

Angalieni anasema, “ Kwa kupigwa kwake MLIPONYWA” na siyo ‘MTAPONYWA’. Ikiwa TULIPONYWA kwa hiyo sasa TUMEPONA!

Ndiyo maana watu wengi sana nimewasikia wakishuhudia ya kuwa magonjwa yaliyokuwa yanawasumbua kwa muda mrefu yamepona baada ya kumpokea Yesu Kristo mioyoni mwao na kuokoka.

Kuna mama mmoja alinishuhudia ya kuwa alisumbuliwa sana na majini kwa muda wa miaka kumi na mitatu. Alikwenda hospitali – hakupona. Alikwenda kwa waganga wa kienyeji – hakupona. Mwili wake ulidhoofu sana.

Siku moja neema ya Mungu ilimzukia aliamua kuokoka. Mhubiri aliposema watu wanaotaka kuokoka waje mbele, huyo mama naye alikwenda – akafanya sala ya toba na kumkaribisha Yesu Kristo moyoni mwake.

Mama huyo alinambia tangu wakati huo maumivu aliyokuwa nayo mwilini kwa miaka 13 yaliondoka. Mume wake na ndugu zake walishangaa sana. Tangu wakati huo aliookoka na kupona hadi alipokuwa ananisimulia ilikuwa imepita miaka minne, na bado alikuwa amepona na afya njema.

Kama wewe unayesoma haya unaumwa na hujaokoka, nakushauri utubu dhambi zako na umpokee Yesu Kristo moyoni mwako, na DAMU YAKE itakutakasa, na utapokea uponyaji unaouhitaji sasa. Kwa sababu imeandikwa, “ Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote” (Zaburi 103:3). 

UZIMA WA MILELE NA MABADILIKO YA TABIA

Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17)

Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi yaani, msamaha wa dhambi”.(Wakolosai 1:13,14).

Yesu Kristo alisema ukiula mwili wake na ukiinywa damu yake yeye anakaa ndani yako na wewe unakaa ndani yake – unapokea uzima wake au uzima wa milele.

Mtu akiwa ndani ya Kristo, anakuwa mtu mpya. Mtu anapokuwa ndani ya Kristo anabadilika tabia yake kwa kuwa amehamishwa toka katika nguvu za giza na tabia yake na kuingia katika ufalme wa Kristo na tabia ya Kikristo.

Mtu akiwa ndani ya Kristo anavua utu wake wa kale na kuvaa utu mpya – anavaa tabia mpya. Wakati fulani nilikuwa mji fulani hapa nchini nikihubiri mkutano wa siku nane, asubuhi moja alikuja mzee mmoja kuniona katika hotel niliyokuwa ninakaa.

Yule mzee akasema; “ Unakumbuka jana ulipoita watu wanaotaka kuokoka waje mbele waombewe, kuna mtoto mmoja alikuwa wa kwanza kufika mbele”.

Ndiyo, nakumbuka”; Nikamjibu.

Yule mzee akaendelea kusema; “Yule mtoto ni wa kwangu, na tangu jana kumetokea mabadiliko makubwa mno ya tabia, nikaona heri nije nikushirikishe”.

Nikamuuliza, “Kumetokea mabadiliko gani?

Huyu mtoto wangu”; yule mzee alieleza; “Kabla ya jana alipoamua kuokoka, alikuwa si mtii, alikuwa hapendi usafi, alikuwa hawezi hata kutandika kitanda chake akiamka asubuhi. Hata tukimwambia afagie uwanja unaozunguka nyumba yetu alikuwa hasikii. Kweli, tumempiga fimbo mpaka tuliogopa tutamuumiza. Lakini kuanzia jana alipookoka (sisi tulifikiri anatania) tabia yake imebadilika kabisa. Amekuwa mtii, kazi anajituma kufanya, amekuwa msafi, hata wakati wa usiku, anachukua biblia na kusali yeye mwenyewe – maajabu haya”.

Usikose Muendelezo wa Somo hili Jumatano ya Wiki Ijayo.