Advertise Here

Friday, December 28, 2012

Maswala ya Udini Tanzania, Maaskofu Wacharuka.

 JUKWAA la Wakristo Tanzania (TCF), limeitaka Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutoa ufafanuzi juu ya baadhi ya madai mbalimbali yanayotolewa na Waislamu dhidi ya Wakristo, vinginevyo Serikali ikiri kwamba inaunga mkono madai hayo ya Waislamu. 
TCF ni jukwaa linalojumuisha Taasisi kuu za Umoja wa Makanisa nchini, ambazo ni pamoja na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT) na Kanisa la Waadventiste Wasabato (SDA).
Tamko hilo limetokana na maazimio ya kikao cha wawakilishi wa taasisi hizo kilichofanyika Dar es Salaam, Desemba 6 mwaka huu, chini ya Mwenyekiti wake Askofu Bruno Ngonyani na Katibu wake, Mchungaji Dk. Leonard Mtaita. Lilianza kutangazwa katika ibada ya Krismasi juzi usiku na kurudiwa jana katika Ibada ya Kataifa mjini Moshi na Askofu Dk. Martin Shao.
Katika tamko hilo ambalo limechapishwa kwa ukamilifu ndani ya gazeti hili , TCF inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi juu ya madai kadhaa yanayotolewa na Waislamu mara kwa mara dhidi ya Wakristo, yakiwamo madai ya kwamba Serikali ya Tanzania imekuwa ikiongozwa na Mfumo Kristo.
Mengine ni madai ya kuwapo kwa ‘Memorandum of Understanding (M.o.U)’ ya mwaka 1992 baina ya Makanisa na Serikali kwa ajili ya huduma za Makanisa kuhusu sekta za afya na elimu, uchochezi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Kislamu dhidi ya Wakristo, tishio la kuuawa kwa maaskofu na wachungaji wa makanisa pamoja na tukio la uchomaji wa makanisa Mbagala na Zanzibar.
Kwa mujibu wa maaskofu na wachungaji hao, kuendelea kukaa kimya kwa Serikali kuhusu madai hayo ya Waislamu, kwanza kunachangia kuongezeka kwa uhusiano mbaya baina ya dini mbili hizo, na hivyo kuhatarisha umoja na mshikamano wa taifa lakini pia kunatoa taswira kwa viongozi hao wa Kanisa kujua kwamba Serikali inaunga mkono chokochoko zote hizo za Waislamu dhidi ya Wakristo.  
Kikao hicho cha TCF kimewaagiza viongozi wote wa makanisa nchini kusoma tamko hilo mbele ya waumini wao kabla ya mwisho wa mwaka huu, wakianzia na ibada za Sikukuu ya Krismsi na Mwaka Mpya kutokana na kile ambacho makanisa hayo yanasema juhudi zao za kutaka kukutana na Rais Kikwete ili wamweleze msimamo wao huo wa Kanisa nchini, kukwama.
Kuhusu madai ya kwamba Serikali ya Tanzania imekuwa ikiongozwa na Mfumo Kristo, tamko hilo la TCF linasema: “Maneno ya kashfa ya hoja kuwa nchi inaendeshwa kwa mfumo kristo, hayana msingi wowote. Jukwaa la Wakristo nchini linakanusha wazi kuwa nchi hii haiongozwi kwa mfumo kristo.
“Labda kwa kuwakumbusha tu, viongozi wote waandamizi wa ngazi ya juu Tanzania asilimia 90 ni Waislamu, itakuwaje nchi iendeshwe na mfumo kristo? Rais wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi (wote hawa ni Waislamu).
“Upande wa Zanzibar (viongozi Waislamu) ni asilimia 100. Na si kweli kwamba Zanzibar hawapo Wakristo wenye sifa za kuongoza. Hata uwakilishi wa Tume ya Kuandikwa Katiba Mpya, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu, na mifano mingine mingi tu hii ni baadhi tu.
“Nchi hii (inaendeshwa kwa) misingi ya kidemokrasia, na Serikali yake haina dini bali wananchi wake ndio wana dini. Jukwaa la Wakristo linaitaka Serikali ithibitishe ukweli huu badala ya kukaa kimya wakati maneno ya uchochezi kama haya yanaenezwa wazi na hadharani.”
Kuhusu M.o.U, tamko linasema: “Memorandum of Understanding (M.o.U) ya mwaka 1992, kwa ajili ya huduma za Makanisa (Afya na Elimu) kwa jamii ya Watanzania katika huduma za hospitali, vituo vya afya na zahanati pamoja na shule mbalimbali zinazoendeshwa na Makanisa. Kanisa limeendelea kujishughulisha na huduma hizi kwa jamii hata kabla ya uhuru na baada ya uhuru pasipo ubaguzi.
“Ili kuondoa hali ya Kanisa kuendelea kutukanwa, chuki na kukashifiwa juu ya M.o.U, ambayo ni jambo zuri la kuwahudumia Watanzania afya zao, Jukwaa la Wakristo linaitaka Serikali ama izirudishe hospitali na shule za Makanisa kwa wamiliki wake wa awali, yaani Makanisa, na zile za Waislamu warudishiwe. Kama hili haliwezekani, basi Serikali itoe tamko la ufafanuzi juu ya M.o.U hiyo, maana na makusudi yake na manufaa yake kwa Watanzania.”
Kuhusu uchochezi, matusi dhidi ya Kanisa na kuzorota kwa uhusiano baina ya Uislamu na Ukristo, Jukwaa hilo linasema: “Ni wakati wa kukubali kwamba misingi ya Haki, Amani na Upendo katika Taifa letu vimetikiswa kwa kiwango kikubwa. Uchochezi, kashfa, matusi na uchokozi wa maksudi unaofanywa na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu ukiendeshwa na kuenezwa kupitia vyombo vya habari vya kidini, mihadhara, kanda za video, CD, DVD, vipeperushi, makongamano, machapisho mbalimbali na kauli za wazi za viongozi wa siasa na dini husika, pasipo Serikali kuchukua hatua yoyote ikibakia kimya tu, inatoa taswira kwa viongozi wa Kanisa kujua kuwa Serikali inaunga mkono chokochoko hizi. Jambo hili linavyoendelea kuachwa hivi hivi, linaashilia hatari kubwa ya kimahusiano siku zijazo.
Aidha, Jukwaa hilo la makanisa nchini limeitaka Serikali kuhakikisha kwamba hadhi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere inahifadhiwa. “Huyu ni kiongozi aliyetoa maisha yake kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu akitetea Watanzania wote bila kuwabagua, akiimarisha umoja, amani na upendo kwa watu wote. Kashfa, kejeli na habari za uongo dhidi yake ni kuondoa moja ya alama muhimu ambazo kiongozi huyo alisimamia kwa ajili ya umoja wa kitaifa, mambo yote hayo yanayoenezwa yanalenga kukipotosha kizazi hiki na vizazi vijavyo juu ya juhudi binafsi za kiongozi huyo kwa Watanzania aliowapenda sana.