Advertise Here

Sunday, December 30, 2012

Mambo ya kukusaidia unapoweka Malengo ya Mwaka 2013.

Mwl. Patrick Samson Sanga
 KATIKA kuumalizia mwaka huu wa 2012, nataka nikutafakarishe kwa kukuuliza swali hili, Je! malengo yako uliyojiwekea katika mwaka 2012 katika nyanja mbalimbali kama vile kiroho, kihuduma, kifamilia, kikazi, kibiashara, kiuchumi nk yamefanikiwa kwa kiwango gani? Na kama hujafanikiwa je umejiuliza kwa nini hujafanikiwa kwa kiwango ambacho unaamini ulitakiwa kufanikiwa? Je, umegundua nini ni vikwazo vya wewe kufikia malengo yako?

Kama ukiyatafakari maswali hayo hapo juu utagundua kwamba najaribu kutaka kujua kama kwanza huwa una tabia ya kuwa na malenngo, na kisha kuweka mikakati inayotekelezeka ili kufikia hayo malengo, na mwisho kufanya tathimini   mara kwa mara ili kupima malengo yako yanafanikiwa kwa kiwango gani kadri siku zinavyozidi kwenda.

Naam najua si watu wengi sana wenye tabia ya kujiwekea malengo na hasa wapendwa. Ukiwauliza kwa nini huna malengo? atakuambia naenda kwa imani. Ukimuuliza imani maana yake nini? Atakujibu, kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo tena bayana ya yale yasiyoonekana (Waebrania 11:1).

Tatizo la wapendwa wengi ni kutokujua uhusiano uliopo kati ya imani na mtu mwenye malengo. Kulingana na tafsiri ya imani ni dhahiri kwamba, kuwa na malengo ni namna mojawapo ya kuwa na imani, kwani ili imani iwepo ni lazima kuwe na matarajio. Hivyo unapoweka malengo maana yake unaifanya imani yako kuwa na uelekeo, kwa kujua mahali unapotaka kufika.

Kuna tafsiri nyingi za malengo na hasa kwa kutegemeana na kile unachotaka kukipata au kukifikia, lakini tafsiri rahisi zaidi ni hii. Malengo ni hatua fulani katika maisha ya mtu ambayo hajaifikia na hivyo anataka kuifikia. Na jambo la msingi, unapaswa kufafanua vizuri lengo husika ambalo unataka kulifikia. Ufafanuzi mzuri wa lengo au malengo yako utakusaidia katika kujiwekea mikakati mizuri yenye kutekelezeka.

Katika ujumbe huu mfupi wa  funga mwaka ya 2012 nataka tu kukukumbusha mambo kadhaa ya msingi yatakayokusaidia unapoanza kuweka  malengo yako ya mwaka 2013.

1. Weka malengo yako mapema, kwa kuzingatia vipaumbele vyako.
Ni vema ukaweka malengo ya mwaka unaofuata kabla mwaka huo haujaingia. Mfano, kama mpaka sasa bado hujaweka malengo unayotaka kuyafikia katika mwaka 2013 basi tumia muda huu uliobaki kufanya kazi hiyo. Kwa nini nasema jambo hili, hii ni kwa sababu utekelezaji wa malengo yako unapaswa kuanza tarehe 01.01.2013 kama tukifika kwa neema yake Kristo.

Kwa hiyo kama tarehe hiyo ikifika hujapanga malengo yako jua kwamba tayari umeanza vibaya na kuna uwezekeano mkubwa wa kutokufikia malengo yako. Ikiwa ulishaweka malengo kwa kipindi cha mika mtatu, mtano au zaidi, bado pia unalazimika, kuyafafanua vizuri hayo malengo yako kwa kuzingatia mazingira yaliyopo na rasilimali utakazohitaji. Naam unapoweka malengo kumbuka kuyawekea  muda wa hilo lengo kufikiwa.

Mfano;
Moja ya malengo yangu kila mwaka kihuduma, ni kuandaa masomo yasiyopungua hamsini(50) na kuyaweka kwenye blog. Ukichukua 50 ukagawanya kwa miezi kumi na mbili unapata wastani wa masomo manne kila mwezi. Na hii ina maana kila wiki ni lazima niandae somo moja. Kwa hiyo ikipita wiki sijaandaa somo, ni dhahiri kwamba nitakwama katika kufikia malengo yangu. Nimekupa mfano huu rahisi ili uone umuhimu wa kuweka malengo mapema tena kwa kuyafunga kwenye muda.

Kwa uzoefu wangu katika kuweka malengo kikazi,kihuduma,kiuchumi, kifamilia, nk, nimejifunza na kugundua kwamba malengo ni muda, malengo ni mikakati na kisha malengo ni nidhamu uliyonayo katika kutekeleza mikakati na hasa ile inayohusu fedha. Muda ni ufunguo mkubwa wa kukusaidia kufikia malengo yako. Ukicheza na muda, huwezi kufikia malengo yako. Na kwa sababu hii ni lazima ujifunze kufikiri kimuda na kim-kakati kwa kila lengo unaloliweka.

Naam kufanikiwa kwa malengo ya Mtu binafsi, Shirika, Serikali nk kutategemea namna mtu/watendaji wa Serikali au Shirika husika wanavyotumia muda walionao, mikakati iliyopo na mwisho nidhamu yao katika utendaji wao. Naam, mambo haya matatu yakizingatiwa yatafanyika funguo za kufikia malengo yako au ya Shirika lako.
  
 2. Weka mikakati ya kutekeleza malengo yako.
Ili malengo yako yaweze kutekelezeka, sharti uwe na mikakati inayotekelezeka, vinginevyo huwezi kuyafikia malengo yako. Mikakati ni mbinu, njia utakazotumia katika kutekeleza malengo yako. Naam kwa kuwa malengo yako yanakuwa ndani ya muda fulani ni lazima na mikakati nayo iwe kimuda. Katika kuweka mikakati, kuna baadhi ya malengo yatakutaka ushirikiane na baadhi ya watu, sasa kuwa makini na nani unashirikana naye katika kuyafikia malengo yako.

3. Fanya tathmini ya utekelezaji wako wa malengo.
Watu wengi sana, huwa wanasahau sana hiki kipengele katika utekelezaji wa malengo yao, na ndio maana si wengi wanaofikia malengo yao. Tathmini unaweza ukafanya kwa vipindi viwili au vitatu kwa mwaka. Maana yangu ni kwamba unaweza uka-ugawa mwaka mara mbili na hivyo kuamua kwamba utakuwa ukifanya tathmini zako mwezi wa sita na kumi na mbili. Naam huu ndio mfumo ambao mimi binafsi huutumia. Hata hivyo kuna baadhi ya malengo huwa nayafanyia tathmini yake kila mwezi, ingawa tathmini kubwa huwa nafanya Juni na Desemba. Katika kufanya tahmini jambo kubwa ni kuangalia mikakati yako imekusaidia kwa kiwango gani kufikia malengo yako.

4. Boresha malengo kadri muda unavyokwenda, kwa kuzingatia tathmini unayoifanya.
Kama katika tathmini unayofanya mara kwa mara umegundua kwamba kuna lengo au malengo haya tekelezeki, basi kwanza litazame hilo lengo tena vizuri, kisha mikakati yake. Lazima kama siyo lengo, basi mikakati unayotumia haijakaa vizuri, na kwa hiyo unaweza kuliboresha lengo lako vizuri na hvyo mikakati yake pia. Mimi hutumia tathmini ya mwezi wa sita kurekebisha baadhi ya malengo na kisha kuboresha mikakati yake. Na kisha baada ya tathmini kubwa ya Desemba ndipo pamoja na mke wangu tunaweka malengo yetu ya mwaka unaofuta. Jambo la msingi hapa ni kuhakikisha kwamba malengo tunayoweka kila mwaka yanalenga kutufikisha kwenye malengo yetu ya miaka mitano mbele, tuliyokwisha kuyaweka tangu mwanzo.

5. Jenga mazoea ya kuyasoma na kutafakari malengo yako mara kwa mara.
Jambo hili litakuwekea msukumo wa kuhakikisha unatekeleza mikakati yako ili kuyafikia malengo yako. Mfano unaweza kuweka malengo yako kwenye Laptop/Computer yako,  unaweza ukaweka malengo yako kwenye meza yako ya kusomea au unaweza ukaweka ‘Remainder” kwenye simu yako iwe inakukumbusha kila wiki kupitia malengo yako nk. Hata hivyo ni vema ukaweka, malengo/mikakati yako, mahali ambapo ni salama kwa maana ambayo haitakuwa rahisi kwa mtu au watu wengine kuona, Shetani asije akawatumia hao katika kukwamisha malengo yako.

Kutokana somo hili, hebu angalia katika mwaka wa 2012 kama uliweka malengo, umeyafikia kwa kiwango gani? Naam kama haujafanikiwa vizuri, basi naamni somo hili litakusaidia katika kujipanga kwa mwaka 2013 ili kama kwa neema ya Mungu tukifika Desemba 2013 unapofanya tathmini ya mwisho wa mwaka uwe na sababu ya kumshukuru Mungu kwa namna alivyokusaidia kuyafikia malengo yako.

Mungu akubariki sana. Mimi na familia yangu, tunakutakia heri ya Mwaka mpya wa 2013 na Neema ya Kristo na iwe nawe daima.

Mwl. Patrick Samson Sanga
+255 755 816 800