Advertise Here

Monday, October 14, 2013

Safu ya James Kalekwa: Umejenga Juu ya Mwamba au Mchanga? - Part IV

James Kalekwa
Somo linaendelea....

Kusoma Sehemu ya Tatu, Bofya Hapa

Hesabu 14:1-5
“Mkutano wote wakapaza sauti zao wakilia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha Wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakamwambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchiya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona BWANA anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri”

Kama unaweza kupata nafasi ya kuwa karibu na Biblia yako tafadhali rejea sura ya 13 ya kitabu cha Hesabu ambayo kwa ujumla inaeleza juu ya habari ya wapelelezi 12 ambao Musa aliwatuma kuipeleleza nchi ya Kanaani.

Kati ya wapelelezi 12, ni wapelelezi 10 ambao walikuja na habari mbaya kwa wana wa Israeli: taarifa ya watu 10 wa kwanza juu ya upelelezi ilijaa vitisho, kushindwa na kila hali ya kukata tamaa. Ndipo sasa kwenye sura ya 14 mistari niliweka hapo juu utaona mrejesho (feedback) wa wateule wa Mungu juu ya taarifa maliyopokea.

Kitu ninachotaka uone ni kwamba hawa ndugu si tu kwamba walisikia taarifa bali walisikiliza taarifa (kuna tofauti kubwa kati ya kusikia na kusikiliza). Taifa zima lilikuwa makini kusikiliza, waliyaelekeza macho na masikio yao kwenye taarifa hii muhimu ya kiintelijensia. Kwahiyo maandiko niliyokuwekea hapo juu ni ufupisho (summary) wa mawazo yao juu ya ahadi ya Mungu kuingia Misri.

Wamekuwa ni watu wa kulaumu, kunung’unika, kujiona ni mateka, kutamani kifo, kutaka kurudi Misri n.k kwasababu tu wameelekeza macho na masikio yao kwenye taarifa zisizosahihi. Ni Muhimu ukakumbuka sana hapa ya kwamba Israeli walikuwa ni taifa teule la Mungu na walikuwa na ahadi zote za Mungu… Mbona hawakuziamini ahadi, mbona hawakumwamini Mungu?... Macho na masikio yalielekzwa kwingine!

Warumi 10:14
“Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikiaje pasipo muhubiri?”
Ili mtu aweze Kuokoka lazima ifikie mahali asikie… Ndiyo Paulo anafundisha hivyo kwenye kanisa la Rumi.

“Tena wamwiteje yeye wasiyemsikia?” hili ni swali muhimu sana kulichambua. Nadhani unaelewa wazi kwamba kusikia ni kazi ya masikio, amabayo ni moja ya milango ya fahamu. Kwa maana hiyo basi, ili mtu amwite Yesu ni lazima apewe taarifa hizo au kwa maneno mengine ni kwamba mtu huyo anapaswa kuyaelekeza masikio yake kusikia taarifa. Ukiona mtu ameokoka tambua kuna kazi ya milango ya fahamu kuleta taarifa kwenye nafsi ya mtu husika!

Kumbuka:
Haijalishi una miaka mingapi katika wokovu, haijalishi umewekewa mikono na watumishi wangapi, haijalishi unanena kwa lugha kwa viwango gani, haijalishi umetolewa unabii mara ngapi… kama milango yako ya fahamu imeelekezwa kwenye vyanzo vibovu vya taarifa, basi dhoruba itakapokuja, siku zako zinahesabika!!! Lakini habari njema ni kwamba: Umeanza kujifunza, umeelekeza milango yako yako kwenye fundisho hili. Mungu akusaidie sana.

Baada ya kukuonyesha walau kwa ufupi sana kwamba mwanzo wa mawazo yote ni milango ya ufahamu, ninaomba tuambatane sasa kuyaelewa mawazo kwa mapana kiasi.

Mithali 23:7a
“Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo…”

Ili uweze kuulewa kwa upana wake huu mstari ni vyema turejee Biblia za tafsiri kadhaa ili tuweze kunasa upana wa maana iliyokusudiwa.
“For as he thinks in his heart, so is he.” (NKJV)
“For as he thinketh in his soul, so is he.” (DARBY)
“For as the thoughts of his heart are, so is he.” (BBE)
“For as he hath thought in his soul, so [is] he.” (YLT)

Ukisoma tafsiri hizo kwa ujumla wake zinazungumzia “mawazo”… Kwahiyo Biblia inaposema “aonavyo” imekusudia hasa kumaanisha “awazavyo”. Kwahiyo twaweza kuusema mstari huo namana hii: “Maana awazavyo mtu nafsini mwake, ndivyo alivyo.”. Yaani kwa ukubwa wa maana yake ni kwamba MTU NI MAWAZO!

Ni wazi kwamba huwezi kuwa kinyume, juu, zaidi ama tofauti na mfumo wako wa mawazo. Kumbuka mawazo ni  hali ya ndani unayoishikilia kuhusu jambo fulani. Wakati fulani nilikuwa ninazungumza na ndugu kadhaa na ili kutambua mawazo yao kuhusu maisha ya ndoa niliwauliza, “Kwa uelewa wenu, Mwisho wa ndoa ni nini?”…

Jibu halikuwa gumu sana kutoka kwa ndugu hawa, “Mwisho wa ndoa ni talaka ndugu James.” Nikatikisa kichwa kwa maana ya kuwaelewa mawazo yao kisha nikawaambia, “Muasisi wa ndoa amekusudia kuwa mwisho wa ndoa ni kifo... Unawezaje kuutenganisha mwili mmoja”… Sasa ndugu msomaji unaona tofauti hapo?

Tafsiri yake ni kwamba mawazo ya hao ndugu ndiyo yatakayoongoza maisha yao ya ndoa… Ipo siku watatumia wazo la talaka, ipo siku watashauri kuhusu talaka, ipo siku wazo la talaka litajifunua…. Ipo siku! Kwahiyo huo ndiyo uelekeo wa maisha yao. Ule ukiri na kiapo “mpaka kifo kitakapotutenganisha…” kwao si halisi kabisa.

Mfano mwingine ni juu ya mwanzo wa maisha… Je, maisha huanza lini? Kipindi mimba inapotungwa au kipindi mtoto anapozaliwa? Majibu juu ya maswali hayo ndiyo yamezaa harakati za kuhalalisha utoaji mimba… wafanyao hivyo husema maisha huanza mtoto anapozaliwa!

Sasa Hebu fikiri kama umeoa mke mwenye mawazo hayo juu ya maisha ya mtoto… saa yoyote anaweza kufanya uamuzi wa kutoa mimba na vado akalindwa na “wanaharakati” wa “haki” za binadamu! Sijui unaelewa ninachomaanisha? Maana awazavyo mtu nafsini mwake, ndivyo alivyo! Hakuna namna yoyote ambapo mtu anaweza kuwa tofauti na mawazo yake.

Wafilipi 4:8
“Hatimaye ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza,  yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakirini hayo.”

Somo litaendelea Jumatatu Ijayo.....

 Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764