Advertise Here

Wednesday, October 30, 2013

Askofu Mkuu apinga wazo la kuwapa viongozi wa Makanisa silaha.


Bunduki na risasi.
Bunduki na Risasi
ASKOFU Mkuu wa kanisa la Redeemed Gospel nchini Kenya Arthur Kitonga amepinga wito wa baadhi ya mapasta kutaka serikali iwape bunduki ili kujikinga kutokana na mashambulizi katika makanisa.

Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu kutoka Amsterdam Jumanne, Askofu Kitonga alikariri msimamo wa kanisa lake kuhusu suala hilo ambalo  limezua mjadala katika vyombo vya habari huku wananchi wengi wakionekana kutofurahia pendekezo la mapasta.

Mashambulizi ya mara kwa mara na watu wasiojulikana hasa katika sehemu za Mombasa na Kilifi yamepelekea kuuawa kwa mapasta wawili hivi majuzi akiwemo pasta wa Kanisa la Redeemed kwa jina Charles Matole.

Katika mazishi ya Pasta Matole, viongozi wa makanisa waliilaumu serikali kwa kutowalinda vilivyo na kuitaka Serikali iwape bunduki aina ya AK47 ili wajikinge kutokana na mashambulizi ya adui.

Askofu Lambert Mbela ambaye ni Kiongozi wa kanisa la Redeemed Gospel eneo la Pwani Kaskazini alinukuliwa akiitaka serikali iyakabidhi makanisa bunduki aina ya AK47.

Lakini hapo Jumanne Askofu Kitonga alipinga jambo hilo na kusema huo sio msimamo wa kanisa.

“Tunapiga jambo la watumishi wa Mungu kupewa bunduki. Jambo hilo  halifai,”akasema Askofu Kitonga kwa njia ya simu.

Askofu huyo mkuu aliahidi kutoa maelezo zaidi kuhusu jambo hilo pindi tu atakaporejea nchini kutoka kwenye ziara yake ya Australia.

Mwito wa mapasta kujihami umezua mjadala mkali kwenye vyombo vya habari huku wengi wakisema ni kinyume na mafundisho ya Biblia  na maandili  ya Kikristo.

“Kama Wakristo hatufai kumwaga damu. Mwito wa mapasata kupewa bunduki una maana watatumia bunduki hizo kuua kinyume na amri kumi za Mungu,”akasema shabiki mmoja huku akichangia kwenye mjadala katika kituo kimoja cha Redio Jumanne.

Wengi wa waliochangia katika mjadala huo walinukuu maandishi matakatifu yanayopendekeza kutolipiza kisasi na kumwachia Mungu kupambana na maadui zao.

Amri za Mungu
Mnamo wiki jana Askofu Kitonga pamoja na viongozi wengine wapatao 200 kutoka kwa madhehebu mbalimbali ya Kiijilisti walikutana mjini Nyeri na kutoa mwito  kwa serikali izidishe usalama katika makanisa.

Viongozi hao wa makanisa walisikitishwa na ukosefu wa usalama nchini na makanisani  na wakaitaka serikali ichunguze wageni walioko nchini  kunyume cha sharia huku wakisema huenda wageni hao ndio wanaosababisha visa vya uhalifu kuongezeka.

Hata hivyo, Askofu Kitonga na wenzake hawakuitisha bunduki mbali walisema ni jukumu la serikali kuwalinda wananchi wote ikiwepo  ni pamoja  na viongozi wa makanisa.

- Swahili Hub -