Advertise Here

Wednesday, November 7, 2012

Msiba wa Mhashamu Askofu Aloysius Balina wa Mkoani Shinyanga.

Askofu Balina enzi za Uhai wake
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Mhashamu Aloysius Balina, amefariki dunia jana katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Antony Makunde, imesema kuwa Askofu Balina alifariki jana mida ya Saa 5 Asubuhi, kutokana na maradhi ya saratani ya ini yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.

Padre Makunde alisema kuwa, mapema mwaka huu, Askofu Balina alipelekwa Ujerumani kwa matibabu, na akarejea nchini akiwa mwenye afya njema.

Hata hivyo, miezi michache alianza tena kusumbuliwa na ugonjwa huo, na afya yake ilizidi kudorora ambapo mwezi uliopita, alilazwa katika Hospitali ya Bugando kabla ya kufikwa na umauti jana.

Askofu Balina alizaliwa Juni 21,1945, Ntuzu, Bariadi mkoani Shinyanga. Baada ya kuhitimu masomo yake mbalimbali, alipewa daraja la upadri Mei 26, 1971.

Kutokana na utumishi wake mwema, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alimteua kuwa askofu wa Jimbo la Geita mwaka 1985. Septemba 1997, aliteuliwa kuwa askofu wa Jimbo la Shinyanga ambako alilitumikia hadi jana alipoitwa na Mungu.

Wakati wa uhai wake, Askofu Balina alishikilia nafasi kadhaa ndani ya Baraza la Maaskofu ambako kwa miaka mingi alikuwa mwenyekiti wa idara ya afya ya baraza hilo, na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Bugando.

Askofu Balina ni mmoja wa maaskofu wachache wa Kikatoliki ambaye alitazama maisha ya waamini wake na watu wote wa majimbo ya Geita na Shinyanga, katika mahitaji yote ya kiroho na kimwili.

Aidha, ni mmoja wa viongozi wa dini aliyesimamia kikamilifu kuinua Hospitali ya Bugando na hasa juhudi zake zilizosukuma kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Afya Bugando.

Kadhalika, alifanya kazi kubwa akishirikiana na maaskofu wenzake, kuhakikisha kuwa kinaanzishwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustine, na hatimaye kufikia mafanikio makubwa.

Salamu za Rambirambi toka kwa Rais Jakaya Kikwete kwa Kanisa Katoliki Tanzania.
Askofu Balina(Kushoto) enzi za Uhai wake akiwa na Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana Jumanne, Novemba 6, 2012, amelitumia Kanisa Katoliki Tanzania salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Baba Askofu Aloysius Balina aliyefariki dunia majira ya saa tano asubuhi leo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza.
 
Katika salamu zake za rambirambi kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mshahamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Mhashamu Baba Askofu Aloysius Balina ambaye nimeambiwa ameaga dunia asubuhi ya leo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Buganda, Mwanza, kwa ugonjwa wa kansa.”
 
Amesema Rais Kikwete katika salamu zake hizo: “Mhashamu Baba Askofu Balina alikuwa kiongozi hodari na mwadilifu ambaye siyo tu alichangia kipekee katika mwenendo mzuri wa kiroho wa waumini wa Kanisa Katoliki bali pia katika maendeleo ya Watanzania wote kwa jumla.”
 
“Kifo chake kimetuondolea kiongozi mwema ambaye tutazikosa busara zake na uongozi wake. Lakini napenda kukuhakishia Mshahamu Baba Askofu kuwa sisi ndani ya Serikali tutaendelea kutambua na kuthamini mchango wa Askofu Balina alioutoa kwa nchi yetu katika maisha yake,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
 
“Baba Askofu, nakuomba upokee salamu za rambirambi za Serikali ninayoiongoza na zangu binafsi kufuatia msiba huu mkubwa. Aidha, kupitia kwako, naomba uwafikishie salamu zangu viongozi na waumini wote wa Kanisa Katoliki kwa kuondokewa na kiongozi na muumini mwenzao. Naungana nanyi kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweka pema peponi roho ya Marehemu. Amen.”

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
6 Novemba, 2012