Advertise Here

Friday, November 16, 2012

Kanisa Katoliki Parokia ya Kihosa lavamiva. Mlinzi ajeruhiwa vibaya.

Muonekano wa Nje wa Kanisa Katoliki Porokia ya Kihesa
WATU wasiofahamika usiku wa kuamkia Jana wamevamia Kanisa Katoliki Parokia ya Kihesa Jimbo la Iringa, Mkoani Iringa na kuiba baadhi ya mali huku mlinzi wa Kanisa hilo Bathlomeo Nzigilwa akijeruhiwa vibaya na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa.
 
Akizungumzia tukio hilo Sista Lucy Grace Mgata amesema aligungua kuwa kunauvamizi majira ya  alfajiri alipofika kanisani hapo kwa ajili ya ibada ya Misa za kila siku zinazoanza saa 12:00 asubuhi.

“Mimi nilifika hapa kanisani saa 11:40 alfajiri, na nilipofungua mlango wa kanisa kwa ajili ya misa nilishangaa mlango ukiwa wazi na kumuona  mlinzi amekaa kwenye kiti huku kichwa chake kikiwa kimeinamishwa chini na kufunikwa kofia, nilijua amelala kumbe alikuwa ameumizwa na hajitambui," Alisema Sista Mgata. 
Ndani ya Ofisi baada ya Uharibifu
Amesema  alipomsogelea mlinzi huyo aliona damu inatiririka chini na mwili wake ukiwa umelowa kwa damu na hapo ndipo alipokwenda kugonga nyumba ya padre kutoa taarifa.

Pamoja na kuvunjwa kwa Kanisa hilo ofisi ya parokia nayo ilivunjwa huku vitabu, na kumbukumbu mbalimbali zikiwa zimechanwa na kuwa mavazi ya ibada na vifaa mbalimbali vya ibada vimeharibiwa vibaya,  Taberenakulo ndogo nayo ikiharibiwa, msalaba kuvunjwa pamoja na Hostia Takatifu zikimwagwa kila mahali.

Damu zilizovuja baada ya mlinzi kupigwa
Sista Mgata  amesema hela za watumishi wa Artare walizokuwa wakichangishana pamoja na fedha za chama cha kitume cha utume wa Fatima zimechukuliwa japo bado hazijajulikana ni kiasi gani.

“Pia wamechukua hela ambazo watumishi wa artare walikuwa wakichangishana kwa ajili ya matumizi ya umoja wao, na fedha za chama cha kitume cha utume wa Fatima nazo wamechukua ingawa sijajuwa ilikuwa ni kiasi gani mpaka wao wenyewe waje waeleze kulikuwa na shilingi ngapi," Alisema sista Mgata.
Muuguzi mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa Rustica Tung'ombe akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya mlinzi aliyeumizwa na kufukishwa hospitalini hapo leo
 Kwa upande wake Katekista Agustino Luhama mhudumu wa ofisi ya Parokia alisema hela anazozikumbuka kwa harakaharaka ambazo zimechukuliwa na wavamizi hao ni zaidi ya shilingi laki tano.

“Hela ninazozikumbuka kwa harakaharaka ambazo zimechukuliwa ni zaidi ya shilingi laki tano lakini zingine sijapata idadi kwa sababu nilikuwa sijazijumlisha na zingine nilizipokea jana kutoka kwa waamini mbalimbali” alisema Kat. Luhama.

Padre Aloyce Mdemu ambaye pia ni Makamu wa Askofu wa jimbo hilo alisema bado ni mapema kujua thamani ya uharibifu uliofanyika kwa kuwa bado wanaendelea na uchunguzi wa vifaa vingine na maeneo mengine ambayo huenda hayajagundulika.
Mlinzi aliyejeruhiwa akiwa hospitali
“Ni kweli tukio hili limetokea na kutushtua sana hata kuumizwa nuzura kuuawa mlinzi wetu lakini bado ni pame sana kujua thamani ya uharibifu wa vitu vyote vilivyoharibiwa kwa sababu tunaendelea na uchunguzi wa vitu vingine na maeneo mengine ambayo huenda nayo yameharibiwa na hayajajulikana. Tutakapokuwa tumekamilisha, taarifa zitatolewa” alisema Pd. Mdemu.

Hata hivyo Muuguzi mfawidhi wa hospitali ya Mkoa wa Iringa Rustica Tung’ombe alikiri kumpokea majeruhi ambaye ni mlinzi wa kanisa hilo na kusema kuwa hali yake ni mbaya japo kuwa anaendelea kupatiwa matibabu.

“Tumempokea majeruhi Bathlomeo Nzigilwa mlinzi wa Kanisa ambaye ni mkazi wa kwa Semtema akiwa na hali mbaya, na bado hajapata ufahamu, ila anaendelea na matibabu,” alisema Tung’ombe.