Advertise Here

Sunday, March 17, 2013

Maganga James Gwensaga: Kutoka kuwa Mpiga Debe mpaka kuwa Meneja wa vituo viwili vya Radio za Kikristo.

Maganga James Gwensaga
Jina lake kamili ni Maganga James Gwensaga Almaarufu kama President. Ni mtoto wa pekee kwa Baba yake Mzee Julius Mashenene Gwensaga na Mama yake, ingawa kwa upande wa Baba ana dada zake wanne na kwa upande wa Mama ana wadogo zake wanne pia.

Alizaliwa mkoani Morogoro kijiji cha Kichangani, wakati Mama yake akiwa ni mluguru wa Mikese, na Baba yake akiwa ni Msumbwa wa Geita.

Baada ya kuzaliwa Mkoani Morogoro, Baba yake mzazi Mzee Julius Mashenene Gwensaga ambaye ni marehemu kwa sasa, alipata uhamisho wa kikazi kutoka Morogoro kwenda Mkoani Iringa.
Maganga akiwa katika Shughuli za uchoraji enzi hizo
Toka walipofika Iringa baba yake alikaa kwa muda wa miaka mine tu na kufariki na kumuacha Maganga akiwa mikononi mwa mama yake wa kufikia ambaye alimlea toka wakati huo, baada ya mama yake mzazi kukataa kuondoka na baba yake Maganga kutoka Morogoro kwenda Iringa.

Baada ya baba yake kufariki ambaye alikuwa ni mwajiliwa wa Wizara ya ujenzi kitengo cha Ufundi katika Kiwanda cha Karatasi cha Mgororo kilichopo Mkoani Iringa, ililazimika kurudi Dar es salaam kwani uongozi wa kiwanda cha karatasi cha mgororo hakikuwa na mkataba na wao isipokuwa baba yake ambaye alishafariki.

Kutoka Iringa walienda Dar es salaam, na mwaka 1989 Maganga akaanza darasa la kwanza katika shule ya msingi Mianzini iliyopo Mburahati Mianzini.

Akiwa hapo shule ya msingi, Maganga alishiriki michezo mbalimbali na jambo analokumbuka akiwa darasa la nne alichaguliwa kujiunga na bendi ya shule jambo ambalo halikuwezekana kwa mwanafunzi yeyote wa darasa la nne kwani ilikuwa ni mpaka ufike darasa la sita ndipo ujiunge na Bendi ya Shule.

Alipomaliza darasa la Saba Maganga hakuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya serikali na hivyo kulazimika kusoma kwenye shule za kulipia(Private School), ambapo alijiunga na elimu ya sekondari kwa masomo ya jioni.
Enzi hizo Maganga akiwa anafuga rasta
Alimaliza elimu ya sekondari mwaka 1999 na kuanza kufuga nywele rasmi kama Rasta. Mwaka 2000 aliingia katika masuala ya uandishi wa habari na uchoraji wa katuni wakati huo akichorea gazeti la maisha na sanifu ya jijini Dar es salaam.

Mbali na uchoraji wa katuni katika Magazeti, lakini pia alikuwa ni mwandishi wa hadithi mbalimbali za maandishi katika gazeti la Majira.

Maganga anasema, “Namshukuru sana dada yangu Juliana Gwensaga aliyekuwa akinitia moyo katika fani hii ya uandishi wa habari.”

Mwaka 2005 Maganga alikata Rasta zake zote na kubaki na nywela za kawaida tu baada ya kufuga Rasta hizo kwa miaka 6. Ilipofika Mwaka 2007 Maganga alikutana na mwanadada Peresia Shilla na kukubaliana kuishi pamoja kama Mke na Mume, na kweli mwaka huo huo walifunga ndoa na kwa sasa wana watoto wawili wote wa kiume ambao ni Brian(mkubwa) na Brighton(mdogo).
Maganga akiwa na Mkewe Peresia Shila siku ya Harusi yao
Kwa mara ya kwanza alikutana na Askofu Magike wa Jijini Mwanza mwaka 2005 jijijni Dar es salaa, wakati huo Maganga akiwa ni msanii wa uchoraji na alikuwa na kibanda chake cha uchoraji maeneo ya mbezi mwisho jijini Dar es salaam.

Wakati akifanya shughuli hiyo ya uchoraji, pia Maganga alikuwa akihubiri Injili katika kituo cha mabasi cha mbezi baada ya kuokoka, huku akiwa ni mwajiriwa katika shule ya msingi St. Ann’s kama mwalimu wa somo la uchoraji.

Baada ya kukutana na Askofu Magike katika moja wapo ya mikutano ya Injili hapo Dar es salaam, Askofu Magike alimuomba Maganga ampigie picha za video katika mkutano wake wa Injili wa Jijini Dar na baada ya mkutano huo, alimuomba tena ampigie picha za video kwenye harambee ya kuchangia uanzishwaji wa radio ya Kikristo ya Living Water katika Jiji la Mwanza.

Baada ya harambee hiyo haukupita muda mrefu, Akofu Magike akamuita Maganga Jijini Mwanza akimwambia kuwa ile radio waliyokuwa wanaifanyia harambee imeanza kuruka hewani hivyo kama anaweza aende Mwanza.

Kweli Maganga alienda Mwanza na kuiacha familia yake Jijini Dar lakini baadaye ilikuja kujiunga naye ambapo mpaka sasa yuko nayo huko jijini Mwanza.
Watoto wa Maganga. Brighton(Kushoto), na Brian(Kulia)
Maganga anaongeza kwa kusema kuwa ” Baada ya muda flani nilichaguliwa kuwa Meneja wa kwanza hapo Living Water na baadaye nikaacha kazi na kwenda katika Radio nyingine ya Kikristo ya  Hhc Alive Fm ya Jijini Mwanza pia nikawa Meneja katika kituo hicho. Badae nikatoka na kwenda Afya Radio kama Mtangazaji wa kawaida na ndipo nikarudi tena Living water na kuwa Meneja kwa mara nyingine tena katika kituo hicho cha Radio. Hapo sikukaa sana tena ndipo Mwanzoni mwa Mwaka huu 2013 nikarudi Hhc Alive Fm na kuwa Meneja tena”

“Nimejifunza kutokukata tamaa katika maisha hasa nikikumbuka toka wakati ule nikiwa mchoraji, kwa kweli kuna wakati ilipita wiki nzima bila kupata kazi, na kuna kipindi nilifanya mpaka kazi ya kupiga debe ili walau Mkono uende kinywani. Lakini kwa sasa namshukuru Mungu hata kama sina gari, lakini la ofisi lipo natembelea ingawa naamini la kwangu linakuja.” – Aliongeza Maganga.
Maganga akiwa katika Studio za Afya Radio
Kwa sasa Maganga ni Station Manager wa radio ya kikristo ya Jijini Mwanza ya Hhc Alive Fm (91.9Mhz) “Sauti ya Tumaini” na pia anajiandaa kuchukua masomo ya Diploma ya uandishi wa habari katika chuo cha uandishi wa habari na utangazaji cha Arusha baada ya kusoma Certificate ya Uandishi wa Habari katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal kilichopo Jijini Dar es salaam.

- To God Be The Glory -