Advertise Here

Tuesday, March 26, 2013

Nitamtambuaje Mke ambaye Mungu ameniandalia?

SWALI
Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu!
Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa ajili yenu kwa huduma mnayoitoa ambayo imekuwa msaada katika maisha yangu kama mkristo na kama mwanajamii. Mungu awabariki sana.


Pili naomba msaada wa maarifa juu ya namna ya Kumtambua mke ambaye Mungu ameniandalia. Nimefanya maombi ya kumuomba Mungu mke mwema tangu septemba 2008 hadi sasa lakini bado sijapokea majibu ya maombi yangu. Ninaamini ninasumbuliwa na Tatizo la upokeaji wa majibu ya maombi yangu jambo ambalo linahatarisha ustawi wangu kiroho.


Naomba kwa manufaa ya wengine pia ambao wana tatizo kama langu. Asante sana na Mungu awatimizieni haja za mioyo yenu na kuimarisha huduma yenu ili watu wengi zaidi waimarike kiroho.


Naitwa Lucas


Majibu;

Hello Lucas, tunakusalimu kwa jina la Bwana, ahsante kutuombea, kututia moyo na kwa swali lako ambalo naamini majibu yake yatawafaa wengi kama ulivyoshauri katika swali lako.


Kaka Lucas swali lako ni pana sana na ‘it is more personal’ kimajibu, lakini namshukuru Roho Mtakatifu anayeweza kutupa majibu ya kutufaa .Katika swali lako nimegundua mambo mawili ya msingi ambayo natakiwa kuyatolea ufafanuzi, moja ni namna unavyoweza kumtambua mke ambaye Mungu amekuandalia na pili namna bora ya kuomba yenye kuleta matokeo.


Katika kujibu maswali haya mawili nitazungumzia mambo manne yafuatayo ambayo naamini baada ya kuwa umeyasoma haya utapata ufahamu wa kukusaidia katika kufanya maamuzi hayo yanayokukabili;


Jambo la kwanza; Mungu hatumii njia au mfumo wa aina moja katika kukujulisha wewe mwenzi wa maisha yako (Isaya 55:8).

Oktoba 2006 naliandika kitabu kuhusu Njia kumi za Kibiblia zitakazokusaidia kumjua na kumpata mwenzi wako wa maisha. Katika ukursa wa nne wa kitabu hicho ndipo nilipoandika wazo hili hapo juu, kwamba, Mungu hatumii njia au mfumo wa aina moja katika kumjulisha mtu mwenzi wake wa maisha.


Nimeona hata sasa nianze na msingi huu na hii ni kwa sababu vijana wengi hujaribu kuuliza wanandoa waliotangulia kwamba waliwapataje wenzi wao wa maisha kwa dhana ya uongozi wa Mungu? Kutokana na majibu ambayo vijana hao hupewa wengi humuomba Mungu na wanasubiri, Mungu aseme nao kwa njia ile aliyotumia kusema na mtu mwingine.


Kibiblia wazo hili siyo sahihi kwani, Mungu ana njia nyingi sana za kusema na watu wake katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na nani atakuwa mwenzi wako wa maisha. Kwa mtu mmoja Mungu anaweza akasema naye kwa ndoto, mwingine kwa sauti yake, na mwingine kwa maono, mwingine kwa mafunuo, mwingine kwa amani ya Kristo, mwingine kwa kutumia watumishi/wachungaji nk

Jambo ninalojaribu kukuonyesha hapa ndugu Lucas ni kwamba ‘Mungu ana namna yake ya kukusaidia kumtambua mwenzi wako wa maisha, ambayo si lazima ifanane na ya mtu mwingine’.

Na mara nyingi namna/njia hiyo haitofautiani sana na ile ambayo Mungu hutumia kusema nawe katika mambo mbalimbali. Hivyo tafuta kujua njia ambayo Mungu huwa anatumia kusema na wewe katika mambo mbalilmbali, naam kwa hiyo aweza kusema na wewe hata kuhusu mwenzi wako.


Jambo la pili; Jenga na kuboresha mahusiano yako na Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu ndiye aliyepewa jukumu la kuwa Msaidizi wako hapa duniani katika kufanya maamuzi mbalimbali. Watu wengi leo wanakwama au wanajikuta wamefanya maamuzi mabaya kwa kosa la kutokumshirikisha Roho Mtakatifu awasaidie. Mwambie Roho Mtakatifu nahitaji mwenzi(Mke), nisaidie kumtambua yupi ni wa kwangu, naomba uongozi wako. Roho Mtakatifu kwa hakika atakuongoza katika njia sahihi (Zaburi 32:8).

Jambo la msingi ni kwa wewe kuboresha mahusiano yako na yake ili kuruhusu mawasilano mazuri kati yenu. Kumbuka mawasilano hutegemea mahusiano. Na jambo la msingi katika kuboresha mahusiano ni utakatifu na kutenga muda wa kuzungumza naye kwa njia ya maombi na neno.


Jambo la tatu; Jifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie kuhusu mwenzi wa maisha yako.

Hili ni jambo lingine la msingi kuzingatia. Endapo umeamua kufuata au kutafuta kumjua mwenzi wako kutoka kwa Bwana, basi ni vema ukaruhusu mapenzi yake juu yako yatimie. Wengi huenda mbele za Bwana wakimuuliza jambo hili lakini anapoleta wazo/jibu lake juu ya nani anafaa, wengi wakishamtazama huyo muhusika kimwili na kwa vigezo vyao humkataa na kusema si Mungu. Ni vizuri ukafahamu kwamba, kama Mungu ndiye aliyemleta mtu wa kwanza kwako na wewe kwa sababu zako binafsi ukasema huyu si wa kutoka kwa Bwana, maana yake umemzuia  Mungu asikusaidie kwenye hilo eneo, na hivyo usitegemee kusikia tena kutoka kwake, labda mpaka ujue kosa lako na kuomba toba.


Kumbuka usimuombe Mungu akujulishe mwenzi wako wa maisha wakati moyoni mwako tayari kuna mtu au watu ambao umeshadhamiria kutaka mmoja wao awe mwenzi wako, Mungu hawezi kusema hapo. Ikiwa unataka Mungu ahusike mpe asilimia mia moja hatafanya makosa kama Mwandamu.


Jambo la nne; Jifunze kuomba kimaswali

Najiribu kufikiri kwa nini umeomba tangu Septemba 2008 hadi sasa Mungu asijibu? Kwa ufahamu nilionao katika Kristo nina hakika yeye alisha-kujibu ila wewe ndiyo hukuelewa kwamba alijibu. Nina uhakika huo kwa sababu mtu amwendeaye Mungu kutaka kujua jambo, Mungu humjibu mtu huyo ili kumsaidia asipotee katika jambo hilo.


Naamini shida ipo kwako, huenda jibu ulilokuwa unataka wewe ni kuambiwa fulani ndiye mwenzi wako, kumbe kwa Mungu huenda alikuwa anasema huu si muda wake endelea kuomba maana kwa kila jambo kuna majira yake. Zaidi huenda shida iko kwenye namna unavyoomba na namna unavyopokea, au kuelewa Mungu anapoleta jibu.


Ili kuweza kupata ufumbuzi juu ya jambo hili jifunze kutumia mfumo wa maswali katika maombi yako, naamini utaona matokeo yake. Jifunze kuyatengeneza maombi yako kimaswali, omba huku ukitaka kujua/ukitafuta ufumbuzi wa lile unaloliombea kwa Mungu.

Swali limejibiwa na;
Mwl. Patrick Samson Sanga

+255 755 816 800