Advertise Here

Wednesday, March 13, 2013

Sipho Makhabane toka Afrika Kusini kushiriki Tamasha la Pasaka.

Mwimbaji Sipho Makhabane
BAADA ya mwaka jana mwimbaji mahiri Rebecca Malope wa Afrika Kusini kutumbuiza Tamasha la Pasaka jijini Dar es Salaam, safari hii ni zamu ya mwimbaji mahiri kutoka nchini humo, Sipho Makhabane.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, raia huyo wa Afrika Kusini amethibitisha kupamba tamasha hilo la Machi 31 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.



“Ni mafanikio mengine kwa tamasha la mwaka huu, mwaka jana tulifanikiwa kumpata Malope (Rebecca), mwaka huu tumemleta Sipho,” alisema Msama, mwasisi wa matamasha ya injili inchini.

Kuthibitisha kwa mwimbaji wa kimataifa Makhabane anayetamba na vibao vingi kikiwAmo cha ‘Over and Over,’ kunazidi kuongeza idadi ya waimbaji kutoka nje ambapo sasa wamefikia wanne.

Wengine kutoka nje ni Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa raia wa DR Congo anayeishi Kenya na Kwaya ya Ambassadors of Christ ya Kigali, Rwanda maarufu kama ‘Kwetu Pazuri’.

“Ni msanii mwenye uwezo mkubwa na aliyejijengea jina, hivyo ujio wake ni jambo la kufurahia,” alisema Msana na kuongeza kuwa msanii huyo amekuwa akipata mafanikio katika muziki wa injili karibu kila mwaka.

Nyimbo zake nyingine ni kama ‘Moya Wami’, ‘Indonga’, ‘Akukhalwa’, ‘Nguy’zolo’, ‘Yizwa Nkosiseju’, ‘Hlalanami Nkosi Jesu’, ‘Yek’intokozo’, ‘Injabulo’, ‘Hlalanami Jesu’, ‘Makadunyiswe’, ‘Vuka Mphemlo’, ‘Mphefumlo’ na ‘Moya Wami’.

Wasanii wa Tanzania ambao watashiriki tamasha hilo mwaka huu ni Rose Muhando, John Lissu, Upendo Nkone, kwaya ya Kinondoni Revival na kundi la Glorious Celebration.

Tamasha la Pasaka litafanyika Dar es Salaam Machi 31 na litaendelea Aprili mosi kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, wakati Aprili 3 ni Uwanja wa Samora, Iringa na Aprili 6 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na siku inayofuata itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Huyu ni Sipho Makhabane

- Tanzania Daima -