Advertise Here

Monday, September 16, 2013

Safu ya James Kalekwa: Mambo yakupasayo Kujua Juu ya Maamuzi - Part III.

Mwl. James Kalekwa
 Somo linaendelea.....

Kusoma Sehemu ya Pili Bofya Hapa

Maisha baada ya kuzaliwa mpaka kifo
 Japo jamii nyingi huyatazama maisha ya mwanadamu katika hatua tatu: kuzaliwa, kuishi na kufa na kimantiki inaweza kuonekana ni kweli lakini unapaswa kung’amua ya kwamba kuzaliwa ni mlango wa kuingilia (entrance) na kifo ni mlango wa kutokea (exit) kwenye jengo fulani. Katikati ya hii miimo miwili ya kimaisha kuna wakati mkubwa wa maisha ambao ni vyema tukaelekeza mioyo yetu ili tujipatie maarifa katika hilo.

Luka 2:40, 52
Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.”
Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.”

Kupitia mistari hii unaweza kuona ya kwamba yule mtoto alipozaliwa hakukua ndani ya siku moja na kufa hapo hapo, bali alipitia hatua zote za ukuaji- naamini unaelewa ya kwamba ukuaji ni hatua, si mara moja (growth is gradual not sudden). Kadiri alivyoendelea kukua ndivyo alivyoukaribia mwisho wa maisha yake, lakini hakuwa anaishi kusubiri kifo. Kwa namna ya kawaida utagundua kwamba alikuwa anaishi kama vile hakuna kifo mbele yake, aliishi kwa kukamilisha kusudi la kuwepo kwake kabla ya kifo.

Kitu ninachotaka uone hapa ni kwamba kuna kiasi cha muda (time gap) kati ya kuzaliwa na kufa au kwa maneno mengine kuna daraja linalounganisho hii miisho miwili ya maisha. Wacha nikuonyeshe kwa maneno rahisi kabisa… ni kwamba, wewe hukufa mara tu baada ya kuzaliwa (japo kuna matukio kama hayo) bali umeendelea kuishi mpaka leo ukielekea kifoni. Hicho ndiyo kipindi ninachopenda tukitazame mahala hapa.

Yoeli 3:14
Makutano makubwa, makutano makubwa, wamo katika bonde la kukata maneno! Kwa maana siku ya BWANA i karibu, katika bonde la kukata maneno.”

Sote tunatambua wazi ya kwamba siku ya Bwana haitakuja kwenye ulimwengu wa maisha ya kabla ya kuzaliwa kwetu na twajua ya kwamba siku ya Bwana haitakuja kwenye ulimwengu ule wa maisha baada ya kifo. Siku ya Bwana inakuja kwenye ulimwengu huu wa maisha ya katikati ya kuzaliwa na kifo. Biblia inatufundisha ya kwamba Yesu hatakuja mara ya pili katika ulimwengu wa maisha baada ya kifo, bali atakuja kwenye ulimwengu huu na hata ndugu waliotangulia kuondoka kwa njia ya kifo na kuingia kwenye ulimwengu wa maisha baada ya kifo, nao watarejeshwa ili kuungana nasi kwenye huu ulimwengu (upande huu wa maisha) ndipo taratibu zingine zitafuata. (Ufunuo 1:7; 1 Thesalonike 4:13-17).

Kwa lugha ya moja kwa moja ni kwamba bonde la kukata maneno ni kipindi kati ya kuzaliwa mpaka kifo, ni hilo jengo fulani ambalo mtu huingia kwa kuzaliwa na huondoka kwa kifo, yaani ni maisha mtu aishiyo baada ya kuzaliwa na kabla ya kufa. Ndugu msomaji, naomba uanze kusoma fundisho hili kwa kujitambua kwamba umo ndani ya bonde la kukata maneno!

Maisha baada ya kifo
 Biblia kwa namna nyingi sana inatuthibitishia ya kwamba kuna maisha baada ya maisha haya ya sasa na maisha yajayo baada ya haya ni maisha yaliyo na umilele- yaani yasiyo na mwisho! Lakini si watu wote tutakuwa na maisha sawasawa katika ulimwengu wa maisha baada ya kifo, kutakuwa na makundi mawili makubwa: mkono wa kuume na mkono wa kushoto; kondoo na mbuzi; wema na waovu; paradiso pamoja na Mungu au ziwa la moto pamoja na shetani na malaika zake. Maisha ya milele yatakuwa na pande mbili tu na habari njema ni kwamba pande zote zitakuwa ni za milele.

Katika muhula huu wa maisha hakuna muda wa kufanya maamuzi na tena si muhula sahihi kufanya maamuzi. Pia ni muhimu kutambua ya kwamba muhula huu ni muhula wa kuvuna kutoka kwenye muhula wa pili wa maisha, kuwajibika juu ya ukataji wa maneno ulioufanya wakati wote ulipokuwa ndani ya bonde.

Waebrania 9:27
“Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu.”

Mwandishi waraka kwa Waebrania analeta picha ya kisheria na kimahakama ya kwamba baada tu ya kufa ni hukumu. Kwa uelewa wa shughuli za kimahakama lazima ujue ya kwamba hukumu haitolewi kutokana na matakwa, maoni au fikra za upande mmoja (jaji, utetezi na mashitaka) bali maamuzi ya mahakama yaani hukumu hutolewa kwa kuakisi ushahidi uliotolewa mahakamani. Kwa namna nyepesi ya kueleweka ni kwamba jaji hutumia jumla ya ushahidi kama ukweli (facts) na malighafi ya kufanya maamuzi ya kimahakama. Kwahiyo, jaji/hakimu hatoi maamuzi yake hewani bali kwenye maisha ya mshitakiwa husika. Kwa mfano mwepesi ni kwamba hakuna mahakama duniani inaweza kunihukumu kwa kesi ya uhaini hata kama utolewe ushahidi uliojaa vitabu vikubwa (volumes of books).

Hakuna mahakama inaweza kumuhukumu kifo ndugu Joshua (nimetumia jina kutolea mfano) hata kama kesi itakuwa na mashahidi milioni moja. Kwanini? Kwasababu hakuna alama hiyo kwenye maisha yangu; hakuna mtiririko huo kwenye maisha ya ndugu Joshua. Si kwamba mahakama haina uwezo na wala si kwamba hakimu/jaji ana mamlaka kidogo, bali ni kwasababu maisha yetu hayastahili hukumu hiyo. Kitu ninachotaka uone ni kwamba kimsingi anayeamua mwenendo wa kesi au aina ya hukumu ni muhusika (mshitakiwa) na si mtu mwingine yeyote.
Hebu nikuonyeshe mfano wenye maelezo mengi zaidi kutoka kwenye kinywa cha ahukumuye kwa haki, Yesu Krsito mwenyewe.

Luka 16: 25-26
“Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo hivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.”

Kuielewa vizuri hii habari unaweza kuirejea kutoka kwenye mstari wa 19 mpaka wa 31. Utaona ya kwamba mistari niliyoiweka hapo juu ni matokeo baada ya maisha ya Lazaro na tajiri wakiwa duniani. Kosa la yule ndugu halikuwa utajiri bali ilikuwa ni nia yake atumiapo utajiri ule, “…aliyevaa  nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa…”. Siku zote za maisha alikuwa na nia ya kufanya anasa- alivaa na kula kwa anasa! Lakini Lazaro hakuwa na nia ya anasa, kula na kuvaa kwake kulikuwa ni kukidhi mahitaji muhimu… Nia zao kuelekea chakula na mavazi zilikuwa ni tofauti, umeona, eeh?

Baada ya kufa ndiyo wanakutana katika maisha ya milele lakini wakiwa kwenye pande mbili tofauti. Kitu gani kiliamua utofauti huo? Hakuna sehemu Biblia inatuambia kwamba baada ya kufa walifika mahala pa njia panda na kupewa nafasi za kuchagua wapi watumie maisha yao ya milele, hakuna! Maisha yao ya baada ya kifo yaliamuliwa na mfumo wa maisha yao kabla ya kifo – kuwa kifuani mwa Ibrahimu au kwenye mateso ni uamuzi wao wenyewe (tajiri na Lazaro) na uamuzi huo hufanyika kwenye maisha kabla ya kifo.

Kitu ninachotaka ujifunze hapa ni kwamba maisha ya baada ya kifo si sehemu ya kufanya maamuzi wala kujitafutia fursa ya kufanya hivyo! Baada ya kifo ni hukumu na hukumu hiyo inatokana na vile maisha ya kabla ya kifo yalikuwa.

- MWISHO - 

Somo limeandaliwa na:
Mwl. James Kalekwa
0714 762669/0754 917764