Advertise Here

Tuesday, September 24, 2013

Safu ya James Kalekwa: Umejenga Juu ya Mwamba au Mchanga?



James Kalekwa

Utangulizi wa somo:

Mathayo 7:24-27
“Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, afuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

Kwa muda mrefu nimekuwa nikizunguka sehemu mbalimbali, makanisani na mikusanyiko, nikifundisha na kuwezesha semina, makongamano ndani ya nchi ya Tanzania. Moja ya msisitizo wangu ni kwamba wokovu si dini, wokovu si tamaduni au mapokeo (tradition).

Hii ni baada ya uchunguzi wangu wa kina na mapito kwenye maisha yangu binafsi ambapo niligundua ya kwamba kuna uelewa tofauti sana miongoni mwa watu juu ya wokovu (hata miongoni mwa watu waliookoka). Uelewa wako juu ya jambo fulani, ndiyo huamua kiwango cha maisha yako juu ya jambo hilo… Kama una uelewa mdogo, uelewa potofu, uelewa finyu… Ndivyo kiwango cha maisha yako kitakavyokuwa… “Your attitude determines your altitude.”

Kama unataka kutambua uelewa wa mtu binafsi kuhusu wokovu, tazama maisha yake ndani ya wokovu au sikiliza msimamo wake kuhusiana na wokovu… Ukikuta ni maisha ya dini, mapokeo/tamaduni… Basi tambua huo ndiyo uelewa wake. Kama asemavyo mfalme Sulemani “Maana aonavyo mtu nafsini mwake, ndivyo alivyo.”

Pia, kuna watu ambao bado hawajaokoka na hawataki kuokoka kwasababu bado hawajapewa taarifa sahihi kuhusu wokovu. Hii inamaanisha ya kwamba uelewa wao juu ya wokovu, umeyaathiri maisha yao. Laiti kama angetokea mtu wa kuwasikilizisha habari njema, basi uelewa wao ungebadilika na kisha wangeuelekea wokovu – Mungu atusaidie tuwasikilizishe wengine taarifa sahihi kuhusu wokovu.

Naamini unaelewa kuna taasisi au makusanyiko ya watu ambao wanajitahidi kujimilikisha wokovu kuwa ni mali yao binafsi yaani kama wewe si mshiriki au mmoja wa wanachama wao basi ni dhahiri kwamba wewe hujaokoka – hujapata wokovu! Wao huamini hakuna mtu mwingine aliyeokoka isipokuwa aliye ndani ya taasisi au makusanyiko yao…  Pia upande wa pili vivyo hivyo kuna wale ambao wamekuwa na juhudi nyingi sana kuukataa wokovu… kwa wao wokovu si dini yao, wokovu si utamaduni wao...

Kwa mtazamo wao, kuokoka ni kujifuta ushirika katika taasisi au makusanyiko yao. Pande zote hizi mbili, wanaoumiliki na wanaoukataa wokovu, wote wapo katika tatizo moja: tatizo la uelewa juu ya wokovu!

Ni heshima kubwa sana mbele za Mungu na mbele zako kwamba ninakukaribisha kujifunza ili kuulekeza uelewa wako juu wokovu. Karibu na uwajulishe na wengine juu ya mafundisho haya! Karibu na Mungu wa amani, Yesu Krsito aliye asili ya wokovu, akufungue macho yako ya ndani upate kuelewa mafundisho haya. 

Tujenge uelewa wa pamoja
 Naomba nikurejeshe kwenye andiko nililoanza nalo hapo awali:

Mathayo 7:24-27
“Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, afuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

Ili kuweza kutembea pamoja katika mfululizo wa mafundisho haya, ni vyema tukajenga uelewa wa pamoja juu ya andiko hilo amabalo ndilo msingi wa mafundisho haya. Bwana Yesu Kristo anazungumza juu ya wajenzi wa aina mbili, mjenzi mwenye busara na mjenzi mpumbavu. Ukitazama kwa umakini kwenye maandiko hayo utagundua ya kwamba maisha ya wajenzi hawa waiwili twaweza kuyafupisha hivi:



Mambo waliyofanana
Mambo waliyotofautiana

Mwenye akili
Mtu mpumbavu
1.        Wote walifanya shughuli ya ujenzi wa nyumba
*      Alijenga nyumba juu ya Imwamba
*I      Alijenga nyumba kwenye mchanga
2.       Wote walipata misukosuko inayofanana kwenye nyumba zao.
*      Nyumba yake haikuanguka
*      Nyumba yake ilianguka
 
Kilichoamua tofauti ya hawa ndugu ni kitu kimoja tu, nacho ni mahali walipochagua kujenga nyumba zao- mmoja alijenga kwenye mwamba na mwingine alijenga kwenye mchanga. Biblia imekaa kimya juu ya viwango vya ubora vya nyumba hizi, lakini imetueleza kwamba japo zilipitia misukosuko inayofanana lakini nyumba moja ilianguka na nyingike ilidumu (haikuanguka)…

Kwanini nyumba moja ianguke na nyingine isianguke wakati zote ni nyumba na zimepitia hali zinazofanana? Jibu ni rahisi sana, tofauti imeamuliwa na mahali nyumba zilipojengwa: kwenye mwamba na kwenye mchanga.

Naomba usisahau kwamba Bwana Yesu alitumia wajenzi kama mfano tu kuelezea dhana tofauti kabisa… Lengo lake lilikuwa ni ili kwamba watu waweze kujenga taswira (mental picture) ya anachokizungumza. Pia, ni hekima kama tukiirejea dhana ya Bwana Yesu huku tukiwa na taswira ya ndugu wajenzi ndani ya mawazo yetu.

Yesu anasema “mtu asikiaye maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa…” kisha anasema, “Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa…” Kwahiyo basi, dhana iliyo ndani ya moyo wa Bwana Yesu ni: kusikia maneno na kuyachukulia hatua (kuyatenda au kutoyatenda). 

Nitamanicho kiumbe ndani ya moyo wako na maisha yako ni kwamba ni wajibu wako kusikia neno na kulitenda kwasababu ni kwa njia hiyo tu ndiyo utafanana na mtu aliyejenga juu ya mwamba.

Kwakuwa sasa tumejenga uelewa wa pamoja, naomba uniruhusu nikuchukue kwenye mambo ya msingi (ambayo ni mwamba) yatakayokusaidia kuukulia wokovu… Kumbuka tunajenga wokovu wetu kwenye neno la Mungu na si mitazamo ya kidini, mapokeo au mifumo ya kimazoea. Ninaamini Mungu ana jambo kwaajili yako unapoendelea kufuatilia maswala haya ya msingi!

Somo litaendelea Jumatatu Ijayo....

Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu, na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764
jameskalekwa@gmail.com