Advertise Here

Thursday, September 12, 2013

KKKT yalalamikiwa kupora shamba.

KANISA la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT) Dayosisi ya mkoani Arusha, linatuhumiwa kuhusika na uvamizi wa shamba la muumini wake na kudaiwa kuliendeleza.  Muumini huyo, Willygasper Mrema wa Usharika wa Kimandolu, anadai kuwa shamba hilo ni mali yake aliyoirithi kutoka kwa wazazi wake.

“Hii ni mali ya wazazi wangu, nashangaa kanisa wamevamia shamba langu na sasa njia imefungwa na nimeshindwa kuliendeleza,” alidai Mrema.


Akifafanua kuhusu shamba hilo, Mrema alidai kufikisha taarifa katika idara zinazohusika na kisha kufungua kesi Baraza la Nyumba ambapo alidai shauri liliamuliwa kwa yeye kupewa haki yake.


“Baraza liliamuru nipewe haki yangu ya umiliki, lakini kanisa wamegoma kupisha ili niliendeleze eneo langu,” alidai Mrema na kuongeza:


“Nashangaa kanisa wameng’ang’ania shamba wakati wanatambua mmiliki wake ni mimi Mrema,” alisema.


Alisema kuwapo kwa mgogoro huo uliodumu kwa miaka mitano kumemfanya ashindwe kuliendeleza kwa kulima mazao mbalimbali, ili kujiingizia kipato na familia yake.


Kwa upande wake, Kaimu Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mkoani Arusha, Mchungaji Simon Massangwa, alikanusha madai ya Kanisa kuvamia shamba hilo.


“Kanisa halijawahi kuvamia wala halina mpango huo, kanisa linafahamu taratibu za umiliki wa maeneo, kamwe haliwezi kuvamia kama inavyodaiwa na muumini huyo,” alisema Kaimu Askofu Missangwa.


Akitoa ufafanuzi wa mgogoro huo, alisema, makubaliano yaliyopo juu ya eneo hilo yalifanywa kati ya Mfinanga na Simba kwa lengo la kubadilishana shamba hilo linalopakana na shamba na Mrema, ambapo wahusika walipewa shamba upande mwingine.


“Kimsingi Mrema si sehemu ya wamiliki wa shamba, bali ni miongoni mwa waumini wa KKKT, tupo tayari kukaa naye kama muumini ili kutafuta ufumbuzi wa madai yake,” alisema.

- Mtanzania -