Advertise Here

Monday, September 9, 2013

Safu ya James Kalekwa: Mambo yakupasayo Kujua Juu ya Maamuzi - Part II.


Mwl. James Kalekwa
Somo linaendelea.....

Kusoma Sehemu ya Kwanza Bofya Hapa

Mihula Mitatu ya Maisha ya Mwanadamu

Nimechagua kuiwasilisha mihula mitatu kwa kutumia taswira hii ifuatayo ambayo tutakuwa tukiirejea kila mara kwa kadiri tunavyoendelea kujifunza juu ya dhana ya kufanya maamuzi hasa kwa mwanga wa maneno ya Mungu kwa kinywa cha Nabii Yoeli.
 Kwenye Hatua ya Pili: Baada ya Kuzaliwa mpaka Kifo, hapo ndo kwenye BONDE LA KUKATA MANENO.

Maisha kabla ya kuzaliwa

Luka 1:30-33
Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Atamiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.”

Mathayo 1:21
“Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”
Ni jambo gani linakuijia mawazoni usomapo mistari hiyo?... Hata mimi kwa muda nilikuwa ninaona mafundisho ya Krsimasi kila nisomapo mpaka nilipofunuliwa jambo hili kwa namna ya tofauti. Hawa watakatifu wawili, waandishi wa Injili, wanaleta picha ya namna ya kipeke sana katika habari ya kuzaliwa kwa Yesu.

Hebu wacha nikuonyeshe kitu hapa… Kama umesoma vizuri na kwa umakini katika mistari hiyo utagundua ya kwamba imeandikwa kabla Yesu Kristo hajazaliwa. Mtakatifu Luka ameandika habari kabla hata ya mimba ndani ya Mariamu; na Mathayo ametueleza habari hiyo wakati wa mimba – lakini yote kwa yote ni kabla ya kuzaliwa kwa Yesu. Kitu gani unaona? Malaika anazungumza na Mariamu na kutaja jinsi ya mtoto kuwa atakuwa mwanaume, anataja jina la mtoto kwamba ataitwa Yesu na anataja baadhi ya majukumu yake baada ya kuzaliwa, yaani wakati wa kuishi kwake.

Hebu tazama kitu anachotuonyesha Mathayo, malaika anamtokea Yusufu ndotoni na kumpa habari kwa upana wake na katika habari hizo malaika anataja jina la mtoto na anataja kusudi la kuja kwake ulimwenguni. Yote hayo yanatajwa kabla ya mtoto kuzaliwa, yaani kabla hajaanza kuishi na kutembea ulimwenguni tayari ameshajulikana kwa namna kubwa sana, taarifa zake zinajulikana, jina lake, jinsi yake na kusudi la kuwepo kwake linajulikana.
Wengi hudhani kwakuwa ni Yesu, mwana wa Mungu, hivyo kwake ilipaswa kuwa dhahiri- ilikuwa ni ya kipekee (special case). Kabla hujahitimisha hivyo ni vyema ukumbuke kuwa Yesu alikuwa mwanadamu asilimia mia moja na Mungu asilimia mia moja, kwahiyo tunapozungumzia sehemu yake ya uanadamu ni vyema tukatazama kwa jicho hilo tu… Si unajua kuzaliwa ni sehemu ya uanadamu?

Naomba uambatane na mimi katika kutanua wigo wa uelewa kwa kuyasoma maisha ya watu wengine katika neno la Mungu kisha Tujifunze jambo kwa pamoja.

Yeremia 1:6
Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.”

Waamuzi 13:5
kwani tazama, Utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.”

Katika andiko la awali utagundua ya kwamba Mungu anazungumza na Yeremia akiwa tayari anaishi, amekwisha kuzaliwa tayari, na anamweleza kabla ya kutungwa mimba Yeremia alikuwa anajulikana kwa Mungu tayari. Ndiyo kusema japo Mungu hakuwaeleza wazazi wa Yeremia au kujifunua kwa mtu yeyote kueleza kuhusu Yeremia hiyo haiubadalishi mstari wa sita wa sura ya kwanza kwamba Yeremia alijulikana na Mungu. Kama Mungu alimjua Yeremia uwe na uhakika alimjua jinsi na kusudi la kuwepo kwake duniani…

Kwahiyo wakati mimba inatungwa, Mungu hakuwa anaona mimba, bali alikuwa anaona nabii wa mataifa. Kabla wazazi wa Yeremia hawajakutana, Mungu bado alikuwa anaona nabii wa mataifa. Si kwamba Mungu alianza kumjua Yeremia  baada ya wazazi wake kukutana, bali Mungu aliwakutanisha wazazi wake Yeremia ili wapate fursa ya kumfahamu Yeremia.

Kwenye andiko linalofuatia ni ujumbe wa malaika kwa familia ya wanandoa ambao bado walikuwa hawajawahi kupata mtoto maishani mwao. Malaika anamtokea mama mtarajiwa, ambaye wakati huo alikuwa ni mwanamke tasa, na anaanza kumpa habari za mtoto wake wa kiume na anaenda hatua ya mbele zaidi kwa kumweleza kusudi la kuja kwa mwanaume huyo ulimwenguni na namna gani anapaswa kulelewa…

Hii inaweza kuonekana ni habari ya kiuendawazimu kidogo, kutoa habari kamili juu ya mtoto fulani kwa mwanamke tasa!!! Malaika anatoa wapi ujasiri wa namna hiyo? Amepewa hizo taarifa na Mungu, kwahiyo malaika hakuwa anabahatisha au anajaribu kutoa utabiri bali alikuwa anazungumza ukweli, yaani ndivyo ilivyo. Huyu mtoto wa kiume alikuwa anajulikana kwa Mungu kwahiyo ilikuwa ni habari sahihi kutoka chanzo sahihi cha habari.

Kwa mwanga wa uelewa huo nilioweka msingi ndani yako naomba ujiulize je, unadhani kuzaliwa kwako duniani kumemshitukiza Mungu? Je, Mungu ameshangazwa na uwepo wako (Is God caught by surprise by your existence?) yaani namaanisha unadhani Mungu amesema “Oooh!!! Kumbe huyu aliyezaliwa ni James?” au “Ahaa!!!

Kumbe leo amezaliwa Sowane?” siku ambapo mimi nilizaliwa au siku ambapo ndugu Sowane alizaliwa?. Hapana, Yahwe si Mungu mdogo kiasi hicho eti kwamba kuna matukio yanamshangaza au kumshitukiza! Angekuwa hivyo, basi asingeweza kuuongoza ulimwengu. Katika lugha ya elimu ya theolojia, Mungu hutambulishwa kama “omniscient” yaani mwenye ufahamu yote- anayejua mambo yote!

Natambulisha ufahamu huu ya kwamba kabla ya kuwepo ulikuwepo na ulijulikana kwa Mungu! Ulikuwa ndani ya mawazo na fikra za Mungu kabla hujatokea duniani. Ulifahamika jinsi na kusudi la kuwepo kwako kabla hujadhihirika katika ulimwengu wa mwili.

Lakini ni muhimu sana ukarejea mistari hiyo juu na kuona ya kwamba aliyekuwa ni chanzo cha taarifa za kuzaliwa, kuishi, kusudi la wanadamu hao alikuwa ni Mungu na hakuna mwingine- hata malaika!

Hiyo ni udhihirisho ya kwamba aliyefanya maamuzi ya jinsi, nyakati na kusudi la kuzaliwa ni Mungu pekee. Ni dhahiri ya kwamba ukiambiwa ufikiri ulikuwaje kabla ya kuzaliwa, picha itakayo kuijia mawazoni mwako ni giza tu! Hukuwa na ufahamu na uelewa na hukuwa na maamuzi ya kuzaliwa kwako.

Binafsi, sikuamua kuzaliwa mtanzania, lakini ile kujua kwamba nimezaliwa kuwa mtanzania ni furaha sana ndani ya moyo wangu kwasababu ni udhihirisho kwamba aliyeniweka amekusudia kitu kwa nchi ya Tanzania kupitia mimi na ndiyo maana akaniweka. Ile kwamba mimi ni mwanaume ninatambua si kwa bahati nzuri au mbaya bali ni kwa kusudi… Nilijulikana kwa Mungu lakini sikuwa na uwezo na nafasi ya kufanya maamuzi yoyote na hivyo siwajibiki na maamuzi ya kuzaliwa na kuwepo kwangu.

Hakuna mtu anaweza kunihoji kwanini nilizaliwa mtanzania na si mtu wa taifa jingine, sipaswi kupongezwa au kulaumiwa kwa kuzaliwa mwanaume, wala siwajibiki kwa kuzaliwa na kuishi kwangu katika zama hizi. Kwani kuna mtoto unaweza kumpa hongera au kinyume chake kwa kuzaliwa kipindi cha siasa za vyama vingi hapa Tanzania? Unadhani kuna mzee wetu yeyote anayestahili kuadhibiwa kwa kuzaliwa kipindi cha mapambano ya uhuru?

Hapana!!! Kwasababu hakuna kati yetu aliyeshiriki kufanya maamuzi hayo lakini hiyo haiubadili ukweli kwamba sote tulijulikana kwa Mungu kabla ya kuzaliwa kwetu.

Somo litaendelea jumatatu Ijayo.....

Somo limeandaliwa na:
Mwl. James Kalekwa
0714 762669/0754 917764