JAMBO LA NANE
Je! Uko tayari kuolewa na nani?
Wengine hawafikirii namna hiyo, ukiwauliza uko tayari kuolewa na
nani, anasema na mtu aliyeokoka. Bwana anawajua walio wake, hakuna mtu
kwa jinsi ya nje atakayemjua mtu aliyeokoka kisawasawa hasa alivyo
kitabia. Maana watu wengi sana wanasema wameokoka lakini hawajaokoka,
wengine wanasema ‘bwana asifiwe’ lakini ni bwana mwingine sio Bwana
Yesu! Ni mambo ambayo unatakiwa kufikiri, unataka kuolewa na nani.
Labda hujawahi kufikiria kitu cha namna hiyo, nataka nikufikirishe
vitu vya kawaida kabisa. Wengine wanasema mimi nataka kuolewa na
mtumishi, hesabu gharama kwanza! Wengine wanaona tunavyoshirikiana na
mke wangu katika huduma wanamtazama wanasema, wanataka kuolewa na
mtumishi; kaamuulize mke wangu, tulipokutana hata wito haukuweko, na
tulikutana wote hatujaokoka. Tulikuja kuokoka baada ya kuoana!
Mungu ametuteremshia utumishi tuko kwenye ndoa tayari, kwa hiyo
usitamani ndoa ya kwetu, tamani ya kwako ambayo Mungu amekupangia. Mke
wangu hakunipendea utumishi, sikuwa na tone la utumishi, wala hata ya
kufanania ya kwamba nitaokoka, na yeye alikuwa hajaokoka pia wakati
huo. Lakini kwa saa na kwa makusudi na kwa utaratibu wa Mungu, tumekuwa
jinsi tulivyo. Akatuteremshia utumishi wakati tumekwishaokoka na
tumekwishaoana!
Usijaribu kufananisha ndoa yako na ndoa ya mtu mwingine, hujui iliko
toka, tamani ya kwako. Sasa unasema wewe unataka mtumishi, lakini
watumishi wako wengi sana, kwa hiyo unataka mtumishi wa namna gani?
Lazima ufikiri juu ya hili pia. Unasema mimi ninataka mhubiri, hata
nabii ni mhubiri, mwinjilisti ni muhubiri, mwalimu anaweza akahubiri.
Kitabia hawafanani, haleluya! Nataka nikufikirishe ikusaidie, maana
nataka nikujengee msingi mzuri wa maisha ambao ukikanyaga vizuri shetani
alie tu, maana hatawezi kukuvuruga.
Maana watu wengi wanapata shida sana wanapotaka kuoa au kuolewa,
utakuta wanasema, mimi ninataka kuoa au kuolewa na mtumishi, hayo ni
maombi ya mtu ambaye hajaenda shule ya Roho Mtakatitu, bado yuko
chekechea, unajua lazima uwe ‘very specific’. Mungu anataka useme naye
kile kitu unachokisikia ndani yako. Anajua kabisa kitu ambacho ni kizuri
kwa ajili yako; lakini Mungu hataki kukulazimishia tu, anataka
ushirikiane naye, ili akikupa kitu ukipokee kwa furaha.
Kwa hiyo kama unataka mtumishi, ni muhimu useme unataka mtumishi wa
aina gani. Kwa mfano ukisema nataka mwinjilisti, hesabu gharama, lazima
uwe na neema ya kukaa na mwinjilisti. Si unajua mwinjilisti hakai
nyumbani, anazunguka, akikosa watu wa kuwachapa injili huko nje, anakuja
kuchapa injili nyumbani hata kama mmeokoka wote! Na ujue hawezi
kumaliza ibada ya jioni mpaka awepo mtu wa kutubu, hajatubu ataendelea
kufanya maombi. Kama hauko tayari kuchukuliana na mtu wa namna hiyo
usiamue kuoa au kuolewa naye.
Lazima useme; au kama unataka kuolewa na nabii jipange, kwa sababu
hajui kuongea na watu, muda wake mwingi yuko kimya, manabii mara nyingi
wanafungwa midomo sio wasemaji ni mtu mkimya. Mara nyingi amejifungia
kuomba peke yake na Mungu.
Hata saa nyingine unatamani uombe pamoja
naye, lakini Mungu anataka yeye peke yake. Wewe nenda kwenye biblia
utaona maisha yake yalivyo kila kitu kinachomzunguka, kila kitu
anachovaa, kila kitu anachokutana nacho, Mungu anaweza akakigeuza
ujumbe.
Kwa hiyo usije ukashangaa kesho akakutazama na akaishia kupata
mahubiri toka kwako, halafu mkirudi nyumbani mnaanza kugombana, na
unamuuliza sasa wewe ulikuwa unanihubirije? Kwani wewe hukujua ya
kwamba ni nabii na anaweza kupata ujumbe unaosema: “kama vile mke wako
alivyovaa, ndivyo na kanisa langu lilivyo asema, Bwana”!
Wewe usifanye mchezo! Sasa nyingine mnaishiwa chakula na anaona jinsi
mnavyohangaika, basi utakuta amekwishapata ujumbe kama huu, “kama vile
mke wako alivyokuwa anahangaika kutafuta chakula kwa ajili ya watoto,
ndivyo na mimi ninavyotafuta chakula kwa ajili ya watoto wangu, asema
Bwana”!
Saa nyingine unavaa nguo zinapasuliwa, mpaka viungo vya ndani
vinaonekana, ujumbe unatoka saa hiyo mara moja, anasema, “Kama vile mke
wako alivyovaa nguo iliyopasuliwa na watu wanaona ndani, ndivyo na
kanisa langu lilivyo vazi lake limepasuliwa na shetani anaona ndani”!
Lazima uwe tayari kuwa ujumbe, kama unataka kuolewa na nabii. Uwe
tayari kuwa ujumbe, hujawa tayari usiombe uolewe na nabii! Unataka
kuolewa na mchungaji uwe na moyo mkubwa wa kupokea wageni. Mwingine
anasema mimi ninataka kuolewa na mtumishi lakini ndani yake anawaza mtu
anayezunguka na kuhubiri, kumbe Mungu ameweka ndani yake mtumishi,
lakini ni mfanya biashara.
Mfanya biashara mwingine anapakwa mafuta kufanya biashara, ndio
sehemu yake kumtumikia Mungu, mwingine ni fundi cherehani, mwingine ni
dereva, wanapakwa mafuta sehemu zao hizo za utumishi, usije ukafikiri
hao wanaoafanya kazi nyingine sio watumishi wa Mungu. Mungu anawapaka
mafuta kwa ajili ya hizo kazi, ili walitumikie kusudi lake.
Kwa hiyo unapokwenda katika maombi unasema tu mimi ninaomba mtumishi,
Mungu atakuletea mtumishi yoyote, wako wengi, wengine wanafagia
barabara, ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha kule kwenye vyoo
vya kulipia ni watumishi wa Mungu, wengine wanasafisha nyumba za watu,
nao ni watumishi wa Mungu,oh haleluya!
Mungu akikuletea mtumishi yeyote unaishia kusema, mimi sikuomba huyu
niliomba mtumishi. Mungu atakuambia huyu ni mtumishi wangu, usimnenee
kitu cha namna hiyo.
Kama msichana ni mfupi usitamani kijana mrefu, au kijana ni mrefu
unatamani msichana mfupi. Kwa kweli, sio kwamba Mungu hawezi kukupa,
lakini wewe fikiri tu mwenyewe, haleluya! Maana mwingine anakuwa mfupi
kiasi ambacho anafanana kama vile ni mtoto kwako, wenzako wanakuuliza
tangu lini umepata mtoto na akakua na akawa mkubwa namna hii, unasema
“ninyi msiseme hivyo, ni mume wangu huyu”.
Ni uamuzi wako. Sasa, si lazima mfanane urefu, lakini msipishane sana; kwa kweli ni kwa faida yenu wenyewe, haleluya!
Kama msichana hupendi mwanaume mwenye ndevu, omba vizuri. Maana
unaweza ukapata mtumishi wa Mungu, lakini ana ndevu na wewe huzitaki.
Ikifika siku umeingia tu kwenye ndoa kitu cha kwanza unamtafutia wembe
ili anyoe ndevu zake – hii ni kumwonea! Ulimpenda akiwa na ndevu, kumbe
wewe ulikuwa unamtegea tu ili baada ya arusi tu umpe wembe! Wako
wasichana wanaopenda wanaume wenye ndevu, waachie hao!
Huyu Bwana Mungu wetu ni mzuri sana, unajua, saa nyingine huwa
ninawaza jinsi Mungu alivyomuumba mwanadamu na nabaki ninashangaa sana.
Maana kuna wanaume wengine hata ndevu hawana, hata wakilazimishia kunyoa
kidevu kitupu haziji. Sasa mtu mwingine anajisikia vibaya, akifikiri
ya kuwa mtu anaonekana ya kwamba yeye ni mwanaume kwa sababu tu ana
ndevu, si kweli. Kuna wanaume wengine wametengenezwa namna hiyo
‘special’ kwa ajili ya wasichana wasiotaka wanaume wenye ndevu,
haleluya!
Maana mwingine anaweza akaachia ndevu zikafunika mpaka karibu na
kwenye pua. Sasa kama ni mtu mweusi sana ‘ni hatari sana’, giza
likiingia tu ndani ya nyumba wewe unamwambia ‘cheka’, akicheka yale meno
yake yanaweza yakamulika kidogo, na utajua yuko wapi! Hivi vitu
ukishaingia kwenye ndoa ni vitu vikubwa sana, kuliko watu
wanapoviangalia kabla hawajaoana.
Wewe unakuta kijana anaoa msichana ana rangi nyeusi nzuri tu, akifika
ndani unamletea madawa ajikoboe, wewe ulikuwa unamwoa wa nini? Hiyo
sasa ni sawa na kumwambia Mungu kwa kweli nimechukua tu huyu, lakini sio
niliyekuwa namtaka!
Niliyekuwa namtaka ni mweupe, sasa maandamu umenipa huyu wacha
nimkoboe mpaka afike rangi ninayotaka, – haviendi namna hiyo bwana!
Mungu alipokuwa anamuumba huyo msichana namna hiyo aliona, alimtazama
alivyo na weusi wake huo akaona kila kitu chema, akajipa sifa, akajipa
maksi asilimia mia moja, amefanya kitu chema!
Sasa akitaka kupaka rangi hiyo ‘nyumba yake’ na kuinakshi ni kitu
kingine. Unajua kuna nyumba nyingine hazipendezi mpaka uzipake rangi
fulani, haleluya! Mwili ni nyumba, kuna wengine hawawezi kupendeza mpaka
wamepaka rangi fulani kwenye miili yao. Sasa utapata mtihani mgumu,
nimeona, kijana anampenda msichana, lakini msichana anaweka rangi kwenye
midomo yake, kucha zake anaweka rangi, anachora na kalamu hapa kwenye
nyusi kidogo, ukimtazama vizuri usoni utagundua ya kwamba ameweka kitu
kingine juu ya uso wake.
Umempenda akiwa namna hiyo. Wakati ulipokuwa unamfuatilia hukumuuliza
hayo maswali, leo ameingia ndani umemuoa, unamwambia sitaki hizo rangi!
Hiyo ni kumwonea, maana ulimkuta akiwa hivyo, kama ulikuwa humtaki
akiwa amejinakshi na rangi hizo, hukutakiwa kumfuatilia, wako wengine
ambao watakuwa radhi na huyo anayejipaka rangi!
Kuna kijana alioa msichana, wamefika ndani wakaanza kugombana naye
habari za nywele, mpaka akamrudisha kwao, – nywele tu! Huyu dada kaenda
katengeneza nywele staili fulani, yule kijana haitaki. Lakini alimkuta
yule msichana anatengeneza nywele kwa staili hiyo, sasa kwa nini hivi
vitu hawakutaka kuzungumza kabla ya kuamua kuoana?
Mimi ninataka nikusaidie upunguze ugomvi ndani ya ndoa utakayokuwa
nayo; maana vitu ambavyo Mungu atawaletea vya kufanya pamoja kwenye ndoa
ni vikubwa kuliko mnavyofikiri, kiasi ambacho hamhitaji kutumia muda
wenu kushindania vitu vidogo vidogo ambavyo mlikuwa muwe mmekwisha
kuvijadili kabla ya kuoana. Mna mambo muhimu sana ya kufanya, kiasi
ambacho kuanza kushindana na kubishana juu ya vitu ambavyo mlitakiwa
muwe mumeshavizungumza kabla ya kuoana; huko ni kutokuelewa utaratibu wa
Mungu ulivyo juu ya kumpata mwenzi wa maisha.
MWISHO!