KANISA la Moravian Tanzania, Jimbo la Misheni Mashariki
limemsimamisha kazi mchungaji wake, Clement Fumbo baada ya kubainika
kwenda kinyume na taratibu za kanisa hilo.
Fumbo alikuwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Jimbo la Mashariki na Zanzibar.
Akizungumza
Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu wa jimbo hilo, Mchungaji Adolf
Mwakanyamale alisema wamefikia hatua ya kumsimamisha kazi Mchungaji
Fumbo, kwa sababu alikuwa anakiuka taratibu za kanisa.
Pia, anadaiwa alikuwa akiidhinisha hundi tupu bila ya kuwapo kwa wajumbe wala kufahamishwa.
Mchungaji
Mwakanyamale alisema kanisa hilo limefikia uamuzi huo baada ya kikao
cha dharura kilichofanyika Oktoba 6,mwaka huu Ushirika wa Moravian,
mkoani Morogoro.
Alisema sababu nyingine iliyochangia
mwenyekiti huyo kusimamishwa kazi, ni kukosekana kwa ushirikano mzuri
katika utekelezaji majukumu ya kanisa kati yake na wajumbe wengine wa
kamati ya utendaji.
Pamoja na kukosekana kwa
ushirikiano mzuri katika utekelezaji wa majukumu ya kanisa, anadaiwa
amekuwa akipinga baadhi ya uamuzi unaotolewa na kuubadili atakavyo na
kudharau maazimio halali yaliyotolewa kwenye mkutano mkuu.
Pia,
Mchungaji Mwakanyamale alisema Mchungaji Fumbo alishindwa kusimamia
vyema Katiba ya kanisa na kanuni zake katika mwenendo wa fedha na mali
za kanisa.
“Mchungaji Fumbo amesimamishwa kazi yake ya
mwenyekiti baada ya kanisa kubaini kuwa, matumizi mabaya ya mali za
kanisa mfano kuchukua vyerehani vya kanisa vilivyokuwa Ukonga na
kuvipeleka mahali pasipojulikana ikiwamo kusaini hundi tupu bila kuwapo
wajumbe wa kanisa au halmashauri kuu,” alisema Mchungaji Mwakanyamale na
kuongeza:
“Kanisa pia liligundua kuwa mwenyekiti
huyu alikuwa na dharau kwa viongozi wenzake wa kamati tendaji na
anawadhalilisha kwa watumishi na wachungaji wengine, pamoja na kwenda
kinyume na matakwa ya kanuni na katiba ya kanisa.”
Anadaiwa
kuvunja agizo la Sinodi la kuendelea na ujenzi wa Makao Makuu ya Kanisa
la Chamazi na kuanza mchakato wa ujenzi wa makao makuu kuwa Tabata.
Gazeti la Mwananchi
Gazeti la Mwananchi