JAMBO LA TATU
Ukiamua kuoa au kuolewa, wakati mwingine
imani yako inaweza ikabadilika.
Wasomaji wa biblia wanamfahamu mtu mmoja aliyeitwa mfalme Sulemani (unafahamu ni kwa nini aliandika kitabu cha Mhubiri, maana alipoandika kitabu cha Mhubiri akasema, mambo yote chini ya jua ni ubatili mtupu). Biblia inatuambia wazi kabisa ya kuwa Mungu alimpa hekima ya ajabu, na wasichana wakatoka sehemu mbali mbali duniani kwenda kufuatilia ile hekima, walipoikuta hawakutaka kuondoka na wakabaki pale kwake.
Kosa alilofanya Sulemani ni kwamba wale wasichana walikuwa wanakuja na miungu yao, na alikuwa anawakaribisha wale wasichana na miungu yao, anawapa na mahali pa kujengea vibanda vya miungu yao. Biblia inatuambia wazi kabisa, ilifika mahali wale wakina mama wakamgeuza moyo wake usiendelee kumpenda Bwana.
Kitabu cha 1 Wafalme 11:4 kinasema hivi: “Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.”
Nimeona vijana wengi sana ambao wanakuwa moto sana kwenye wokovu kabla hawajaolewa au kuoa, wewe ngoja waingie kwenye ndoa na wafuatilie baada ya muda, utakuta wengine wamepoa mpaka wameganda kama barafu! Ukiwauliza ni nini kimewafanya wapoe kiroho kwa kiwango hicho – wanaweza wakashindwa kusema. Maana kuna watu wengine wanafikiri ni kuolewa tu na mtu yoyote kwa sababu tu anasema Bwana asifiwe, ibilisi Pia huwa anaweka na watu wa kwake huko ndani ya makundi ya watu waliookoka.
Na ukikaa na vijana utapata baadhi yao wanaosema, ukitaka kupata vijana waaminifu siku hizi nenda katikati ya waliokoka, kwa hiyo wanajifanya wameokoka. Akikufuatilia juu ya kuoana na ukimwambia mbona wewe hujaokoka, na ukamtaka kwanza aokoke ndipo mzungumze, utakuta baada ya siku chache kupita anajifanya ameokoka, lakini ni yakubabaisha tu ili akupate. Nimekutana na watu wa namna hiyo, msichana anaolewa akishafika ndani, ndio kijana anamwambia, na Yesu wako na wokovu wako nauvua hapa hapa, mimi nilikuwa nakutafuta wewe, nimekupata basi!
Nimeona! Sisemi kitu cha hadithi, ninasema kitu ambacho nimeona kwa macho. Ikiwa umefika katika hali hii basi, ni mpaka kifo kiwatenganishe, na alikwishawaambia wenzake kwamba Mungu amenifunulia; kwa hiyo hana ujasiri wa kurudi na kusema kweli nilikuwa nimekosea, yalikuwa ni mafuniko sio mafunuo! Akitaka kwenda kwenye maombi anaambiwa hakuna; akitaka kwenda kuhudumu anaambiwa hakuna; anataka kwenda ‘fellowship’, anaambiwa hakuna; kaa hapo ndani. Kwa hiyo inabaki kazi moja tu ya kuombea chakula na chai na kwenda kulala!
Na ni kwa sababu huyu mtu hakufikiri sawasawa, hakukaa akaona jinsi ambavyo hili jambo linaweza likambadilishia imani yake kabisa. Wewe nenda kwenye maandiko, utaona ya kuwa ndoa inaweza ikakubadilisha. Ndio maana kuna watu wengine wanaolewa, na wengine wanaoa na wanabadilisha dini, hii sio kitu cha mchezo, ni maamuzi magumu sana kuyafanya.
Unapobadilisha imani yako unabadilisha msingi wako kabisa wa maisha yako; kwa hiyo ni lazima uamue jambo ya kuoa au kuolewa kwa uangalifu sana.
Lakini pia inaweza ikawa ni mkristo kwa mkristo wanataka kuoana, lakini fahamu kuoa au kuolewa kunaweza kukakubadilisha dhehebu lako la kikristo, ndio maana lazima mkubaliane juu ya jambo hili kabla ya kuingia kwenye ndoa. Nilikuta vijana wamekubaliana kuoana, kijana mmoja mlutheri, kijana mwingine mpentekoste. Mambo yakawa magumu sana kwao, walipofika masuala ya kujadiliana, juu ya imani zao. Ilikuwa ngumu sana, mpaka wachungaji wao wakaingilia kati.
Walipokuja kuniona, nikawauliza mko tayari kabisa na mnataka kuoana? Wakasema, ndio. Wakati huo walipokuja kwangu walikuwa tayari wameshaenda nyumbani kwao, wameshazungumza na wazazi wao, na kote huko na wakati wote huo hawakufikiria hilo jambo. Sasa imefika mahali mchungaji wa kanisa hilo la pentekoste hakubali msichana wake aolewe kwa kijana wa kilutheri. Nikamuuliza maswali yule msichana akashindwa kujibu.
Unajua wapentekoste hawabatizi watoto, walutheri wanabatiza watoto. Mnapooana matokeo yake ni kwamba watoto watazaliwa. Ni lazima hicho kitu ufikiri kabla hajasema ndio kuolewa, au ndio kuoa. Sio umekwisha olewa ndipo unasema watoto wangu hawawezi kwenda huko, – ulikuwa wapi toka mapema ili uliseme hili tatizo? Maana unaweza ukafikiri ni masuala marahisi, sio masuala marahisi.
Maana wengine wanalichukulia jambo hili kirahisi, wakati jambo lenyewe sio rahisi. Masuala ya kwenda kusali kanisa tofauti tofauti huku mmeoana sio mambo rahisi. Nimeona watu wakisema hakuna tatizo maana tutaoana, lakini kila mtu wetu atakuwa anakwenda kanisani kivyake; sawa, ninyi mnaweza mkaenda kivyenu, na watoto je? Labda kama hamna mpango wa kuzaa!
Maana niliona kwenye TV, mtu mmoja, – dada mmoja huko ulaya amefuga mbwa akasema, tuliamua huku ndani tusizae watoto na badala yake tumefuga mbwa badala ya mtoto, wamempa na jina, wamempa na chumba wamempa na kitanda, anasahani yake, na bajeti yake, ana daktari, wameamua wasizae na badala yake, wamefuga mbwa! Labda kama unataka kuelekea njia hiyo! Lakini kama unaingia kwenye ndoa na unajua utakwenda kupata mtoto, suala la mahali mnapokwenda kusali ni muhimu sana kulijadili na kuliamua kabla ya kuingia kwenye ndoa.
Usiende kupeleka vita kwenye ndoa yako ambayo haitakiwi kuwepo! Unajua kuna vita vingine tunavianzisha bila sababu, hata Yesu alijua, wakati saa yake ya kupigwa mawe ilipokuwa haijafika, alikuwa anawakwepa wale watu waliokuwa wamepanga kumpiga mawe. Sasa kama Yesu alikuwa anakwepa majaribu mengine kwa nini wewe unajitumbukiza? Saa ikifika ya jaribu kuja kwako utalishinda tu, kwa sababu umetengenezwa na Mungu uwe na uhakika wa ushindi, kwa sababu ukiwa ndani ya Kristo unashinda na zaidi ya kushinda.
Imeandikwa hivi katika kitabu cha Warumi 8:37; “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda”. Lakini majaribu ya kujitafutia, yanaweza yakayumbisha imani yako.
Maana watu wengi sana huwa hawajiulizi hili swali mapema lakini nimeona likiwapa shida. Wengine hata imefika saa ya kufunga ndoa, ndio kwanza wanaanza kujiuliza, ‘ndoa sasa tunakwenda kufungia wapi’, hilo sio swali la kujiuliza saa hiyo, utakuwa umechelewa! Wewe ulikuwa unajua kabisa mwenzako anasali mahali fulani, na wewe unasali mahali pengine, imefika saa mnataka kufunga ndoa mnaanza kujiuliza, tukafunge ndoa kwenye kanisa la nani, ikiishafika hapo mnaanza kushindana na kuvutana; na haifai mambo kuwa hivyo.
Somo hili bado linaendelea. Usikose sehemu ya Nne ya somo hili Siku ya Jumapili.