KIJANA mmoja Dastani Sichivula(34) ambaye anajihusisha na vitendo vya uporaji katika mji wa Tunduma mkoani Mbeya, ameamua kumrejea Mungu kwa kutamka kanisani kuacha vitendo hivyo huku akidai kuwafichua wenzake aliokuwa akifanya nao uharifu.
Akizungumza katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God(TAG), Sichivula alisema kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo kufuatia kujiona ametengwa na jamii kutokana na kuhofia kuporwa jambo ambalo aliona anaweza kuuawa kama walivyouawa ndugu na rafiki zake aliokuwa akishirikiana nao.
“Nilianza vitendo vya uporaji mwaka 1993, katika wakati wote huo wapo jamaa zangu wengi ambao wamepoteza maisha kufuatia kupigwa na wananchi wenye hasira kali, pia nakumbuka tukio moja ambalo mdogo wangu alipigwa hadi kufa kufuatia kumpora mtu shilingi 10,000/= "
Aliongeza kwa kusema kuwa, “Katika kipindi chote hiki nimekuwa nikishuhudia watu ninaokutana nao njiani wakiniangalia kwa hofu, jambo ambalo lilinifanya nijisikie kutokubalika na jamii na hivyo nikikumbuka vifo vya wenzangu nilipata picha kuwa ipo siku nami nitauawa kama hao hivyo kuamua kuokoka na kuacha tabia hiyo ili niwe raia mwema.”
Aliongeza kwa kusema kuwa, “Katika kipindi chote hiki nimekuwa nikishuhudia watu ninaokutana nao njiani wakiniangalia kwa hofu, jambo ambalo lilinifanya nijisikie kutokubalika na jamii na hivyo nikikumbuka vifo vya wenzangu nilipata picha kuwa ipo siku nami nitauawa kama hao hivyo kuamua kuokoka na kuacha tabia hiyo ili niwe raia mwema.”
Aidha Kijana huyo alitumia nafasi hiyo kuomba msamaha kwa umma wa Watanzania na wanaTunduma wote ambao aliwahi kuwapora au kuwafanyia ubaya wowote kumsamehe na kumwombea kwa Mungu ili aendelee kuishi kama raia mwema.
Kwa upande wake Mchungaji kiongozi wa Kanisa hilo Paulo Mfwomi akihubiri katika siku hiyo aliwataka watanzania kumcha Mungu ili kuachana na vitendo viovu vya wizi ambao alisema upo wa aina nyingi na ambao unaleta machukizo mbele za Mungu na Taifa kwa ujumla.
Alifafanua kuwa wapo watu waliopewa dhamana ndani ya serikali ambao wamekuwa wakishiriki vitendo vya wizi kwa kutumia kalamu, wafanyabiashara huiba kwa kutoza bei kubwa ili kujipatia faida kubwa na kuwa vitendo hivyo vyote ni wizi na hivyo vinapaswa kuachwa.
Akizungumzia kujisalimisha kijana Dastan ambaye alikuwa tishio kwa jamii, mchungaji Mfwomi alimpongeza kwa uamuzi huo na kusema kuwa, baada ya kuokoka kwake hatakuwa na kazi basi kanisa litaangalia namna ya kufanya ili aweze kuendesha maisha yake.
Katika kuonesha kuunga mkono uamuzi wa Sichivula waumini waliohudhuria ibada hiyo walimchangia shilingi 72,000 ili aweze kuanzia maisha asifikirie tena kurudi katika matendo ya uporaji na unyang’anyi.