BABA Mtakatifu Francis, amekubali ombi la Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea, Norbert Mtega (68),pichani, kustaafu katika utume wa kuongoza jimbo hilo.
Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Anthony Makunde, kutoka kwa Balozi wa Papa nchini, Askofu Mkuu Frascisco Padilla, ilieleza kuwa, Papa amekubali ombi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ombi la Askofu Mtega kwa Papa, lilitokana na kuwa na matatizo ya kiafya, hivyo kushindwa kuwahudumia waumini inavyopaswa.
Hata hivyo, kikanisa ni siri ya mtu mwenye hadhi ya Askofu, anapoomba kwa Papa kustaafu.
“Baba Mtakatifu Francis amekubali ombi la Mhashamu Askofu Mkuu Norbert Mtega, kustaafu kutoka majukumu ya utawala wa kichungaji wa Jimbo Kuu la Songea, kwa sababu ya kiafya,” ilieleza taarifa hiyo.
Hata hivyo haikufafanuliwa maradhi yanayomsumbua Askofu Mtega, ambaye pia kiumri ni miongoni mwa maaskofu wakongwe katika kanisa hilo nchini.
Katika hatua nyingine, Papa amemteua Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, wa Iringa, kuwa msimamizi wa kitume wakati kiti cha Askofu wa Jimbo Kuu la Songea, kikiwa wazi, kwa mamlaka ya kiti kitakatifu (Mamlaka ya Vatican).
Kwa kawaida, hakuna muda maalum wa uteuzi wa Askofu Mkuu mwingine kuongoza jimbo, panapotokea askofu amestaafu utume, lakini huchukua hata miezi sita hadi mwaka kufanyika uteuzi. Hivi sasa jimbo hilo linaongozwa moja kwa moja kutoka Vatican kwa usimamizi wa Askofu Ngalalekumtwa.
Askofu Mkuu Mtega alizaliwa katika kijiji cha Kinyika (Lupanga-Njombe), Agosti 17, 1945. Alipata daraja la Upadri Novemba 14, 1973, aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Iringa Oktoba 28, 1985.
Aliwekwa wakfu na Papa John Paul II Januari 6, 1986, huko Roma II, na miezi miwilli baadae, Machi 9, 1986 alisimikwa Iringa. Aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Songea Julai 6, 1992 na kusimikwa huko Songea Septemba 20 mwaka huo huo.
Mwisho.