JAMBO LA SABA
Je! Uko tayari kuoa au kuolewa?
Je! Uko tayari kuoa au kuolewa?
Ni swali muhimu, uko tayari, maana yake umefika mahali hali yako ya
ndani na nje, inakuruhusu kuoa au kuolewa? Uko tayari kuoa au kuolewa?
Umefika mahali pa namna hiyo?. Wengine wanasema huyu ni mtoto, lakini
unajua pamoja na kwamba ni mtoto, ni vizuri kujua kama uko tayari
kiumri. Lakini ninapozungumzia hapa juu ya utayari wa kuoa au kuolewa,
sizungumzii tu habari za miaka, bali ninazungumzia habari za hali yako
ya ndani.
Nimeona kuna mtu mwingine ana miaka arobaini, lakini kwa kweli
hayuko tayari kukaa na mwanamke, ndani yake, mawazo yake na kufikiri
kwake, hayuko tayari kukaa na mwanamke, hawajibiki hata yeye mwenyewe
juu yake mwenyewe. Wengine hata wana miaka hamsini, lakini ana hali kama
hii. Nimeona akinadada hata wana miaka arobaini na tano, hayuko tayari
kuolewa, maana akiolewa ni shida tu.
Nilienda mahali fulani, nikakuta dada ana umri mkubwa tu, lakini
wakati wa maombi hakusema kama anataka tuombe ili aolewe. Nikaona ngoja
nimuulize labda anaona aibu kusema hitaji hili kwa sababu umri umesogea,
nikamwambia “hutaki tuombe uolewe”? Akasema, “hapana, sitaki kuolewa”
(Na alikuwa ana umri wa miaka kama arobaini na zaidi). Nikamuuliza, “kwa
nini”. Akasema, “kwa sababu sitaki kuomba ruhusa kwa mwanaume
ninapotaka kutumika”. Nikamuuliza unafanya kazi, akasema, “ndio”.
Nikamwambia, “unapokwenda kumtumikia Mungu huwa unafanyaje, – unaomba
ruhusa au unatoroka huko kazini?”
Akasema, “ninaomba ruhusa”. Nikwamwambia, “kwa nini unaona ni rahisi kuomba ruhusa kwa mwajiri wako na unaona taabu kuomba ruhusa kwa mume wako?” Alishindwa kujibu hilo swali.
Akasema, “ninaomba ruhusa”. Nikwamwambia, “kwa nini unaona ni rahisi kuomba ruhusa kwa mwajiri wako na unaona taabu kuomba ruhusa kwa mume wako?” Alishindwa kujibu hilo swali.
Nikamwambia tatizo lako ni kubwa kuliko unavyo fikiri.
Unaweza ukaona kabisa ya kwamba, huyu mtu hayuko tayari kuolewa, wala
msijaribu kumlazimisha aoelewe – pamoja na kwamba umri wake ni mkubwa.
Usijaribu kumsukuma kwenye maamuzi ya kuolewa maana hayuko tayari
kuolewa, akiingia kwenye ndoa atakwenda kuleta shida tu!
Ndio maana ninakuuliza swali, je uko tayari kuoa au kuolewa? Lina
vipengele vingi vya kulitazama, na linabadilisha vitu vingi sana.
Mwingine unakuta ni msichana, wazazi wake ndio wanamtegemea karibu
katika kila kitu. Mimi ninakuambia kabla hujafikiria kuoa au kuolewa,
fikiria hilo swali. Kwa sababu ukiishaolewa tu biblia inakuambia wasahau
watu wa nyumbani mwa wazazi wako (Zaburi 45:10). Sasa haimaanishi
usiwasaidie, ila maana yake ni kwamba huwezi ukawasaidia tena ‘moja kwa
moja’ kama ulivyokuwa unawasaidia zamani. Ni vitu lazima ujadiliane na
mume wako juu ya kuwasaidia wazazi wenu wa pande zote mbili – maana mna
mipango yenu sasa.
Na inawezekana labda umeoa au umeolewa kwa kijana ambaye hana mzigo
na wazazi wake kabisa, kila mtu anaishi kivyake vyake kama simba
porini, suala la kusaidia wazazi hana ndani ya moyo wake. Wewe umekuwa
na huo mzigo, wazazi wako wamekulea, umefika mahali umeanza kazi, sasa
na wewe unawatunza hatua kwa hatua, siku unaolewa yule baba anasema basi
usiwatunze tena, – fikiri hilo.
Litakuwa linakuumiza kila siku jinsi wazazi wako wanavyopata shida.
Utafika mahali utakuwa unachukua vitu kisiri siri unapeleka kwa wazazi,
na hiyo ina shida yake pia. Kwa hiyo kabla hujakubali kusema mimi nataka
kuolewa, fikiri kwanza na kuomba, maana ndoa inakwenda kukubadilishia
mambo yako mengi.