Sipho Makhabane |
Sipho Makhabane, Mwimbaji mwenye jina kubwa
barani Afrika, ambapo umaarufu wake umepatikana kutokana na uwezo wake
wa kutunga nyimbo zenye ujumbe wa hali ya juu wa kumsifu na kumuabudu Mungu.
Kutokana na uwezo wake huo mashabiki wengi wa muziki wa Injili wamekuwa wakimfananisha na wanamuziki mahiri kama Joyous Celebration ama Sfiso Ncwane.
Makhabane mwenye umri wa miaka 45 ni mmoja wa magwiji wa uimbaji nchini Afrika Kusini, na ameshiriki katika shughuli mbalimbali za kiroho na kijamii.
Kutokana na kutingwa na shughuli zake mwaka 2010 alitangaza kuachana na kazi ya kuimba, hata hivyo mwaka 2012 aliushangaza ulimwengu kwa kuachia albamu yake mpya iliyokubalika na watu wengi.
Historia ya maisha yake inaonesha kuwa ni mtu aliyekulia katika muziki huo, na kutokana na ugumu wa maisha uliokuwa ukiikabili familia yake, Makhabane alilazimika kuacha shule akiwa darasa la tano na akiamua kufanya kazi katika shamba la miwa la Kaaruls huko Mpumalanga kama ilivyokuwa kwa mwimbaji mwingine nguli Rebecca Malope.
Makhabane alifanya hivyo walau aweze kupata fedha ya kuwasaidia
wazazi wake pamoja na ndugu zake ambao walikuwa wakimtegemea yeye.
Alipotimiza miaka 17, alihamia kwenye kazi za ujenzi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Afrika Kusini ya Kruger.
Akiwa huko alifanya kazi ya kuwasaidia mafundi waliokuwa wakijenga nyumba kambini hapo na alipotimiza miaka 21 alikuwa tayari na ujuzi wa kutosha katika kazi ya ujenzi na akapata kazi katika eneo la Pienaar.
Mwaka 1986, Makhabane alipata ofa nzuri katika kampuni ya Telkom kama fundi, lakini katika kuhangaika kwake alijikuta akiishia kwenye muziki wa Injili.
Hata hivyo hakuwa akijua kuwa nyota ya mafanikio yake ilikuwa kwenye huduma hiyo ya uimbaji na badala yake alikuwa akifanya muziki wa kujifurahisha zaidi na si wa biashara.
Mwaka 1990, wakati huo akiwa na umri wa miaka 25, Makhabane alifunga ndoa na binti aliyekuwa na umri wa miaka 18.
Baada ya hapo ndipo alianza kazi ya kununua na kuuza kazi za muziki ndani na nje ya nchi ya Afrika Kusini.
Kutokana na kuona muziki umeanza kuingia kwa kasi kwenye akili yake, Makhabane aliamua kuachana na kazi ya ufundi mitambo ya simu na kujikita kwenye muziki.
Katika kuhakikisha anapunguza wizi wa kazi zake, mwanamuziki huyo aliamua kusambaza kazi zake mwenyewe, lakini kikwazo kwake kikawa ni namna ya kuwavutia wasambazaji waliokuwa tayari kununua kazi kutoka kwake.
Kazi yake iliyomfanya kukubalika ilianza kusikika kwenye redio ya Swazi ambayo inajulikana zaidi kwa jina la Ligwalagwala FM, ambapo kibao kilichomtambulisha ni kile cha Ngitinikela Kuwe.
Hatimaye mwaka 1996, Makhabane aliamua rasmi kuifanya kazi hiyo
ya muziki wa Injili na kuacha kazi aliyokuwa akiifanya kwenye kampuni ya
simu.
Mwaka huo huo aliachia album yake iitwayo “Yek’intokozo” wimbo ambao mpaka leo unakumbukwa na mashabiki wake kwani ndio ulimtambulisha vema, ingawa tayari alishatoa album nyingine mbili miaka ya 1993 hadi 1999 za ‘Thum'umlolo” na “Jesu Uliqhawe”.
Mwaka 1998, kupitia kampuni ya CCP Records aliachia album yake ya nne iitwayo “Uyigugu” iliyofanya vema kabla ya mwaka uliofuata kuachia nyingine iitwayo “Makadunyiswe,”.
Mwaka 2001, alifyatua album ya Calvary ambayo iliuza kufikia kiwango cha juu na mwaka uliofuata (2002), aliachia albamu nyingine ya ‘Akukhalwa’ ambayo ilitikisa kama album ya “Yek’intokozo,” akiuza zaidi ya nakala 70,000.
Mwaka 2003, Makhabane aliachia album ya ‘Moya wami’ ambayo pia iliuza zaidi ya nakala 70,000.
Kutokana na umahiri wake, Makhabane ameweza kushirikishwa katika album na waimbaji wakongwe wa nchini kwake kama Jabu Hlongwane, Marehemu Vuyo Mokoena, Lundi, Hlengiwe Mhlaba na wengine wengi.
Pia akiwa nyuma ya mafanikio ya waimbaji lukuki kama Hlengiwe Mhlaba, Ncandweni Christ Ambassadors, Shongwe na Khuphuka Saved Group.
Nje ya uimbaji, Makhabane ni mtayarishaji wa kazi za muziki wa injili akiwa daraja la waimbaji wengine kutokana na kuwika vilivyo kupitia kazi zao zilizoandaliwa na gwiji huyo.
Sipho Makhabane ni mmoja kati ya Waimbaji watakaohudumu siku ya Tamasha la Pasaka la Mwaka huu litakalofanyika Uwanja wa Taifa.